WABUNGE 45 CCM WAANGUKA KURA ZA MAONI

Author
Wakati vyombo vya juu vya
baadhi ya vyama vya siasa vikiwa vimeanza
hatua za mwisho za kupitisha wagombea
wa ubunge na udiwani tayari kwa Uchaguzi
Mkuu wa Oktoba 25, hadi juzi wabunge 51
walikuwa wameanguka kwenye kura za
maoni za ndani ya vyama vyao.
Idadi hiyo ni takriban asilimia 14 ya
wabunge 357 wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano, inayojumuisha waliochaguliwa
na wananchi na wa viti maalumu, ambao
waliamua kwenda kupambana majimboni.
Miongoni mwa walioanguka ni mawaziri
wa Serikali ya Muungano na Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar, ambao walikuwa
wakitetea viti vyao majimboni.
Kati ya wabunge hao walioanguka, wawili
wanatoka Chadema, wanne CUF na wengine
45 waliosalia wanatoka CCM.
Matumaini pekee yaliyosalia kwa wabunge
hao ambao baadhi yao wamekata rufaa
kupinga matokeo ya kura za maoni, ni
huruma za vikao hivyo ambavyo vinaweza
kubadili matokeo ya baadhi ya majimbo,
hasa ambayo taratibu zilikiukwa na
ushahidi wa kuwapo matumizi ya rushwa.
Wakati wabunge walioanguka Chadema
wanasubiri kwa hamu kikao cha Kamati
Kuu kilichoanza juzi kupitia majina hayo,
wa CCM wanasubiri mfululizo wa vikao
vinavyoanza leo hadi Agosti 13, wakati
mchakato kupitisha wagombea wa NCCR-
Mageuzi bado.
Kwa wabunge wa CUF, hakuna matumaini
kutokana na vikao vya juu vya chama hicho
kukamilisha kazi yake hivi karibuni.
Mbali na walioanguka, wabunge waliopita
katika kura za maoni lakini vyama vyao
vinaunda Umoja wa Katiba ya Wananchi
(Ukawa), nao watalazimika kusubiri hadi
vyombo hivyo vya mchujo vitakapomaliza
kazi, kujua kama wamepita.
Hiyo inatokana na makubaliano ndani ya
umoja huo ya kusimamisha mgombea
mmoja atakayeungwa mkono na vyama
vyote.
Kwa mujibu wa makubaliano ya vyama
hivyo vinne; Chadema, CUF, NLD na NCCR -
Mageuzi- kinachooonekana kina nguvu
kwenye jimbo fulani ndicho mgombea wake
ataachiwa kupeperusha bendera ya umoja
huo, jambo ambalo vyama hivyo vilisema
vimekamilisha kazi ya mgawanyo kwa
asilimia 95.
Wakati Chadema, CUF, NCCR na NLD
wakisubiri utekelezwa wa makubaliano
hayo, wabunge wa CCM watakuwa
njiapanda baada ya chama hicho kueleza
kuwa hakitarudia makosa ya mwaka 2010
ya kupingana na maoni ya wanachama kwa
kutengua matokeo ya kura za maoni.
Profesa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
(UDSM), Jamidu Katima alisema kuanguka
kwa wabunge hao kunatokana na wengi
wao kutoonekana majimboni baada ya
kupewa dhamana ya kuongoza wananchi.
“Kama kiongozi umepewa dhamana, lakini
huonekani jimboni basi ni dhahiri
wananchi watakukataa. Wakikuona
unachukua fomu watakushangaa lakini
ujue watakukataa kwa sababu huwatatulii
kero zao kama ulivyoahidi awali.”
Profesa Katima alisema kwa sasa
Watanzania wameamka, hivyo ni vigumu
kudanganyika na kwamba kama kiongozi
hatumii vyema dhamana aliyopewa,
wananchi watamuacha apumzike kwa
amani.
Maoni kama hayo yalitolewa na mhadhiri
wa sayansi ya siasa wa Chuo Kikuu cha Dar
es Salaam, Dk Alexander Makulilo ambaye
alisema zipo sababu chekwa za baadhi ya
mawaziri kushindwa kwenye kura za
maoni, mojawapo ikiwa ni makundi na
kushindwa kutimiza ahadi.
Kujaribu mtu mwingine
Dk Makulilo alisema ni rahisi kwa
wananchi kuacha kumchagua kiongozi
baada ya kuona hajatimiza kile alichoahidi
hivyo wakaona wajaribu kiongozi mwingine
pengine atawatatulia kero zao.
Kuhusu kuanguka kwa wanasiasa nguli wa
CCM, mhadhiri huyo alisema sababu
nyingine ni siasa za makundi ambako kundi
moja tu linaweza kufanya juhudi ili
mwingine ashindwe.
“Sasa hivi tunazungumzia mtu kuanguka
katika chama chake, kwa hiyo siasa za
makundi ndani ya chama hicho inaweza
kusababisha kuanguka katika kura za
maoni,” alisema.
Sababu nyingine aliyoitaja Dk Makulilo ni
wimbi la vijana na kuwa inawezekana
wananchi wanahamia kwa wanasiasa
vijana zaidi baada ya kuona wengine
amekaa madarakani kwa muda mrefu.
Pia, aliitaja rushwa kuwa miongoni mwa
sababu za kuanguka kwani inawezekana
kuwa mgombea mwenzake ametoa fedha au
yeye ametoa, lakini mwingine ametoa
nyingi zaidi.
“Nadhani umeona jinsi ambavyo Takukuru
wamekamata wagombea wengi kwa tuhuma
za rushwa kwa hiyo hapana shaka kuwa
suala la rushwa lilikuwepo,” alisema.
Utafiti wa Twaweza
Idadi ya wagombea hao walioanguka katika
hatua ya awali inaashiria kuanza kutimia
kwa matokeo ya utafiti uliofanywa na
taasisi ya Twaweza mwishoni mwa mwaka
jana ambao ulionyesha kuwa nusu ya
wabunge wataanguka kwenye kura za
maoni.
Kwa mujibu wa utafiti huo uliotangazwa
Novemba 12, 2014, kuanguka kwa wabunge
hao kutatokana na kushindwa kutekeleza
ahadi zao. Asilimia 47 ya wananchi
walioulizwa iwapo watampigia tena kura
mbunge wao, walisema “hapana” huku
asilimia kama hiyo ikisema “ndiyo”.
Utafiti huo ulieleza kuwa ahadi nyingi
zilizotolewa na wabunge kwenye mikutano
ya kampeni wakati wa uchaguzi
hazijatekelezwa na kwamba asilimia 78 ya
wananchi bado wanazikumbuka.
CCM kutorudia makosa
Wakati utafiti wa Twaweza ukizungumzia
kutotimizwa kwa ahadi, wabunge waliopita
kura za maoni watakuwa wakijifariji na
matamshi ya viongozi wao kuwa majina
yao hayatakatwa kama ilivyokuwa mwaka
2010.
Akihutubia kwenye mkutano wa hadhara
mjini Iringa Oktoba mwaka jana, Katibu
Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana
alisema chama hicho hakitarudia makosa
ya kuengua majina ya wagombea
wanaopitishwa na wanachama kwenye
kura za maoni baada ya Frederick
Mwakalebela kuenguliwa na Halmashauri
Kuu kugombea ubunge wa Jimbo la Iringa
Mjini na baadaye Mchungaji Peter Msigwa
wa Chadema akatwaa jimbo hilo.

0 comments:

Post a Comment