Mchakato wa kumpata mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM)
umeendelea kuibua mapya na kuleta mvutano baada ya Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Rais (Kazi Maalum), Prof. Mark Mwandosya, kunukuliwa akisema
kuwa majina matano yaliyopelekwa kwenye Kamati Kuu ya CCM (CC) kutoka
kwenye Kamati ya Maadili yalijulikana hata kabla ya kikao cha Kamati ya
Maadili hakijaketi.
Prof. Mwandosya ambaye ni Mbunge wa Rungwe Mashariki amenukuliwa
akisema hayo kwenye sauti yenye maelezo yake iliyorekodiwa na kusambazwa
katika mitandao mbalimbai ya kijamii.
Akizungumza kwa simu akiwa uwanja wa ndege jana ambao
hata hivyo hakuutaja wala alikokuwa akienda, Prof. Mwandosya alisema
amepata taarifa za kusambazwa kwa sauti hiyo lakini hafahamu kama
yanayozungumzwa humo ni ya kwake.
Prof. Mwandosya alisema anachokumbuka akiwa kijijini kwao Lufilio
wilayani Rungwe aliitwa na wazee na kufanya nao mkutano wa ndani
wakitaka kujua nini kilichojiri wakati wa mchakato wa kumpata mgombea
urais CCM.
“Niliitwa na wazee kwenye mkutano wa ndani wakitaka kujua nini
kimetokea na inawezekana yaliyomo ndani ya hiyo clip yana ukweli, lakini
wewe unadhani nilichokisema ni uongo?, Si kinalingana na hali halisi
ilivyokuwa Dodoma,” alisema.
Hata hivyo, alisema taarifa zilizosambazwa kwamba anataka kuhamia Chadema siyo za kweli.
Katika sauti iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii, Prof.
Mwandosya amenukuliwa akisema kuwa majina ya makada walioingia tano bora
katika kinyang’anyiro cha urais yaliyopelekwa Kamati Kuu yalijulikana
hata kabla ya kikao cha Kamati ya Maadili hakijaketi.
Alisema Mwenyekiti wa Kamati Kuu, Rais Jakaya Kikwete, alikuwa na
majina yake matano mfukoni na kamati yenyewe pia ilikuwa na majina yake.
Akizungumzia madai hayo, Prof. Mwandosya alithibitisha kuwa madai
hayo ni ya kweli na kwamba wajumbe wote wa Mkutano Mkuu wa CCM
waliokuwapo Dodoma wanalijua hilo.
“Hapo mimi sioni kwamba kuna jambo ambalo limepotoshwa, kwani yote
yanayosemwa ni ya kweli na hata wajumbe wote waliokuwa Dodoma kwenye
Mkutano Mkuu wanayajua vizuri mambo hayo,” alisema Prof. Mwandosya.
Alisema ingawa hajaisikia sauti inayodaiwa kuwa ni yake, lakini
kama ni suala la kusema kuwa mgombea urais mteule wa CCM, Dk. John
Magufuli hajawahi kuwa hata mwenyekiti wa tawi la CCM ni kweli.
Alizidi kueleza kuwa, anaona ni sahihi kwa sababu katika kumbukumbu
zake hajawahi kusikia wala kumwona Dk. Magufuli akiwa Mwenyekiti wa
Chama katika ngazi yoyote.
“Nina kazi nyingi sijafungua mitandao ya kijamii kwa muda mrefu
kidogo, lakini kama mambo yanayosemwa ni hayo, sioni kama kuna uongo
ndani yake, ningepata shida sana kama mambo yanayozungumziwa yangekuwa
siyo ya kweli, katika kumbukumbu zangu sijawahi kusikia Dk. Magufuli
amekuwa Mwenyekiti wa Chama au Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama,
lakini sasa ndiye atakayekuwa mwenyekiti wa Chama chetu nadhani hilo
liko wazi,” alisema.
Akizungumzia uamuzi wa Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa,
kuhamia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Prof. Mwandosya
alisema kuwa Lowassa ametumia haki yake ya kidemokrasia na yeye haoni
kama kwa uamuzi huo amefanya kosa lolote.
Alisema vyama vya siasa ni sawa na madhehebu ya dini, ambapo
waumini wanayo haki ya kwenda kuabudu katika kanisa wanalolitaka au
ambalo imani yao inawatuma na hakuna mtu wa kuwapokonya haki hiyo.
“Alichokiamua Lowassa sidhani kama ana kosa, kwani anayo haki na
uhuru wa kufanya alichokifanya, siku hizi kuna makanisa mengi, mtu
anapoamua kwenda kuabudu katika kanisa analoona linamfaa huwezi kusema
kuwa amekosea, labda ninachoweza kushauri ni CCM kujiuliza sababu za
Lowassa kuondoka na ikiwezekana ijisahihishe ili watu wengi zaidi
wasiondoke,” alisema.







0 comments:
Post a Comment