Wakati wenyeviti wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa) pamoja na kamati zake za kitaalamu wanakutana Zanzibar
kutafuta suluhu kuhusu mgawanyo nafasi za kugombea katika uchaguzi mkuu
ujao, kuna uwezekano mkubwa vyama hivyo kuteua mgombea urais kutoka
Chadema.
Tovuti hii inaweza kuripoti kwa uhakika kuwa
uwezekano huo unatokana na vigezo vinavyotumiwa na vyama hivyo
kusimamisha mgombea mmoja kwa kila jimbo na kwenye nafasi ya urais
ambavyo vinaipa Chadema nafasi hiyo dhidi ya vyama vingine katika umoja
huo ambavyo ni CUF, NCCR-Mageuzi na NLD.
Vigezo hivyo ni matokeo ya uchaguzi 2010, idadi ya
madiwani kwa kila chama, matokeo ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa
Desemba mwaka jana, mtandao wa chama nchini na nguvu ya mgombea iwapo
Chadema kitamsimamisha katibu mkuu wake, Dk Willibrod Slaa kwa mara ya
pili.
Taarifa zilizolifikia kutoka ndani ya
kamati ya ufundi ya Ukawa zinasema pamoja na kuwapo mvutano katika
baadhi majimbo Tanzania Bara, kwa upande wa Zanzibar hakuna tatizo hilo,
jambo linaloipa CUF nafasi ya moja kwa moja kwenye ubunge, uwakilishi
na hata urais wa visiwa hivyo.
Kwa mujibu wa habari hizo, nafasi nzuri ya CUF
kupita moja kwa moja Zanzibar bila ushindani ndani ya Ukawa, inatoa
fursa kwa upande wa Bara, kwa vyama vilivyosalia kupitishwa kuwania
urais wa Muungano.
Hata hivyo, kwa vigezo vilivyotajwa hapo juu,
Chadema ndiyo inakuwa na nafasi isiyo na kipingamizi kutokana na rekodi
vyama vilivyosalia Bara.
Katika Uchaguzi Mkuu wa 2010, Chadema
kilimsimamisha Dk Slaa na aliibuka wa pili baada ya Rais Jakaya Kikwete
akiwa na kura 2,271,941 (asilimia 26.34) akifuatiwa na Profesa Ibrahim
Lipumba aliyepata kura 695,667 (asilimia 8.06) na Hashim Rungwe wa
NCCR-Mageuzi aliyepata kura 26,388 (asilimia 0.31). NLD haikusimamisha
mgombea urais.
Kwa upande wa majimbo yaliyotokana na uchaguzi wa
2010, Chadema kiliongoza kikiwa na wabunge 24 (wote kutoka Bara), CUF 23
(wawili kutoka Bara, 21 Zanzibar) na NCCR-Mageuzi wanne (wote wa Bara).
Katika rekodi za uchaguzi wa mitaa zilitolewa na
Tamisemi kabla ya chaguzi za marudio, Chadema ilipata mitaa 980,
ikifuatiwa na CUF (mitaa 266), NCCR Mageuzi (28) na NLD mtaa mmoja.
Kwa upande wa vijiji, Chadema kilishinda vijiji 1,754, CUF (516),
NCCR-Mageuzi (67) na NLD vijiji viwili.
Hata kwa upande wa vitongoji Chadema kiliviongoza
vyama hivyo kwa kupata vijiji 9,145 kikifuatiwa na CUF (2,561),
NCCR-Mageuzi (339) na NLD vitongoji viwili.
Tayari NCCR-Mageuzi kimeonyesha nia ya kumteua Dk
George Kahangwa kuwania urais wakati Mwenyekiti wa NLD, Dk Emmanuel
Makaidi alikaririwa na gazeti hili hivi karibuni akisema kuwa chama
chake kimekwishamteua kuwania urais, hivyo jina lake litapelekwa Ukawa
kushindanishwa.
Mvutano mkali
Hali ikiwa hivyo, wajumbe wa Ukawa leo watakumbana na wakati
mgumu wa kufikia maridhiano ya kugawana majimbo 19 kutokana na taarifa
za kuwapo mvutano mkali wa pande zote za vyama husika.
Wanaokutana leo ni wenyeviti wa vyama, makamu wenyeviti, makatibu na wajumbe wa sekretarieti kutoka vyama hivyo.
Kabla ya kuanza kikao cha leo, jana asubuhi
wajumbe 16 wa Kamati ya Ufundi walikutana na baadaye jioni wenyeviti wa
umoja huo wakawa na kikao cha awali, ikiwa ni sehemu ya vikao vya hatua
za kugawana maeneo ya kuwania ili kutoa ushindani na hatimaye ushindi
dhidi ya CCM.
Chanzo cha habari kutoka ndani kimelieleza Mwananchi kuwa NLD nayo imeongeza mvutano ikihitaji majimbo matano.
Wiki iliyopita, gazeti hili liliandika kuwa Ukawa
ilikuwa imekamilisha kazi ya ugawaji wa majimbo 170 lakini ukawapo
mvutano katika majimbo 19 ambayo vyama zaidi ya kimoja vilikuwa
vinayataka.
Majimbo hayo ni Segerea, Kinondoni, Kigamboni na
Ukonga ya Dar es Salaam, Morogoro Mjini na mengine ya mikoa ya Mwanza,
Shinyanga na Kagera.
“Mvutano ni kwamba, kuna vyama vinavyotaka
uwakilishi tu wa majimbo hayo lakini kiukweli yanaweza kupotea bure tu
endapo vitakabidhiwa. Wengine wanataka kuangalia zaidi ushawishi wa
chama ndani ya jimbo husika ila wengine wanapinga, wakisema umoja huo
hautakuwa na sababu kama watakosa uwakilishi,” kilieleza chanzo hicho.
“NLD wanahitaji majimbo matano, CUF na Chadema
wanavutana zaidi, ila NCCR-Mageuzi wameonekana kushtushwa sana na hali
hiyo,” kilisema chanzo kingine kutoka NCCR-Mageuzi.
Chanzo kingine kilieleza kuwa kamati ya wataalamu
ilishakamilisha kazi yake ya uchambuzi wa majimbo hayo na kuwasilisha
taarifa zake lakini kuna upinzani mkali ambao umeendelea kuibuliwa na
wajumbe wa umoja huo.
“Kikao cha leo kinaashiria kuwa na mvutano,
ninaamini kuna uwezekano wa kufikia mwafaka lakini ikishindikana kabisa
kwa leo lazima vitaandaliwa vikao vingine,” kilieleza chanzo kingine.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Wataalamu,
Benson Kigaila (Chadema) alisita kuweka wazi juu ya mvutano uliopo huku
akibainisha kuwa maridhiano yatapatikana.
Kigaila alisema kikao cha leo kina nafasi kubwa ya kumaliza mvutano huo na kueleza Watanzania juu ya mwelekeo wa safari yao.
Kigaila ambaye pia ni Mkurugenzi wa Oganaizesheni ya Mafunzo na
Usimamizi wa Kanda wa Chadema, alisema: “Kwa sasa siwezi kueleza
chochote kwani vikao ndiyo vinafanyika kwa sasa, lakini naomba vikao
vikishamalizika viongozi wetu watazunguza tu,” alisema.
Alipoulizwa juu ya NLD kuhitaji majimbo matano,
Kigaila alikiri kuwa kweli wanataka mgawo wa majimbo lakini alikataa
kutaja idadi yake.
“NLD wanayo haki kama vyama vingine, kwa nini
wasipate? Watapata, lakini kuna taarifa sahihi zitakazoelezwa baada ya
kikao cha leo.”
Jumanne wiki hii, Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Bara,
Magdalena Sakaya alilieleza gazeti hili kuwa kikao hicho kitakuwa na
ajenda ya kukusanya maoni na mapendekezo ya wanachama, kujadiliana kwa
pamoja ili kufikia muafaka wa majimbo hayo.
Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Mosena Nyambabe
alisema katika hatua za kutafuta maridhiano ya majimbo hayo, vyama vyote
vinapaswa kutambua kila nafasi ya chama kilichoshiriki kwenye
makubaliano ya Ukawa.
“Tukifuata kanuni, nadhani kuna vyama ambavyo
havitakuwa na nafasi Ukawa na haitakuwa na maana ya kuungana, kwa hivyo
lazima busara itumike zaidi. Haiwezekani chama fulani kilazimishe
kuchukua majimbo mengi kuliko kingine,” alisema Nyambabe.
Alipoulizwa kuhusu utata katika mgawanyo wa
majimbo, Dk Slaa alisisitiza kumalizika kwa mvutano kutokana na busara
za viongozi wa vyama hivyo.
0 comments:
Post a Comment