Ukawa kuonyesha jeuri jumatatu

Author
AGOSTI 10 mwaka huu, Umoja wa Katiba ya
Wananchi (UKAWA) umekusudia kufanya
msafara mkubwa wa kumsindikiza Edward
Lowassa kuchukua fomu ya kugombea urais
katika Ofisi za Tume ya Uchaguzi (NEC), Jijini
Dar es Salaam.
Kwenye msafara huo Lowassa
ataongozana na mgombea
mwenza wake Juma Duni Haji.
Lowassa alijiunga na Chadema
Julai 28 mwaka huu akitokea
Chama Chama Cha Mapinduzi
(CCM) huku Duni alijiunga
Agosti 4 akitokea CUF.
Msafara huo utaanzia kwenye Ofisi Kuu ya
CUF, Buguruni, Dar es Salaam saa 3:00
asubuhi ambapo wanachama wa vyama
vinavyounda umoja huo (Chadema, NCCR-
Mageuzi, NLD na CUF) watakutana na kuanza
safari ya kwenda NEC.
Baada ya Lowassa kuchukua fomu NEC,
msafara huo utaelekea Makao Makuu ya
Chadema yaliyopo Mtaa wa Ufipa, Kinondoni
ambapo wateule hao watafanyiwa sherehe ya
kupongezwa kwa hatua waliyofikia.
Akizungumza na waandishi wa habari leo
jijini Dar es Salaam, Kaimu Katibu Mkuu wa
Chadema-Bara, Salim Mwalimu akiwa kwenye
Ofisi za NCCR-Mageuzi walipofanyia mkutano
amesema, wagombea hao wapo tayari.
Akifafanua kuhusu msafara huo amesema,
wagombea hao watasindikizwa na viongozi
wa UKAWA, wanachama wa umoja huo
pamoja na wananchi watakaojitokeza
kumsindikiza Lowassa.
Kuhusu suala la ugawanywaji wa majimbo
baina ya umoja huo Mwalim amesema
“tumeshamaliza kila kitu na tumeshagawana
ila bado kutangaza tu muda ukifika
tutawatangazia wananchi”.
Mbali na hilo Mwalimu ameongelea kuhusu
mbinu za wizi zinazofanywa na NEC kwa
kushirikiana na Chama tawala (CCM) ambapo
amedai kuwa kumekuwa na malalamiko mengi
toka kwa wananchi ambao wanafanyiwa
udanganyifu.
“Kumekuwa na wizi wa waziwazi unaofanywa
na CCM na tunasikitika kuwa tume ipo kimya
ikionesha kuridhia na matendo hayo. Vijijini
watu wanaombwa namba zao za vitambulisho
vya kura na watu wanaodai wametumwa na
serikali, sisi tumegundua tayari.
“Namba ya kitambulisho ni mali ya
mwananchi na sio ya serikali wala tume.
Tumegundua mbinu zote zinazofanywa na
CCM ili waendelee kubaki madarakani ila
wakae wakijua mawimbi haya hayawezi
kuzuilika kwani Ukawa ni chaguo la
wananchi.”
Kuhusu kuachia ngazi kwa aliyekuwa
Mwenyekiti wa CUF, Prof. Ibrahim Lipumba
amesema, kuondoka kwake hakuwezi kubomoa
Ukawa wala kusambaratisha CUF.
“Ukawa bado tupo hai wala hatutapoteza
muda wetu kukaa kumlilia aliyejitoa kwani
yawezekana mwezetu hana ndoto ya
matumaini ya kushika dola, anapenda tubaki
chini,” amesema na kuongeza;
“Nawapongeza sana CUF kwa kuweza
kulichukulia wepesi hilo na kutomjali kwa
kujiuzulu kwake kwani hakujaharibu chochote.
Sisi bado tunasonga mbele na Jumatatu
tutawasha moto Ofisi Kuu ya CUF.”
Naye Tozzy Matwanga ambaye ni Katibu
Mkuu wa NLD amewataka wanachama wa
chama hicho wote wajitokeze kwa wingi siku
hiyo katika msafara wa kwenda NEC.
“Pia tunaomba serikali kuimarisha ulinzi pale
unapohitajika. Hivyo hivyo kwa NEC
wasimamie haki na misingi ya kazi yao kwani
damu ya wananchi ikimwagika wao ndio
kitakuwa chanzo.”

0 comments:

Post a Comment