BULAYA AKATAA UWAZIRI

Author
Mbunge wa Viti Maalum alihama
juzi CCM na kujiunga Chadema, Ester
Bulaya amesema licha ya kuahidiwa vyeo
vingi ukiwamo uwaziri na ukuu wa wilaya
ili asihame CCM, aliamua kuviacha ili
aweze kuwasaidia Watanzania wa chini
ambao wameonewa na serikali ya chama
hicho kwa miaka 50 iliyopita.
Akihutubia katika mkutano wa hadhara
uliofanyikia katika Viwanja vya Stendi ya
zamani mjini Bunda jana, Bulaya alisema
wakati chama chake cha zamani
kilipogundua mikakati yake ya kuhamia
Chadema, makada wake walimwendea
wakimsihi asitoke, bali abakie ili apatiwe
ukuu wa wilaya au uwaziri.
Bulaya aliyeambatana na Mbunge wa
Kahama, James Lembeli ambaye pia
alijiunga na Chadema juzi, alisema baada
ya kutafakari kwa muda mrefu uhalisia wa
maisha ya Watanzania hasa wa vijijini na
jinsi ambavyo Serikali ya CCM imekuwa
ikiwatendea, aliamua kuachana na ahadi
hizo na kujiunga na Chadema kwa kuwa
inalenga kuwakomboa Watanzania.
“Ngojeni niwaambie, niliahidiwa ukuu wa
wilaya na uwaziri ilimradi tu nisihame
CCM. Lakini nikaona yote hayo ni upuuzi,
bali cha muhimu ni kuwakomboa
Watanzania, nikaachana nayo yote nikaja
Chadema,” alisema.
Bulaya aliyejigamba kukulia na kufanya
kazi ndani ya CCM, alisema chama hicho
hakina sera zozote za kuwakomboa
Watanzania badala yake kuna za
kuwanufaisha wachache, jambo ambali
yeye na Lembeli hawakulitaka.
Bulaya alitangaza azma yake ya kugombea
ubunge katika Jimbo la Bunda Mjini,
akisema tayari ameshajaza fomu za kuomba
kuteuliwa na chama hicho kugombea nafasi
hiyo.
“Niwaambie tu kwamba nimeshajaza fomu
na kuirejesha na kesho (leo) nitashiriki
kura za maoni. Inshallaah Mungu
akinisimamisha nitagombea nafasi hiyo na
nina uhakika wa kushinda,” alisema
Bulaya.
Akihutubia mkutano huo, Lembeli
aliwataka wakazi wa jimbo hilo kutoipigia
kura CCM katika Uchaguzi Mkuu ujao,
badala yake waichague Chadema kwa nafasi
zote bila kumsahau Bulaya kwa ubunge
kwa kuwa ni mtu mwadilifu.
Mwenyekiti wa Bawacha, Halima Mdee
akihutubia mkutano huo aliwataka
Watanzania wakubali kula fedha
wanazogawa na makada wa CCM ili
wachaguliwe kwa nafasi mbalimbali za
urais, ubunge na udiwani lakini kura zote
waipatie Chadema.

0 comments:

Post a Comment