09:05:00
No comments
MTIHANI wa Taifa wa Kidato cha Nne na Mtihani wa Maarifa wa mwaka 2014 unatarajiwa kufanyika nchini kote kwa takribani siku 20 kuanza keshokutwa huku idadi ya watahiniwa ikiwa pungufu ikilinganishwa na watahiniwa wa mwaka jana.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Jenista Mhagama alisema idadi hiyo imepungua kutokana na kurudishwa kwa utaratibu wa mtihani wa Kidato cha Pili ambao waliopata alama chini ya kiwango walirudishwa nyuma.
Alisema mtihani huo umetanguliwa na mtihani wa vitendo wa somo la Mapishi na Lishe uliofanyika kuanzia Oktoba 6 hadi 23.
“Jumla ya watahiniwa walioandikishwa kufanya mtihani ni 297,488 ambapo kati yao 245,030 ni watahiniwa wa shule na 52,458 ni watahiniwa wa kujitegemea. Waliojiandikisha kufanya mtihani wa maarifa ni 14,723,” alisema.
Alisema kati ya watahiniwa wa shule 245,030 walioandikishwa, wavulana ni 132,244 sawa na asilimia 53.97 na wasichana 112,786 sawa na asilimia 46.03.
Alisema watahiniwa hao wa shule wa mwaka 2014 ni pungufu ya watahiniwa 122,369 sawa na asilimia 33.3 ikilinganishwa na watahiniwa wa shule 367,399 wa mwaka 2013.
Aidha alisema kati ya watahiniwa hao, 51 ni wasioona wakiwemo wavulana 37 na wasichana 14 ambapo jumla ya watahiniwa wenye uono hafifu ambao huhitaji maandishi makubwa kwa ujumla ni 356.
Alisema watahiniwa wa kujitegemea walioandikishwa ni 52,458 ambapo wanaume ni 25,774 sawa na asilimia 49.13 na wanawake 26,684 sawa na asilimia 50.87 ambapo pia wapo watahiniwa wasioona 15 kati yao wanaume ni 11 na wanawake 14.
“Watahiniwa wa kujitegemea walioandikishwa mwaka huu ni pungufu ya watahiniwa 8,049 sawa na upungufu wa asilimia 13.3 ikilinganishwa na watahiniwa 60,507 walioandikishwa mwaka 2013. Upungufu huu unatokana na hali za watahiniwa kwa kuwa ni wa kujitegemea,” alisema.
Alisema kufuatia maoni mbalimbali ya wadau wa elimu, maboresho yamefanywa katika uendeshaji wa mitihani kwa watahiniwa wa kujitegemea ambapo kuanzia mwaka huu watahiniwa wa kujitegemea watafanya karatasi mbili kwa kila somo walilojisajili badala ya karatasi moja waliyokuwa wakifanya awali.
“Karatasi ya pili limeongezwa kwa lengo la kuwafanya watahiniwa wa kujitegemea kuwa na alama zitakazounganishwa na alama za karatasi ya kwanza kwa uwiano maalumu uliowekwa kama inavyofanyika kwa watahiniwa wa shule,” alisema.
Mhagama alisema jumla ya watahiniwa wa Mtihani wa Maarifa walioandikishwa ni 14,723 wakiwemo wanaume 5,940 sawa na asilimia 40.34 na wanawake 8,783 sawa na asilimia 59.66 ambapo nao ni pungufu ya watahiniwa 3,491 sawa na asilimia 19.1 ikilinganishwa na watahiniwa 18,214 walioandikishwa mwaka jana.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment