
Rais wa Marekani Barack Obama hatimaye
amejiunga na Facebook, na ujumbe wake wa
kwanza umekuwa ni wa kuhimiza watu
kuchukua hatua kukabiliana na mabadiliko ya
tabia nchi.
Ikulu ya White House kwenye ukurasa huo
wake imepakia video ya Obama akitembea
katika eneo la South Lawn katika ikulu ya
White House.
Hatua yake ya kujiunga na Facebook,
mtandao wa kijamii wenye zaidi ya watumiaji
bilioni moja, inaonekana kama juhudi za
kiongozi huyo kuwafikia zaidi vijana na
makundi mbalimbali ya watu.
“Natumai mtachukulia huu kuwa ukumbi
ambao tunaweza kutumia kujadiliana kuhusu
masuala muhimu kuhusu taifa letu,” anasema
kwenye video hiyo.
Obama anaonekana akitembea kwenye bustani
hiyo ambayo imekuwa chini yake kwa miaka
saba iliyopita, ambayo kama anavyosimulia,
ina mbweha, mwewe na vichakuro.
Lengo kuu la kisiasa hata hivyo linaonekana
kuhimiza ulimwengu kuunga mkono juhudi za
kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
Obama atazuru Paris mwezi Desemba,
kutafuta uungwaji mkono wa mkataba wa
kuweka vikwazo kwa mataifa kuhusu viwango
vya utoaji wa gesi zinazochangia ongezeko la
joto duniani.
Kutokana na hali kwamba Bunge la Congress
linadhibitiwa na chama cha Republican,
ambacho hakijatambua hatari inayotokana na
mabadiliko ya tabia nchi, anahitaji kutafuta
uungwaji mkono zaidi hata nyumbani.
White House imesema inatumai Facebook
itasaidia kama ukumbi wa kubadilishana
mawazo.
“Ukurasa huu utawapa Wamarekani jukwaa la
kubadilishana mawazo yao na Rais kuhusu
masuala ambayo wanayajali sana,” amesema
naibu mkurugenzi wa mkakati wa dijitali
katika White House Kori Schulman.
Bw Obama alijiunga na mtandao wa kijamii wa
Twitter mwezi Mei mwaka huu.






0 comments:
Post a Comment