WAKALA WA SHETANI -22

Author

#Wakala_wa_Shetani - 22-...

Taratibu kama komandoo wa kivita aliyekuwa akiwatoroka maadui, alifanikiwa kuwatoroka baada ya kuwaona kwa mbali.
Alielekea upande wa mashariki kuwakimbia adui zake. Baada ya mwendo mfupi aliamua kupumzika kwani mwanaye alianza kutetemeka kwa baridi.
Alijitahidi kumkumbatia lakini haikusaidia kwa vile naye mwili wake ulikuwa wa baridi la muda ule na ubaridi wa maji uliufanya mwili wake uanze kufa ganzi.

#SASA_ENDELEA...

Kila dakika hali ya mwanaye ilibadilika na kuonesha kupoteza uwezo wake wa kawaida. Hali ile ilimfanya Ng'wana Bupilipili kuchanganyikiwa na kuona jinsi alivyokuwa akimpoteza mwanaye huku akimuona.
Baada ya kuanza kuhema kwa shida, alijilaumu kwa kukaidi ombi la shoga yake Bupe la kumuacha mtoto kambini. Aliamini kama mwanaye atakufa yeye ndiye atakayebeba lawama kwa vile hali ile isingemtokea kama angemuacha mtoto kambini.
Moyoni alijuta na kuona kama mwanaye atakufa, basi kwake yeye hakuwa na sababu yoyote ya kupoteza maisha ya mume wake, kupoteza maisha ya wanakijiji na sababu ya yeye kuteseka vile.
Hali ya mwanaye ilizidi kuwa mbaya hata akawa haoneshi kupumua. Aliamini kabisa njia iliyokuwepo ya kumsaidia mtoto wake ni kujisalimisha kwa wale askari ambao wangeweza kuokoa maisha ya mwanaye kama wakifanikiwa.
Kwake hakuona hatari yoyote kama atafungwa au kunyongwa na mwanaye kubakia salama japokuwa hakujua mtoto wake ataishi maisha gani.
Alimchukua mtoto wake na kumuweka begani na kuwafuata wale askari waliokuwa wakimsaka huku akitokwa na machozi kwa uchungu wa mwanaye. Askari waliokuwa wamejipumzisha walishtuka kumuona mwanamke akiwa amembeba mtoto begani huku akionekana ametota kwa maji.
Wote walimtazama na kujiuliza anatoka wapi. Alipofika mbele yao alimbwaga mtoto wake mbele yao huku akisema:
"Haya mleni nyama sasa," alisema huku akifoka kwa sauti ya kilio.
"Mbona hatukuelewi, tumle nyama kivipi?" askari mmoja alimshangaa.
"Si mlikuwa mnataka kuona mwanangu anakufa? Haya amekufa furahini, haya nipelekeni mkaninyonge sasa."
Mkuu wa oparesheni hiyo alimchukua haraka yule mtoto na kugundua tatizo lake ni baridi yabisi, kwa haraka walitengeneza joto ambalo lilimsaidia mtoto kurudi katika hali ya kawaida kisha alichukuliwa na kupelekwa kwenye kituo chao cha huduma ya kwanza kabla ya kumpeleka hospitali kwa matibabu zaidi.
Wakati huo Ng'wana Bupilipili alikuwa ame wekwa chini ya ulinzi baada ya kugundulika ndiye adui aliyekuwa akitafutwa. Hakutaka kuwabishia.
Walimshangaa mtu ambaye walikuwa na wasiwasi huenda ni mkakamavu tena mwenye mafunzo ya kijasusi, kumbe ni mwanamke. Mkuu wa oparesheni ile alishtuka na kuuliza mara mbili.
"Ndiye huyu?"
"Ndiyo mkuu," alijibu askari aliyekimbiwa na Ng'wana Bupilipili.
"Sasa mbona anaonekana tofauti na sifa nilizosikia, nilijua ni mkakamavu mwenye mwili wa mazoezi."
"Mkuu usimtazame kwa macho, ni zaidi ya gaidi, mwanamke huyu kama alivyoniahidi alipania kukimaliza kijiji kizima."
"Eti mama ni kweli?" Mkuu alimuuliza kwa upole.
"Maswali ya nini, si mmeshanikamata? Ninyongeni basi au niueni kwa risasi si mmekuja na bunduki kuniua?" Ng'wana Bupilipili alisema huku akilia kwa hasira.
"Hatuwezi kukunyonga kwa vile sisi si mahakama, la muhimu maelezo yako yanaweza kusababisha tukuache huru."
"Hayatasaidia kitu kwa vile maelezo ya awali nimueleza huyu kaka, lakini mliamua kunisaka kama gaidi. Mmefanikiwa kunikamata nipelekeni nikanyongwe ili mfurahi. Lakini naapa Mungu atalipa kwa kila roho isiyo na hatia," Ng'wana Bupilipili alizungumza kwa uchungu huku akimwaga machozi.
"Serikali haipo kwa ajili ya kumuonea mtu bali kuhakikisha kila mwanadamu anaishi kwa uhuru na amani bila kuvunja sheria," mkuu alionesha ustaarabu kwa kujibu kwa upole.
"Kwa vile wao wamekufa ndiyo serikali imeliona hilo, na sisi tuliopoteza roho za watoto wetu na waume zetu serikali yetu ni ipi?"
"Mmepotezaje hizo roho?"
Ng'wana Bupilipili alirudia maelezo ya mauaji ya albino Kijiji cha Nyasha na kifo cha mumewe, ikiwemo kuporwa mali zao na wanakijiji cha Nyasha.
Baada ya kumsikiliza mkuu alisema:
"Bado hukutakiwa kuchukua sheria mkononi kwa vile kuna vyombo vya sheria."
"Mmh! Vyombo vya sheria kwa vile wamekufa wao, mbona vifo vya watoto albino hamkuwahi kuja hata siku moja ila hivi ndiyo mmetengeneza mtego wa kuninasa, ndiyo maana nikasema nipelekeni mkani.ni..ni..ni.. Haaa!"
Ng'wana Bupilipili alishika chini ya titi la mkono wa kushoto baada ya kusikia mchomo mkali kwa ndani kama kumepasuka.
Maumivu yalikuwa makali na kuhisi kama mbavu zinagusana. Alipiga kelele za maumivu na kuanguka chini akiwa amepoteza fahamu.
***
Ng'wana Bupilipili baada ya kurudiwa na fahamu, alipofumbua macho alijiona yupo ndani ya hema amelazwa chini kwenye turubai lililokuwa limetandikwa na pembeni yake alikuwepo mwanaye Kusekwa ambaye alikuwa amepitiwa na usingizi.
Alijikuta akijiuliza pale ni wapi na amefikaje, alimuangalia mwanaye ambaye alikuwa amelala huku akionekana yupo katika hali ya kawaida. Ili kuhakikisha mwanaye ni mzima aliweka sikio kifuani ambako alimsikia akihema vizuri.
Akiwa bado anamuangalia vizuri mwanaye, alishtushwa na sauti za watu waliokuwa wakisogea kwenye hema lile huku wakizungumza.
"Huenda amesharejewa na fahamu, ngoja tukamuangalie, yule mwanamke simuamini kabisa."
"Lakini mbona sifa za yule mwanamke hazilingani naye? Huenda kuna wahusika wakuu na yeye ni mtu wa kutumwa tu," askari mmoja alisikika akisema.
Ng'wana Bupilipili alipowasikia wamekaribia alirudi sehemu aliyokuwa amelala na kujilaza kana kwamba hajarudiwa na fahamu kwa kujitahidi kuhema kwa taratibu sana. Askari wale waliingia hadi ndani na kumkuta amelala, hata kuhema kwake hakukuwa kwa kawaida.
"Bado hajaamka twende zetu," alisema mmoja baada kuwa na uhakika mtuhumiwa bado amelala.
"Sasa tutaondoka saa ngapi?"
"Mkuu amesema tumsikilizie kwa muda zaidi ya hapo tutambeba na kuondoka naye."

Itaendelea....

0 comments:

Post a Comment