Serikali ilianzisha mpango wa kujenga shule za sekondari za
kata moja ya mikakati ikiwa kupunguza adha ya umbali kwa wanafunzi na
kusogeza huduma za elimu jirani na wananchi ili kila mtoto apate haki ya
kupata elimu.
Pamoja na mpango huo kutekelezwa kwa asilimia
kubwa, bado adha ya umbali wa shule kwa baadhi ya wanafunzi iko
palepale, hali inayosababisha wanafunzi wengi kuacha masomo.
Shule ya Sekondari Shantamine katika Kata ya
Mtakuja, Geita mjini ni miongoni mwa shule nyingi mkoani Geita na
maeneo mengi nchini ambayo bado wanafunzi wana changamoto ya umbali wa
kuifuata elimu au kurudi nyumbani.
Zaidi ya wanafunzi 27 wameacha masomo kwenye shule hiyo katika kipindi cha miezi mitano tangu kuanza kwa mwaka huu.
Taarifa zinaonyesha kuwa kati ya wanafunzi 200
walioanza kidato cha kwanza katika shule hiyo, waliomaliza kidato cha
nne mwaka jana ni wanafunzi 50.
Takwimu hizo zinamaanisha kwamba wanafunzi 150
waliacha shule huku sababu kubwa ikiainishwa kuwa ni umbali, pia mimba
kwa wasichana.
Kwa mujibu wa taarifa ya Ofisa Elimu wa Mkoa wa
Geita, Eufransia Buchuma aliyoitoa mwaka 2013, wanafunzi 8,606 sawa na
asilimia 50.2 kwa katika Mkoa wa Geita hawakumaliza kidato cha nne
mwaka huo kati ya wanafunzi 17,113 walioanza kidato cha kwanza mwaka
2010.
Mwalimu mkuu wa shule hiyo Kakila Swillah
anabainisha kwamba tatizo hilo ni kubwa katika shule yake akieleza kuwa
limesababisha wanafuzi wawili kuandika barua ya kuomba kuacha shule
mwanzoni mwa mwezi Mei mwaka huu.
“Hii inaonyesha ni jinsi gani tatizo hilo ni
kubwa. Nimekuwa mwalimu mkuu katika shule nyingi, lakini sijawahi kuona
mwananfunzi kwa hiari yake mwenyewe anaomba kuacha masomo kwa kigezo cha
umbali. Hili ni tatizo,”anasema mwalimu huyo.
Anaeleza kuwa changamoto ya umbali imesababisha
shule hiyo kuwa na matokeo yasiyoridhisha kwa wanafunzi, hasa wasichana
ambapo na kwamba tangu kuanzishwa kwa shule hiyo mwaka 2005, haijawahi
kutoa mwanafunzi wa kike aliyefaulu kwenda kidato cha tano na sita, bali
wengi wanafeli.
Wanafunzi wanasemaje?
Zawadi Masibile (16) na Dickson Shilinde(14) ni
miongoni mwa kundi kubwa la wanafunizi walioamua kuacha shule kutokana
na umbali shuleni hapo.
Katika mahojiano na Mwananchi, wanafunzi hao wanaoishi Kijiji
cha Mgusu, umbali wa kilomita 20 kutoka shuleni wanasema kuwa walikata
tamaa kutokana na kuchelewa shule kila siku huku wakitegemea kuomba
lifti barabarani hivyo kuamua kuandika barua kwa mkuu wao wa shule
wakieleza uamuzi wao kuacha shule.
“Kwa kweli maisha ya shule yamenishinda,sioni
umuhimu wa kuendelea na masomo wakati kila siku nachelewa vipindi
darasani. Kama unavyojua, huku kwetu hakuna gari kuna usafiri wa
pikipiki tu unaobeba abiria kuwaleta mjini,” Masibile akionyesha kukata
tamaa na kuongeza:
“Hakuna mwenye pikipiki anayekubali kunibeba mimi
kunileta shule bure, lazima nitoe pesa na wazazi wangu hawana uwezo,
hivyo kila siku natembea kwa mguu zaidi ya kilomita 20 kutoka Mgusu
hadi shuleni, njia yote imejaa mapori, nikihitaji kuwahi natakiwa kuamka
saa 10 usiku kila siku.”
Masibile anafafanua: “Nikichelewa shule, nafikia
kwenye adhabu ya kuchapwa viboko. Iliniumiza sana hali hii, tunatukanwa
na madereva wa pikipiki kila siku tukiwaomba lifti, nyumbani nafika
usiku kila siku, hakuna hata raha ni karaha tu.
“Nikirudi nyumbani usiku sipati muda wa kujisomea,
nafikia kwenye kazi za nyumbani, hapo unalala ukiwa umechoka na unaamka
usiku wa manane kuwahi shule. Unaweza kuamka mapema, lakini ukakosa
usafiri.”
