MAFANIKIO YA SAMATTA NA ULIMWENGU

Author
Mshambuliaji wa TP
Mazembe, Mbwana Samatta amesema
medali yake ya ubingwa wa Ligi ya
Mabingwa na ufungaji bora wa Afrika,
ameitoa kwa baba na marehemu mama
yake.
Katika fainali hiyo, TP Mazembe ilishinda
jumla ya mabao 4-1 dhidi ya USM Algers.
Katika mchezo wa kwanza uliochezwa
nchini Algeria, Mazembe waliibuka na
ushindi wa mabao 2-1 yaliyofungwa na
Samatta na Rainford Kalaba, kabla ya
kupata ushindi wa mabao 2-0 yaliyofungwa
na Samatta na Roger Assale mjini
Lubumbashi juzi.
Akizungumza katika kipindi cha michezo
cha radio Clouds FM, Samatta alisema cha
muhimu kwake ilikuwa ni kuibuka
mabingwa na si kuwa mfungaji bora.
“Natamani mama yangu angekuwa hai leo
hii ashuhudie mafanikio yangu, naamini
angefurahi zaidi, ushindi huu ni zawadi
kwake na baba pia,” alisema Samagol.
“Nashukuru nimekuwa mfungaji bora,
ndoto zangu naona zinaanza kutimia,
namshukuru Mungu kwa kusikia maombi
yangu, lakini kitu nilichokuwa nakitamani
ni kutwaa ubingwa, kwa sababu ni jambo
kubwa katika historia yangu.”
Samatta amechukua tuzo ya mfungaji bora
baada ya kufunga mabao saba, sawa na
Bakry ‘Al Medina’ Babiker wa Al Merreikh
ya Sudan. Kwa mujibu wa rekodi za CAF,
Samatta amefunga mabao saba tofauti na
ilivyoripotiwa awali.
Naye Thomas Ulimwengu alisema:
“Nimefurahi sana, yaani sijui nielezee vipi
furaha niliyonayo, Mungu mkubwa!”
Baada ya mafanikio hayo ya Samatta na
Ulimwengu wadau mbalimbali wa soka
nchini wamewapongeza nyota hao na
kutaja kile wanachodhani ni siri ya
mafanikio kwa nyota hao.
Lowassa awapongeza
Aliyekuwa mgombea urais wa Chadema
aliyeungwa mkono na vyama vilivyounda
Ukawa, Edward Lowassa amempongeza
Samatta kwa kuwa Mtanzania wa kwanza
kutwaa tuzo ya mfungaji bora barani
Afrika.
Lowassa aliyekuwa akifuatilia pambano
hilo kwa njia ya runinga, alisema Samatta
amedhihirisha kwamba wanasoka wa
Tanzania wakiamua kujituma na kuwa
wavumilivu watafika mbali.
“Yule kijana na yule mwenzake
(Ulimwengu) ni wavumilivu na wanajua
nini wanatafuta, watafika mbali sana... hii
ni fahari kwa taifa letu, tunao uwezo wa
kuwa na kina Samatta wengi zaidi kama
tukiwekeza zaidi kwenye soka,” alisema
Lowassa.
“Moja ya sera za Chadema na Ukawa ni
kuondoa ushuru katika vifaa vyote vya
michezo pamoja na kuanzisha shule
maalumu za soka ambako huko tutakuza
vipaji na kuwatoa kina Samatta,” alisisitiza
na kuongeza, “Serikali ya CCM isione aibu
kuchukua sera hizo kwa manufaa ya
michezo nchini.”
Siri ya mafanikio
Ikumbukwe Samatta ni zao la timu inayolea
vipaji vya soka ya Kimbangulile Academy,
wakati Ulimwengu akiibukia kwenye
kilichokuwa kituo cha soka Tanzania (TSA),
ambacho kilikuwa kinamilikiwa na
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Ofisa Maendeleo wa TFF, Jemedari Said
alisema kitendo cha washambuliaji hao
kufanya vizuri hivi sasa kinaonyesha
umuhimu mkubwa wa kuviendeleza vyema
vipaji vya soka kwa watoto.
“Wito wangu ni kuwaomba Watanzania
kukubali mpira una sayansi yake na
unafundishwa tangu utotoni, tutumie vituo
vilivyopo katika kutupa talanta za vijana
wetu,” alisema Jemedari.
Kocha Msaidizi wa Majimaji, Hassan Banyai
alisema: “Binafsi nafarijika kwa mafanikio
waliyofikia kwa sababu mtu kama Samatta
nilimfundisha kwenye timu ya Mkoa wa
kisoka ya Temeke kipindi hicho akiwa bado
mdogo.
“Ni lazima tuendeleze vipaji vya vijana na
ndio maana hata mimi mwenyewe
nimefungua kituo changu kule Kigamboni
ili niwaibue akina Samatta wengine.”
Kocha Kennedy Mwaisabula alisema siri
kubwa ya mafanikio ya nyota hao ni
kutolelewa katika misingi ya timu kubwa
hapa nchini ambazo zinajulikana kwa
kuharibu wachezaji.
“Samatta hakukaa Simba na Ulimwengu
hakupitia kabisa katika hizo timu ambazo
mchezaji halelewi katika misingi ya
kinidhamu. Ni katika hizo timu ndiyo
unakuta mchezaji anachelewa kambini,
lakini kiongozi anamtetea.
“Watazame vizuri Samatta na Ulimwengu
maisha yao utagundua kuwa yana tofauti
kubwa na wachezaji waliopo nchini
kuanzia uwanjani hadi maisha yao binafsi,”
alisema Mwaisabula.
Matumla, Cheka wasifia
Mabingwa wa dunia wa mikanda ya ndondi
ya WBU na WBF, Rashid Matumla na
Francis Cheka wamempongeza Samatta kwa
kuitoa Tanzania kimasomaso katika soka
Afrika.
“Mafanikio ya Samatta ni hatua kubwa si
kwake pekee bali kwa Tanzania yote, katika
ushindi wake anatajwa kama Mtanzania,
hiyo ni faraja kwa taifa, akijituma atafika
mbali zaidi,” alisema Matumla.
Bingwa wa zamani wa dunia wa WBF,
Cheka alisema Samatta ni mfano wa kuigwa
katika soka la Tanzania na kumshauri
kutobweteka na mafanikio aliyopata.

0 comments:

Post a Comment