By Mwanahiba Richard
(email the author)
CHAMA cha Waamuzi wa Soka Tanzania (FRAT),
kimewasimamisha kazi waamuzi wanane wanaohisiwa kujihusisha na vitendo
vya rushwa ikiwa ni mpango wa kutokomeza rushwa kwenye soka.
Mwenyekiti wa FRAT, Nassoro Mwalimu, aliliambia
Mwanaspoti kuwa, kumekuwapo na malalamiko mengi, hivyo wameamua kuchukua
hatua za kuwasimamisha na uchunguzi ukikamilika wanaweza kuwafungia
kabisa.
Jambo hilo limeungwa mkono na Rais wa TFF, Jamal
Malinzi, ambaye aliwasisitiza wajumbe wa Mkutano Mkuu kuwa wawazi na
kushirikiana na shirikisho hilo kumpelekea wanaojihusisha na rushwa ili
wachukuliwe hatua kali za kisheria.
“Nampongeza Malinzi akiendelea kuchukua hatua kwa
atakayepatikana na tuhuma za rushwa, hii isiwe kwa mpokeaji tu, bali na
mtoaji. Kuna waamuzi ambao tumewasimamisha kwa hisia za kujihusisha na
vitendo hivyo huku uchunguzi ukiendelea, mmoja ameondolewa kabisa na
alifikia hatua nzuri ya kuchezesha Ligi Kuu.
“Tuna waamuzi 18 wenye beji za Fifa, kati yao sita
ni wanawake, naamini umakini wa kuwapata wengine utaendelea rushwa
ikipigwa vita, ila viongozi wa klabu ambao ndio vichocheo zaidi nao
waadhibiwe,” alisema.
Aliitaka TFF kuchukua hatua kali pia kwa
wanaowapiga waamuzi timu zao zinapofungwa. “Hii ni hatari waamuzi,
wanapigwa, wanaumizwa, ipo siku watauawa, TFF bado hawajachukua hatua
kwa matukio haya,” alilalamika.
Naye Malinzi alisema: “Sikubaliani na suala hili,
naomba ambaye ameona kuna rushwa mahali iwe kwa waamuzi kupokea rushwa
au kiongozi kutoa au mchezaji kupokea anitaarifu ili mhusika apewe
adhabu itakayokuwa mfano, hatuwezi kuvumilia rushwa itutawale katika
soka.”
0 comments:
Post a Comment