#Wakala_Wa_Shetani-3-
Ndipo siku ya kujifungua ilipowadia hakutaka aitwe mtu yeyote kushuhudia anazaliwa mtoto gani kwa kuhofia siri yake kutoka nje kama atajifungua mtoto albino. Mumewe baada ya kukatazwa na mkewe asimwite mtu yeyoye aliamua kumsaidia mkewe kujifungua. SASA ENDELEA...
Kwa vile alikuwa na uzoefu aliweza kumsaidia mkewe kujifungua mtoto salama. Baada ya huduma zote mtoto alilazwa pembeni huku wakijitahidi kuzuia sauti ya mtoto kabla ya kujua mtoto aliyezaliwa ni wa aina gani ni albino au wa kawaida.
Mathayo baada ya kumhudumia mtoto wake na mkewe ambaye aliweza kukaa mwenyewe, kazi akawa kumtazama mtoto aliyezaliwa wa aina gani. Uchunguzi ulionesha mtoto yule ni albino. Walijikuta wote wakikosa raha hasa ngw’ana Bupilipili ambaye aliamini ana mtihani mkubwa wa kumpoteza tena mtoto mwingine ambaye amekaa naye tumboni kwa kipindi kirefu halafu watu wamchukue na kwenda kumuua kiurahisi.
“Unaona sasa mume wangu, ungemwita mama Sabina lazima siri hii ingetoka nje.”
“Sasa tutafanyaje na hali hii imetokea?”
“Dawa ni kumficha mtoto wetu ili wasijue nimejifungua.”
“Tutamfichaje? Pia mtu aliyejifungua anajulikana kwa tumbo kupungua na mtoto wetu tutamlea vipi usionekane kwa watu?” Mathayo aliona mtihani mgumu.
“Mume wangu nitaendelea kuweka nguo tumboni siku zote ili lionekane kubwa.”
“Tumbo sawa litaonekana kubwa, mtoto tutamweka wapi? Tukimficha ndani lazima atalia na kutoa sauti majirani watataka kujua ni mtoto wa aina gani. Na wakimuona hawatakubali kumuacha lazima watamuua, pia kutupiga faini ya ng’ombe watano huoni kama zizini kwetu ng’ombe watapungua?”
“Hilo nililijua toka mwanzo na nilijipanga kwa ajili ya hili,” ngw’ana Bupilipili alimtoa hofu mumewe aliyeonekana kuchanganyikiwa zaidi.
“Tutafanyaje mke wangu, huwezi kuamini hapa akili haifanyi kazi kabisa, siwezi kupoteza mtoto wa pili hivi hivi. Mke wangu sikubali nitaua mtu safari hii siwezi kukubali mtoto wangu auawe,” Mathayo alisema kwa uchungu kumuunga mkono mkewe.
“Nimepanga kitu kimoja kama nitajifungua albino.”
“Kipi hicho?” Mathayo aliuliza kwa shauku ya kujua mke wake amepanga nini.
“Usiku huu tutakwenda hadi kwenye mlima wa karibu na shamba letu, kuna pango nimeliandaa kwa ajili ya kumficha mtoto wetu.”
“Mke wangu unataka kuniambia usiku huu tutamwacha mtoto peke yake kisha turudi nyumbani?”
“Hapana, kila siku tutatoka alfajiri hadi kwenye pango hilo, kisha wewe utaingia shambani nami nitakuwa karibu na mtoto mpaka atakapokua kidogo, tutatoroka usiku kwa usiku na kwenda kijiji kingine.”
“Lakini mke wangu ni kijiji gani tutakachoweza kuishi na mtoto huyu bila matatizo?”
“Mume wangu hebu tufanya hili kwanza mengine yatafuata baadaye.”
Usiku uleule walimchukua mtoto wao na kutoka naye kiza kwa kiza. Japokuwa usiku ulikuwa mkubwa wenye kutisha, Ngw’ana Bupilipili alionesha ujasiri wa ajabu kwa kumuongoza mumewe hadi shambani kwao ambapo pembeni yake kulikuwa na kilima kidogo ambacho ndipo alipoandaa pango la kumtunzia mtoto wao.
