WAKALA WA SHETANI -07

Author

#Wakala_wa_Shetani - 7

...ILIPOISHIA;
"UNAJUA hapa kitongojini kwetu aliyekuwa na ujauzito wa kujifungua ni mke wa Mathayo Ngw’ana Bupilpili." SASA ENDELEA...
“Eeh.”
“Unaitikie eeh, nilikuambia nini baada kukutana na Ngw’ana Bupilipili?” Mama Sabina alimkazia macho mumewe ambaye alionesha hayupo makini.
“Ooh! Nimekumbuka, ina maana mtoto huyo atakuwa wa Ngw’ana Bupilipili?”
“Huo ndio wasiwasi wangu mkubwa, japokuwa sina uhakika.”
“Sasa kama ni mtoto wa Ngw’ana Bupilipili kwa nini amfiche, una uhakika anaweza kuwa wake?”
“Sina uhakika, lakini sasa hivi nakwenda kujifanya naomba moto ili nijue mtoto aliyelia anatoka nyumba ile.”
“Lala mke wangu, achana nao.”
“Hapana mume wangu, kutakuwa na kitu, kama ni kweli kwa nini wamfiche?” alihoji mama Sabina.
Mama Sabina alinyanyuka kitandani alipokuwa amekaa kwa ajili ya kulala. Alitoka na kumwacha mumewe akimsubiri mkewe alipokwenda kufanya uchunguzi wake.
Alikwenda hadi kwa jirani yake Ngw’ana Bupilipili, alipofika aliwasikia wakizungumza mtu na mkewe ndani.
“Mmh, mtoto huyu alitaka kutuumbua,” alimsikia Mathayo akizungumza.
“Alikuwa amekojoa ndo maana kalia, sijui sauti yake imefika mbali?”
“Mmh, sidhani, lakini watu wote wamo ndani hawawezi kujua nani mwenye mtoto asubuhi.”
“Mmh, afadhali.”
Mama Sabina hakutaka kuwashtua, alirudi hadi ndani mwake na kumweleza mumewe aliyosikia kwa jirani zao.
“Sasa mke wangu kwa nini wanafanya siri, kwani mtoto wao ana nini?”
“Labda albino?”
“Mmh! Inawezekana maana mvua ya leo si ya kawaida, haijawahi kutokea kijijini.”
“Kwa hiyo?”
”Hiyo kazi niachie nitaifikisha kwenye kamati ya kijiji, kama ni kweli tutaweka ujirani pembeni, hawezi kutuletea balaa kama hili, hebu ona hasara iliyoingia. Tumepoteza mifugo kibao.”
“Na kweli mume wangu, lazima tuwashtaki hasa aliyeniuma ni yule ng’ombe mjamzito aliyekuwa na mapacha.”
“Tulale mke wangu, tutayajua yote asubuhi.”
Walizima taa na kujilaza.
Kabla ya kuanza kulala mama Sabina alikuwa na wazo, alimshtua mumewe aliyekuwa amegeuka kumpa mgongo ili aanze kuutafuta usingizi.
“Mume wangu kabla ya kulala nilikuwa na wazo.”
“Lipi tena mke wangu?”
“Kuhusu jirani yetu.”
“Mmh, ulikuwa na wazo gani?”
“Nilikuwa nataka kesho alfajiri niwahi nijifanye naenda kuomba moto, kisha niwaeleze kuwa nimemsikia mtoto kisha niliwasikia wanasema.”
”Wazo lako ni zuri, lakini kama mtoto ni albino siamini kama watakubali zaidi ya kukataa.”
“Sasa unanishauri nini?”
“Wee waache tu ili tuwashitukize.”
“Lakini mume wangu kama mkikuta mtoto si albino tutajipa picha gani kwa jirani yetu kama sio uhasama wa kisasi.”
“Usemalo ni kweli, basi fanya ulivyofikiria tutajua tufanye nini?”
“Haya, tulale.”
Kila mmoja aligeukia kwake na kuvuta shuka.
****
Siku ya pili Mathayo na mkewe walidamka alfajiri na kukusanya vitu muhimu vya kutumia huku wakiendelea kuomba Mungu awaonee huruma kwa ajili ya kukiponya kiumbe kile.
Baada ya kuandaa kila kitu walitoka taratibu na kushika njia ya shambani japo ilikuwa ikitisha sana kutokana na hali ya hewa ya ukungu iliyotanda alfajiri ile.
Waliondoka na kurudi shambani kwao, walikuta maji yamepungua sehemu nyingine na kuwafanya wavuke bila kuingia ndani ya maji ambayo yalikuwa ya baridi kali.
Walifanikiwa kufika hadi sehemu ya pangoni ambayo maji yote yalikuwa yametoka. Ng’wana Bupilipili alimuandalia mtoto sehemu nzuri na kumlaza kisha na yeye kujilaza pembeni yake huku akimwacha mumewe aende shambani kufanya usafi na matengenezo ya sehemu zilizoharibika.
Mathayo alikwenda hadi shambani na kuanza kazi ya kurekebisha baadhi ya sehemu zilizozolewa na mvua ambayo iliharibu mazao mengi katika mashamba.
Kitu cha ajabu pamoja na mvua kunyesha sana, shamba lao tu ndilo ambalo mazao yao yalipona. Hata mifugo yake nayo ilipona tofauti na majirani zake ambao mashamba yao mengi yaliharibiwa na mvua.
****
Mama Sabina aliyepanga kuamka alfajiri kwenda kuwaona Mathayo na mkewe, baada ya kuamka alikuwa amechelewa. Alipishana dakika dano tu, wakati yeye anaamka wao wanaondoka tena kimyakimya. Alipofika kwenye nyumba ya jirani yake alijua bado amelala.
Alikwenda hadi kwenye mlango wa jirani yake na kusikiliza akidhani atawasikia wakizungumza au hata sauti ya mtoto. Kwa ukimya ule aliamini bado wamelala, aliamua kuwagongea.
“Hodi.. Ngw’ana Bupilipili hodi hapa...,” kila alipogonga hakukuwa na jibu, aligonga huku akiliita jina la Ng’ana Bupilipili, hakukuwa na jibu. Alipoangalia aliona mlango umefungwa kwa nje kuonesha hakukuwa na mtu ndani.
Alirudi haraka kwa mumewe aliyekuwa bado amelala huku amejikunja gubigubi kwa baridi la alfajiri.
“Mume wangu hawapo.”
“Kina nini hao?” baba Sabina aliuliza.
“Si Mathayo na mkewe.”
“Si nilikuambia.”
“Kuhusu nini?”
Itaendelea

0 comments:

Post a Comment