Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema hakiko tayari
kuona kura ya maoni ya katiba mpya ikifanyika kabla au wakati wa
uchaguzi mkuu.
Badala yake kimesema kwamba mchakato wa katiba utapaswa kufanyika
mwakani baada ya serikali mpya kuundwa.Kauli hiyo ilitolewa juzi na
Naibu katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika mjini Mtwara, wakati wa
uzinduzi wa kanda mpya ya
kusini inayohusisha mikoa ya Lindi na Mtwara, katika mkutano wa
hadhara uliofanyika viwanja vya Mashujaa. Alisema kwa kuyafanya hayo,
taifa litakuwa na fursa ya kuwekeza nguvu ya rasilimali, fedha, fikra na
maamuzi kwenye kazi muhimu ya uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga
kura kwa kuandikisha wapiga kura upya na kuwe na muda wa kulihakiki ili
kupata daftari bora.
Alitoa kauli hiyo baada ya Tume ya Uchaguzi (Nec) kutangaza kuwa
uandikishwaji wa wananchi katika daftari la kudumu la wapigakura
utaendelea mpaka Julai na kwamba baada ya kukamilika mkoa wa Njombe,
uandikishaji utaendelea katika mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma na Iringa
kwa pamoja na baadaye kutangaza ratiba ya maeneo mengine.
Mnyika aliwataka wajumbe wa kanda hiyo mpya kukubaliana kumwambia
Mwenyekiti wa Nec kutangaza ratiba inayooyesha tarehe ya kuanza na
kumaliza katika mikoa hiyo minne na wilaya zake.
“Katika mazingira haya ndugu zangu, kauli ya mwenyekiti wa Tume ya
Uchaguzi, pamoja na kujenga matumaini ya wadau kuwa kura ya maoni ya
katiba mpya imeahirishwa, bado haitoshelezi kujibu hoja za msingi
tulizozisema bungeni na Waziri Mkuu akaahidi kwamba kabla ya Pasaka,
ratiba kamili ya uandikishwaji wa wapiga kura itatolewa, lakini
kilichotolewa na tume ni kiashiria cha mikoa itakayofuata baada ya
Njombe,” alisema.
0 comments:
Post a Comment