MBOWE AUNDIWA NJAMA

Author
 Wanachama wa Chadema wamedai kufichua mpango unaofanywa na baadhi ya viongozi wa CCM wa kumwekea pingamizi Mbunge wa Jimbo la Hai, Freeman Mbowe ili asiwanie ubunge.

Kiini cha mipango hiyo ni hukumu ya Mahakama ya Wilaya ya Hai iliyomtia hatiani kwa kosa la kumshambulia mwangalizi wa ndani katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, Nassir Yamin.

Katika hukumu hiyo, iliyotolewa Juni 17 na Hakimu Mkazi wa Wilaya ya Hai, Dennis Mpelembwa alimhukumu Mbowe kulipa faini ya Sh1 milioni au kwenda jela mwaka mmoja.

Hata hivyo, Mbowe ambaye ni mgombea pekee na kushinda kura za maoni kwa kupata 269 za ndiyo na tano za hapana, alilipa faini hiyo na kuachiwa huru baada ya wafuasi wake kuchanga fedha hizo.

Mipango hiyo inayodaiwa kuwa ni ya CCM kutaka kutumia hukumu hiyo kumzuia Mbowe kuwania ubunge, ilielezwa jana katika Mkutano Mkuu maalumu wa kura za maoni za ubunge Jimbo la Hai.

Mmoja wa wajumbe wa mkutano huo, James Swai alimuuliza Mbowe amejiandaaje, kwa sababu kuna madai kuwa CCM wana mpango wa kutumia kesi hiyo ili kumwengua kugombea nafasi hiyo.

Hata hivyo, wakati akijibu swali hilo, Mbowe hakueleza wazi kama anafahamu mpango huo zaidi ya kuitaka CCM isitafute ushindi wa mezani.

“Wangekuwa na wanasheria wasingefikiria kabisa wala kuzungumza hivyo. Kifungu nilichohukumiwa nacho hakinizuii kugombea. Wasitafute ushindi wa mezani waje uwanjani,” alisema Mbowe.

Mbowe alisema tayari jopo la mawakili sita wa Chadema, ambao hata hivyo hakuwataja kwa majina, limeweka mkakati maalumu wa kukata rufaa kupinga hukumu hiyo aliyodai ni batili.

0 comments:

Post a Comment