MANCHESTER City imepangwa kuikabili Barcelona katika hatua ya 16 bora ya Ligi ya soka ya Mabingwa Ulaya kwa mwaka wa pili mfululizo. Chelsea itacheza na Paris St-Germain, na Arsenal imepangwa dhidi ya Monaco katika mapambano hayo yatakayochezwa Februari na Machi mwakani.
Mabingwa watetezi, Real Madrid wataikabili Schalke 04, huku timu iliyopoteza fainali ya msimu uliopita, Atletico Madrid ikikabiliana na Bayer Leverkusen.
Bayern Munich itacheza na Shakhtar Donetsk, Juventus itaivaa Borussia Dortmund na Basel imepangwa na Porto. Mechi za kwanza zimepangwa kufanyika kati ya Februari 17, 18, 24 na 25 na marudiano ni Machi 10, 11, 17 na 18.
Manchester City ilifuzu kwa bahati, ikihitaji ushindi katika mechi ya mwisho dhidi ya AS Roma kufuzu, lakini ilimaliza ikiwa nyuma ya Bayern Munich hivyo kuwa na maana kwamba itapangiwa miamba ya Ulaya kama vile mabingwa mara nne, Barcelona ya Hispania. Katika mtoano msimu uliopita, timu ya Catalunya ilishinda kwa jumla ya mabao 4-1.
Chelsea iliyomaliza mshindi wa kundi mbele ya Schalke 04 ya Ujerumani, imepangwa kuikabili Paris St-Germain kwa mwaka wa pili mfululizo, baada ya kuwatoa mabingwa hao wa Ufaransa kwa bao la dakika za mwisho katika robo fainali mwaka jana.
Kuna utamu zaidi katika pam-bano hilo kwani Chelsea imemuuza beki wake, David Luiz kwa PSG kwa ada inayoaminika kuwa pauni milioni 40 msimu huu. Arsenal iliyomaliza nyuma ya Borussia Dortmund katika kundi lao, imepangwa dhidi ya timu iliyowahi kufundishwa na kocha Arsene Wenger kuanzia mwaka 1987 hadi 1994.
Monaco ilifunga mabao manne tu katika kundi lake, lakini ilimaliza ikiwa kileleni. Mkurugenzi wa Soka wa Manchester City na mchezaji wa zamani wa Barcelona, Txiki Begiristain aliiambia Sky Sports News: “Kila pambano katika ratiba hii linafanana. Ni la kuvutia, kwa hiyo tunajiandaa kwa hilo.
“Tunajiamini sana kwa jinsi tulivyofuzu kwa kuishinda Bayern Munich nyumbani na Roma ugenini, kwa hiyo wachezaji wanajituma sana kujiweka fiti na kujiamini kwa ajili ya mechi hizo.
“Tumeimarisha kikosi chetu kuanzia msimu uliopita na tunao wachezaji mahiri mbele.” Katibu Mkuu wa Klabu ya Arsenal, David Miles alisema: “Wakati ratiba ikiendelea kupangwa, timu nyingi kubwa zilikwishatoka.
Tuna furaha kupangwa hapo. “Tunajiandaa kwa hamu kubwa kwa mechi hizo. Tumepangwa na baadhi ya timu kubwa Ulaya kwa miaka kadhaa iliyopita, lakini hatutadharau. Monaco imejipatia haki ya kuwa katika hatua hii.
“Mashabiki wana matarajio makubwa, na itakuwa jambo zuri kuvuka hatua ya 16 na kuendelea kutoka hapo.” Katibu Mkuu wa Chelsea, David Barnard alisema: “PSG inafahamika kwetu kwani tumecheza nao katika robo fainali mwaka jana na wanaye David Luiz ambaye naye anacheza kwao. “Ni ratiba nzuri pia kwa mashabiki wetu.
Timu zote mbili zina vikosi tofauti na vile vya mwaka jana, kwa hiyo kama ingekuwa PSG au mwingine yeyote, ingekuwa hali ile ile.” Aidha, katika Kombe la Europa hatua ya 32 bora, Tottenham imepangwa kuikabili Fiorentina, Everton dhidi ya Young Boys, Celtic itacheza na Inter Milan wakati Liverpool iliyotolewa katika Ligi ya Mabingwa, itacheza na Besiktas.
Mabingwa watetezi wa kombe hilo, Sevilla ya Hispania imepangwa na Borussia Monchengladbach. Ratiba kamili ya timu za hatua ya 16 bora Ulaya ni: Paris St-Germain v Chelsea Manchester City v Barcelona Bayer Leverkusen v Atletico Madrid Juventus v Borussia Dortmund Schalke 04 v Real Madrid Shakhtar Donetsk v Bayern Munich Arsenal v Monaco Basel v Porto






0 comments:
Post a Comment