Wakati Chama Cha Mapinduzi (CCM) kikiendelea kutafakari jinsi
kitakavyompata mgombea wake atakayepeperusha bendera ya urais katika
uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu, Mwenyekiti
mstaafu wa chama hicho mkoa wa Arusha, Yona Merisho Nnko (74), ametoa ya
moyoni akisema adhabu iliyotolewa na chama chao kwa makada sita kwa
madai ya kuanza mapema kampeni za urais, inamlenga zaidi Waziri Mkuu wa
zamani, Edward Lowassa.
Nnko akizungumza na wanahabari nyumbani kwake kijiji cha Kikatiti,
wilayani Arumeru, mwishoni mwa wiki iliyopita, alisema makada wote
waliopewa adhabu na chama hicho anawafahamu, lakini anayemfahamu zaidi
ni Lowassa ambaye pia ni Mbunge wa Monduli kwamba amelegwa zaidi katika
adhabu hiyo.
“Lowassa amehisiwa tu kwamba huenda kutokana na uchapaji kazi,
uaminifu na uhodari wake wa kuchukua hatua na maamuzi magumu, basi
imekuwa nongwa kwa baadhi ya watu wenye chuki ndani ya chama kumzushia
mambo bila ushahidi,” alisema.
Alisema wakiwa na Lowassa mwaka 2005 walihangaika sana bila kulala
ili kuhakikisha mgombea wa CCM wakati huo, Rais Jakaya Kikwete,
anashinda kiti cha urais, na ikawa hivyo.
Alisema hata Rais Kikwete mwenyewe katika nafsi na moyo wake anatambua hilo hata akiamshwa usiku wa manane na kuulizwa.
“Namshauri amuunge mkono ndugu yake lakini asimpendelee,” alisema Nnko ambaye kwa sasa anajishughulisha na kilimo.
Aliwaomba Watanzania wakati ukifika kuhakikisha wanachagua kiongozi atakayejali maslahi yao na ya nchi kwa ujumla.
Alidai kuwa ndani ya chama hicho kwa sasa hakuna anayemfikia
Lowassa kwani anajali makundi yote ya wananchi yakiwamo ya vijana, akina
mama,wazee na watoto. “Lowassa amefanya mengi kwa nchi yetu, naomba
Watanzania muda ukifika tumchague kuwa Rais wetu na mimi namshauri
asiogope muda ukifika achukue fomu agombee kwani wananchi wako nyuma
yake,” alieleza.
Hata hivyo, alisema CCM inayo hazina kubwa ya wagombea ambao wanaweza kufaa kwa nafasi yo yote ya uongozi.
Katika hatua nyingine, Nnko alitoa angalizo kuhusu tabia ya kila
mmoja ndani ya chama hicho kupayuka na kujifanya ‘msemaji’ wa chama.
Alisema tabia hiyo inakidhoofisha chama huku wanachama wakikosa
mweleko, wasijue nani wamsikilize, hali inayotishia kukisambaratisha
kabisa chama ikiwa hali hiyo haitadhibitiwa.
Alisema viongozi wa chama wanatakiwa kujenga utamaduni wa kuwa na
msemaji mmoja badala ya sasa ambapo kila mmoja amekuwa msemaji jambo
ambalo linasababisha chama na wanachama kukosa mwelekeo.
Nnko ambaye alikuwa Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Arusha kwa kipindi
cha miaka 14 mfululizo kuanzia 1993 hadi 2007, alisema vurugu, makundi
ndani ya chama pamoja na chuki miongoni mwa baadhi ya viongozi na
wanachama yanatishia kukisambaratisha chama hicho.
Alisema kitendo cha baadhi ya viongozi wa juu wa chama hicho
kukurupuka na kutoa matamko aliyoyaita ya kupayuka ovyo, huku wakitoa
vitisho kwa baadhi ya wanachama bila kufuata vikao halali ni kujitafutia
umaarufu na kudhoofisha chama.
Alisema zamani wakati chama kikiwa imara na chenye nidhamu, msemaji
wa chama alikuwa mwenyekiti au kama sio yeye basi atatoa kibali maalum
kwa katibu mkuu wa chama na matamshi yote ya chama yanatokana na vikao
sio kupayuka tu. Alisema akiwa kama mwenyekiti mstaafu anaamini Rais
Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM ni kiongozi madhubuti, lakini
baadhi ya viongozi wa juu ndani ya chama wanataka wawe maarufu kuliko
mwenyekiti kwa kupayuka ovyo nje ya vikao.
Alisema CCM kwa wakati huu kinakabiliwa na upinzani mkubwa hali
ambayo inakifanya kuwa dhaifu katika maeneo maeneo mengi hususani ya
kuisimamia serikali ili viongozi wake wafuate sheria, kanuni na maadili.
Februari mwaka jana, Kamati Kuu (CC) ya CCM ilitangaza adhabu dhidi
ya makada wake sita kwa kuwafungia kugombea nafasi za uongozi ndani ya
chama hicho kwa miezi 12, huku pia wakiwa chini ya uangalizi.
Mbali na Lowassa, wengine waliokumbwa na adhabu hiyo baada ya
kuitwa na kujojiwa mjini Dodoma ni Waziri Mkuu mstaafu, Frederick
Sumaye; Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard
Membe; Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira; Naibu
Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba na Mbunge
wa Sengerema, William Ngeleja.
Makada hao walipewa adhabu hiyo baada ya kuitwa na Kamati Ndogo ya
Nidhamu chini ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Philip Mangula,
na kuwahoji kwa tuhuma za kuanza kampeni za uchaguzi mkuu ujao kabla ya
wakati.
Adhabu dhidi ya makada hao ilimalizika Februari mwaka huu, lakini
haijatenguliwa na vikao vya juu vya chama hali inayotia mashaka
kuhusiana na hatma yao.
Baadhi yao wamekwishatangaza nia ya kuingia katika kinyang’anyiro cha urais mwaka huu.
Makada wa CCM wanaotajwa kutaka kuwania urais mwaka huu ni pamoja na Lowassa, Sumaye, Membe na Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta.
Wengine ni Mbunge wa Songea Mjini, Dk. Emmanuel Nchimbi; Ngeleja;
Spika wa Bunge, Anne Makinda; Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Asha-Rose
Migiro; Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), Prof. Mark
Mwandosya na Wasira.
Hadi sasa makada wa CCM waliotangaza nia na wanaotajwa kuwania
urais kupitia chama hicho ni pamoja na Makamba; Naibu Waziri wa Fedha,
Mwigulu Nchemba; Mbunge wa Nzega, Dk. Hamis Kigwangalla; Waziri Mkuu
Mizengo Pinda na Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu.
0 comments:
Post a Comment