Azam imezima ndoto ya Yanga ya kutwaa taji la sita la
mashindano ya Kombe la Kagame baada ya kuitoa kwa penalti 5-3 katika
mchezo wa robo fainali uliofanyika jana kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam.
Baada ya timu hizo kumaliza dakika 90, bila ya
kufungana ndipo ilipokuja changamoto ya mikwaju ya penalti ambayo mwaka
huu imekuwa mwiba mchungu kwa Yanga ambayo kabla ya penalti za jana
tayari ilishakosa penalti tatu katika michezo ya hatua za makundi.
Shujaa
wa Azam katika mchezo wa jana alikuwa ni kipa Aishi Manula
aliyechaguliwa mchezaji bora wa mechi baada ya kudaka penalti ya tatu ya
Yanga iliyopigwa na Haji Mwinyi.
Azam iliyoanza kupiga
penalti ilipata penalti zake zote tano zilizopigwa na Kipre Tchetche,
John Bocco, Himid Mao, Pascal Wawa na Aggrey Morris wakati kwa upande
wa Yanga waliopata ni Salum Telela, Nadir Haroub na Godfrey Mwashiuya
huku Mwinyi akikosa.
Akizungumzia mchezo huo kocha wa Yanga, Hans Pluijm alisema ameumia kupoteza mchezo huo ambao kwake ulikuwa kama fainali.
“Kupoteza mchezo huu ni pigo kwangu, kwa sababu tulikuwa na malengo ya kutwaa ubingwa katika ardhi ya nyumbani.”
Pluijm
alisema,“Kipindi cha kwanza hatukucheza vizuri, japo kipindi cha pili
tulitengeneza nafasi nyingi zaidi, lakini mashuti yetu mengi hayakulenga
goli.
“Sasa nguvu zetu tunaelekeza katika maandalizi yetu ya ligi inayokaribia kuanza hivi karibuni,” alisema Mdachi huyo.
Kwa
ushindi huo sasa Azam itacheza nusu fainali Ijumaa na KCCA ukiwa kama
marudiano ya mchezo wa Kundi C ambao Azam walishinda 1-0.
Katika
mchezo wa jana timu hizo zilianza mchezo kwa kasi na kushambulia
mfulululizo tangu dakika ya kwanza ambapo Azam ilikosa bao baada ya
krosi ya Shomari Kapombe kuwapita mabeki wa Yanga, lakini John Bocco
alishindwa kufunga.
Yanga ilijibu mapigo dakika moja
baadaye kupitia mshambuliaji wake Donald Ngoma aliyewatoka mabeki wa
Azam na kupiga shuti lililopanguliwa na kipa Aishi Manula na kuwa kona
ambayo haikuzaa matunda.
Kipa wa Azam, Manula
alilazimika kufanya kazi ya kupangua shuti la Juma Abdul alililopiga
akiwa umbali wa mita 18 katika dakika ya 8. Pia mpira wa kurushwa wa
Mbuyu Twite nusuru uingie golini kama si ustadi wa Manula kuutoa nje.
Yanga
iliyokuwa ikitumia mfumo wa 4-2-3-1 ambao ni mabeki wanne wakisaidiwa
na viungo wawili wakabaji, viungo watatu washambuliaji na mshambuliaji
mmoja, ilifanya mashambulizi mengi kipindi cha pili.
Azam
iliyokuwa ikitumia mfumo wa 4-3-3, ambao ilitumia mabeki wanne, viungo
watatu na washambuliaji watatu, ilitumia mashambulizi ya kushtukiza na
katika dakika 34 nusura ipate bao, lakini shuti la Tchetche
lilipanguliwa na kipa wa Yanga, Mustapha ‘Barthez’ na kurudi uwanjani na
kumkuta Himid Mao aliyepiga shuti la chini na Tchetche alipojaribu
kuunganisha mpira ulipaa juu.
Tofauti na michezo
iliyopita, jana washambuliaji wa Yanga, Tambwe, Ngoma, Mwashiuya na
Kaseke walikuwa kwenye wakati ngumu mbele ya ngome ya Azam iliyoongozwa
na Wawa, Morris, Kapombe na Kheri Abdallah iliyocheza kwa maelewano
makubwa kuziba njia.
Kipindi cha pili kocha wa Azam,
Stewart Hall aliwapumzisha Frank Domayo, na Kheri Abdallah na kuwaingiza
Ame Ally na Said Morad wakati Hans Pluijm aliwatoa Kaseke, Juma Abdul,
Niyonzima na kuwaingiza Salum Telela, Joseph Zutah na Malimi Busugu.
Pamoja
na mabadiliko hayo bado timu hizo ziliendelea kutengeneza nafasi nyingi
za kufunga, lakini hakuna timu iliyofanikiwa kutumia na mchezo ukaingia
katika ubabe wa hapa na pale.
Twite alinusurika kupewa
kadi nyekundu katika dakika ya 74 baada ya kumchezea vibaya Himid Mao
wakati akiwa tayari na kadi ya njano aliyopewa dakika 71 kwa kumchezea
vibaya Mao. Pia Jean-Baptiste Mugiraneza alipewa kadi ya njano kwa
kumchezea vibaya Tambwe dakika 78.
Hadi filimbi ya
mwisho inapigwa kuashiria kumalizika kwa mechi hiyo, Azam ilikuwa
imetunza rekodi yake ya kutofungwa bao lolote hadi sasa katika
mashindano hayo, wakati Yanga ikiwa imefungwa mabao mawili.
Awali KCCA ya Uganda ilijihakikishia kucheza nusu fainali baada ya kuichapa Al Shandy ya Sudan kwa mabao 3-0 kwenye Uwanja huo.
Mabao
ya Joseph Ochaya, Muzamir Mutyaba na Tom Masiko yalitosha kuihakikishia
KCCA kufuzu kwa nusu fainali kwa mara ya pili mfulululizo.
Mabingwa
hao wa 1978 ni mara ya kwanza katika mashindano ya mwaka huu kufanikiwa
kufunga mabao matatu kwani katika mechi zake tatu zilizopita ilifunga
mabao mawili tu.






0 comments:
Post a Comment