Naye Shilinde anabainisha kilichokuwa kikimuuma
hata kuamua kuacha shule ni kuchelewa vipindi vya asubuhi kila siku na
kuambulia vipindi vya mchana tu huku akidai kwamba pia walimu hawajali
kuwa wanafunzi wanatoka umbali mrefu ba kuwapa adhabu.
Anasema kwamba licha ya kutembea umbali mrefu
kwenda shuleni, siku nzima inaweza kuisha wakitumikia adhabu kwa kosa la
kuchelewa shule, jambo ambalo limekuwa likirudisha nyuma taaluma yake,
hivyo kuona akiendelea kwenda shule ni sawa na kupoteza muda wake.
Siyo Masibilie na Shilinde waliokumbana na adha ya
umbali, bali pia Matokeo Kamuli, mwanafunzi wa kidato cha kwanza
shuleni hapo pia ni anakabiliwa na tatizo hilo.
Anaeleza kuwa kila siku huamka saa 9:00 usiku na
kuanza safari ya kwenda shule akitumia baiskeli, lakini hufika saa
4:30 au saa 5:00 asubuhi kila siku, hivyo pia hukosa vipindi vya
asubuhi na kusoma vipindi vya mchana pekee na kwamba akitoka shule saa
9:00 alasiri hufika nyumbani saa 4:30 usiku kila siku.
Kamuli anaeleza kuwa kijiji chao kimezungukwa na
msitu uliojaa wanyama wakali hivyo kukabiliwa na hatari ya kushambuliwa
na wanyama hao.
“Ikitokea baiskeli imeharibika, basi hujipa likizo
hadi itakapotengemaa, ikitokea siku baiskeli haipo, hatuwezi kwenda
shule kabisa kwa sababu wazazi wetu hawana uwezo wa kutupangia chumba
kama walivyo wengine. Kwa kweli tunapata shida, ukiangalia huko kwetu
hakuna usafiri wa gari, yakiwepo ni ya watu binafsi au maroli ya
mchanga,”alieleza.
Kwa upande wa wanafunzi wanaotoka mjini katika
mkoa huo, wao kilio chao ni usafiri wakidai kwamba madereva wa magari
aina ya Hiace zinazofanya safari za mbali hukataa kuwachukua kwa kile
kinachoelezwa kuwa wakiwapakia wanafunzi wanapata hasara.
“Tunaishi kwa kuomba msaada wa usafiri kwenye magari ya watu
binafsi, magari ya abiria huwa hayatubebi wanafunzi bila pesa, wazazi
wetu hawatupi pesa za usafiri, hivyo siku nyingine tunajikuta tunakosa
lifti hadi saa 4:00 asubuhi, hapo tunaogopa kwenda shule na unaamua
kurudi,”anasema Delisi Ndigeli.
Neema John, mwanafunzi wa shule hiyo anayeishi
mjini, anasema kwamba kila siku huamka saa 11:00 alfajiri ili kwenda
stendi kusubiri usafiri, lakini anaweza kusubiri usafiri hadi saa 4:00
bila kupata gari, hivyo huamua kurudi nyumbani. “Ukiangalia tunakosa
nafasi ya kujisomea, unaamka usiku, unarudi nyumbani usiku. Hupati
nafasi ya kujisomea, hii inakatisha tamaa kwa wanafunzi, wasio na
uvumilivu wanaacha shule,”anasema Neema.
Wazazi wanasemaje.
Shilinde Masanja ni baba wa mwanafunzi Dickson
aliyeandika barua kuacha shule, anaeleza kuwa hapendi mtoto wake aache
shule, lakini mazingira yamemsukuma akubali aache masomo.
“Mwanangu,kama unavyoniona sina uwezo wa kulipa
nauli kila siku Sh4000 siwezi, hiyo ada yenyewe inanipa shida, shule
wanayosoma ni mbali. Labda Serikali itusaidie usafiri kwa wanafunzi kuwe
na mabasi yanayowabeba kuwapeleka shuleni,”anasema akieleza kuwa
umaskini ndiyo sababu kuu ya wanafunzi wao kupata shida huku akiitupia
lawama Serikali kwa kushindwa kujenga mabweni.
“Serikali kama iliamua kusogeza huduma za elimu
kwa wananchi wake basi wafanye utaratibu shule zote za kata ziwe na
mabweni ili kuondoa usumbufu na karaha wanazopata wanafunzi,”anasema
Jonas Matenge.
Mkuu wa Wilaya ya Geita, Manzie Mangochie anasema:”Jukumu la kuhakikisha mtoto anapata elimu bora ni la mzazi.”






0 comments:
Post a Comment