KESI YA VITAMBULISHO VYA TAIFA (NIDA) BADO INA NGURUMA

Author
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu jana ilifurika watu huku vilio vikitawala wakati aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Dickson Maimu na wenzake saba, walipofikishwa kizimbani kwa mashtaka 27 ya uhujumu uchumi na kusababisha hasara ya Sh bilioni 1.16.

Ndugu na jamaa waliofurika katika mahakama hiyo waliangua kilio walipowaona washtakiwa wakiingizwa mahabusu wakitokea polisi walikolala tangu juzi, na vilio viliongezeka baadaye walipoamuriwa kurudi gerezani.

Washtakiwa walifikishwa mbele ya Hakimu Mkazi , Respicious Mwijage, wakikabiliwa na mashtaka ya kutumia madaraka vibaya, kula njama, kutumia nyaraka za uongo kumdanganya mwajiri na kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya Sh 1,169,352,931.

Hakimu Mwijage, kabla ya washtakiwa kusomewa mashtaka, aliwafahamisha kwamba mashtaka yanayowakabili yako chini ya Sheria ya Uhujumu Uchumi hivyo hawataruhusiwa kujibu kwa vile Mahakama Kuu ndiyo yenye mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo iliyofikishwa mahakamani na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ni Meneja Biashara, Avelin Momburi, Kaimu Mhasibu Mkuu wa NIDA, Benjamin Mwakatumbula, Mkurugenzi wa TEHAMA, Joseph Makani, Mkurugenzi wa Kampuni ya Aste Insurance Brokers, Astery Ndege, Ofisa Usafirishaji, George Ntalima, Mkurugenzi wa Sheria, Sabina Raymond na Xavery Kayombo.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Awamu Mbagwa akishirikiana na mawakili kutoka TAKUKURU, Janeth Machulya, Leonard Swai, Joseph Kiula na Fatuma Waziri waliwasomea washtakiwa hao mashtaka yanayowakabili.

Mbagwa alidai shtaka la kwanza linamkabili Maimu na Mwakatumbula ambao wanadaiwa tarehe tofauti kati ya Januari 15 hadi 19, mwaka 2010 katika makao makuu ya NIDA wilayani Kinondoni Mkoa wa Dar es Salaam, wakiwa watumishi wa umma kwa nafasi walizokuwa nazo walitumia madaraka vibaya.

Alidai waliidhinisha malipo kwa Gotham International Limited (GIL) ya Dola za Marekani 2,700,00 bila ya kutumia viwango vya kubadilisha fedha za kigeni vilivyowekwa na Benki Kuu ya Tanzania, kinyume na kifungu 19.3 cha mkataba kati ya NIDA na GIL, hivyo kuifanya GIL kupata faida ya Sh 3,969,000.

Mshtakiwa Maimu na Mwakatumbula katika shtaka jingine wanadaiwa kati ya Juni 3 na 5, 2013 katika makao makuu hayo walitumia madaraka vibaya kwa kuidhinisha malipo kwa GIL ya Dola za Marekani milioni 1.8, bila ya kuzingatia viwango vya kubadilisha fedha, hivyo kuifanya GIL kupata faida ya Sh 106,346,000.

Washtakiwa hao wawili wanadaiwa Juni 20, 2014 katika makao makuu hayo, waliidhinisha tena malipo ya Dola za Marekani 675,000 kwa GIL bila ya kuzingatia viwango vya kubadilisha fedha, hivyo kuifanya kampuni hiyo kupata faida ya Sh 42,471,000.

Maimu na Mwakatumbula wanadaiwa kutumia madaraka yao vibaya kwa kupitisha malipo mengine ya Sh milioni sita kwa GIL bila ya kupiga hesabu kwa kutumia viwango vya kubadilishia fedha hivyo kuifanya kampuni hiyo kupata faida ya Sh 14, 661,676.76.

Mbagwa alidai Maimu na Mwakatumbula wanadaiwa tarehe tofauti kati ya Januari 15, 2010 na Mei 16, 2015 katika makao makuu hayo ya NIDA kwa kuidhinisha malipo kwa GIL ya Dola za Marekani bila ya kuzingatia viwango vya kubadilisha fedha za kigeni waliisababishia NIDA kupata hasara ya Sh 167,445,676.76.

Mshtakiwa Ndege anakabiliwa na mashtaka ya kutumia nyaraka kumdanganya mwajiri.

Anadaiwa Aprili 16, 2012 katika makao makuu ya NIDA akiwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Aste Insurance Broker ambayo imeingia mkataba na NIDA wa kutoa huduma za bima, kwa nia ya udanganyifu.

Ilidaiwa kuwa Ndege aliwasilisha hati ya malipo yenye taarifa za uongo NIDA akionyesha kwamba kampuni yake inastahili kulipwa Sh 22,582,281 kwa huduma za bima iliyoitoa huku akijua taarifa hizo za uongo na zilikuwa na lengo la kumdanganya mwajiri wake.

Mshtakiwa Momburi, Mwakatumbula na Ntalima wanadaiwa kati ya Februari 22 na Aprili 17, 2012 katika makao makuu hayo walitumia madaraka yao vibaya kwa kupitisha malipo ya Sh 22,582,281 kwa Kampuni ya Aste Insurance Brokers hivyo kuifanya kampuni hiyo kupata faida ya kiasi hicho.

Maimu, Mwakatumbula na Ntalima pia wanakabiliwa na mashtaka ya matumizi mabaya ya madaraka wakidaiwa kupitisha malipo ya bima kwa kampuni ya Aste hivyo kuifanya kampuni hiyo kupata faida ya viwango mbalimbali vya fedha.

Mkurugenzi huyo wa NIDA, Mwakatumbula, Ndege na Ntalimwa wanadaiwa katika tarehe tofauti kati ya Agosti 2012 na Januari 4,2013 katika makao makuu ya NIDA waliisababishia mamlaka hiyo hasara ya Sh 55,312,800.

Katika mashtaka mengine, Maimu, Mwakatumbula na Makani wanadaiwa kati ya Januari 29 na 30, 2013 katika makao makuu hayo walitumia madaraka yao vibaya kwa kuidhinisha malipo ya Dola za Marekani milioni mbili kwa IRS Corporation Berhad.

Ilidaiwa kuwa mapendekezo ya utaratibu mpya wa haraka wa upatikanaji wa vitambulisho na vifaa bila ya kufanya marekebisho ya mkataba ulioko kati ya NIDA na kampuni uliiwezesha IRIS kupata faida ya fedha hizo.

Pia washtakiwa hao Maimu, Mwakatumbula na Makani wanadaiwa kupitisha malipo kwa kampuni hiyo ya IRIS ya viwango mbalimbali hivyo kuifanya ipate faida.

Mwakatumbula, Ntalima na Kayombo wanadaiwa kati ya Juni mosi na 6, 2013 katika makao makuu hayo kwa pamoja walikula njama za kutenda kosa la kutumia nyaraka za uongo kwa nia ya kumdanganya mwajiri.

Washtakiwa Mwakatumbula, Ntalima na Kayombo wanadaiwa kati ya Juni 4 na 6,2013 katika makao makuu hayo waliisababishia hasara NIDA ya Sh 45,515,96

Chanzo: Mtanzania.

posted from Bloggeroid

0 comments:

Post a Comment