Walitumia majani makavu kuyawasha moto ili kutengeneza tochi ya dharula kumulika sehemu ile. Mumewe alishangaa kukuta sehemu ile imetengenezwa vizuri sana.
“Mke wangu umetengeneza lini huku?”
“Toka nilipopata wazo la kujifungua tena mtoto albino basi nilijawa na mawazo ya kunusuru maisha ya mwanangu na kupata wazo la kupatengeneza huku.”
Walimlaza vizuri mtoto wao kisha Ngw’ana Bupilipili alijilaza pembeni ya mwanaye, naye Mathayo alilala pembeni kidogo ya mkewe, kwa vile muda ulikuwa bado usingizi uliwapitia.
Waliamshwa na sauti ya mtoto aliyekuwa akilia, Ngw’ana Bupilipili alishtuka usingizini na kukuta kumeanza kupambazuka, alimnyonyesha mtoto wake aliyeonekana ana njaa. Wakati huo mume wake alikuwa amekwisha amka na kutoka nje kuangalia hali ya usalama.
“Mke wangu wacha nirudi nyumbani nikawaandalieni chochote kitu.”
“Hakuna tatizo usisahau dawa zangu tumbo nalisikia kwa mbali.”
“Hakuna tatizo mke wangu.”
Mathayo kabla ya kuondoka alimtazama mkewe na kisha mtoto wake ambaye hakuwa na habari yeyote zaidi ya kuchezesha mikono na miguu baada ya kushiba na kufurahi kuja dunia salama, bila kujua hatari iliyo mbele yake ya kuonekana mkosi kwa jamii.
Bila kutegemea machozi yalimtoka kumwonea huruma mkewe ambaye aliamua kuishi maisha ya siyo yake kuhofia uhai wa mtoto wao.
Pia alimuonea huruma mtoto wao ambaye bado alikuwa hajapewa jina kutokana na misukosuko ya moyo wa kutaka kuokoa kwanza maisha yake baada ya wanakijiji kuona watoto maalbino ni mkosi kama wakiachwa kijiji kitapata balaa kubwa.
Japokuwa awali naye alikuwa ni mmoja wa watu walioamini albino ni mkosi, lakini mambo yalibadilika baada ya kutokewa yeye. Mwanzo naye alishiriki kuwaua watoto wa wenzake. Siku zote msiba wa mwenzio hauumi lakini msiba ikiwa kwako utajua uchungu wake. Mathayo baada ya mkewe kujifungua mtoto wa kwanza albino alikubali auawe lakini mkewe alisimama kidete asiuawe na kuwa tayari wafukuzwe kijijini.
Wakati wanahama kijiji walipovamiwa na vijana wa kijiji wenye jukumu kusaka na kutoa uchafu wa watoto wanaoonekana wanaleta mikosi kijijini. Mtoto albino alipouawa nyumba ilifanyiwa tambiko na kutengwa kwa muda wa wiki mbili.
Kilio cha mkewe baada ya kubeba ujauzito wa pili cha kuhofia uhai wa mtoto wake kilimfanya Mathayo naye abadili uamuzi na kuwa tayari kukisaliti kijiji pindi mkewe atakapo kifungua mtoto albino. Aliapa moyoni hatakubali kumtoa mtoto wake auawe tena.
Michirizi ya machozi iliendelea kumtoka huku miguu ikiwa mizito kunyanyuka. Mkewe alimwona na kunyanyuka alipokuwa amejilaza na mtoto na kumfuata mumewe. Alimkumbatia na kumbembeleza huku akimpigapiga mgongoni taratibu.
“Mume wangu hii ni mitihani aliyotupa Mungu tunatakiwa kupambana nayo, tunatakiwa tumtegemee yeye kwa kila kitu na kumtumai kwenye majaribu mazito kama haya. Hakika tutashinda japo kukua mwenetu itakuwa sawa kabisa na ngamia kupita kwenye tundu la shindano. Lakini tukimuamini yeye lolote kwake linawezekana,” Ngw’ana Bupilipili alimpa moyo mumewe.
“Ni kweli la..la..kini...” Mathayo hakumalizia kutokana na donge la uchungu kumkaba kooni huku machozi yakimdondokea mkewe.
Etaendelea
0 comments:
Post a Comment