KATIBA MPYA: Hakuna kura ya maoni Aprili 30, uboreshaji daftari kukamilika Julai

Author
Tume ya Taifa ya
Uchaguzi (Nec) imekubali kuahirisha
upigiaji Kura ya Maoni ya Katiba
Inayopendekezwa iliyopangwa
kufanyika Aprili 30, mwaka huu
kutokana na kutokamilika kwa
uandikishaji wa Daftrai la kudumu la
wapiga kura kwa kutumia teknolojia
ya Biometric Voters Registration
(BVR).
Hatua hiyo inakuja baada ya kuwepo
mfululizo wa matamko na ushauri
kutoka kwa wadau mbalimbali wa
demokrasia kwamba zoezi hilo
lisingewezekana kwa sasa hasa
kutokana kusuasua kwa mwenendo
wa BVR.
Mwenyekiti wa Nec Jaji Mstaafu
Damian Lubuva aliwaambia
waandishi wa habari jijini Dar es
Salaam leo kuwa kazi ya uboreshaji
daftari la wapiga kura ni ya msingi
kabla ya taratibu zote za upigaji kura.
Jaji Lubuva aliyeonekana kuwa mpole
zaidi, alisema kwa uzoefu walioupata
Njombe, zoezi la uboreshaji wa daftari
la kudumu la wapiga kura bado
halijakamilika katika mkoa huo na
mingine iliyosalia.
“Hivyo tume haitaweza kuendelea na
zoezi la upigaji kura ya maoni na zoezi
hilo lililotangazwa hapo awali
kufanyika Aprili 30, 2015
limeahirishwa hadi tarehe
itakapotangazwa na Nec baada ya
kushauriana na Tume ya Uchaguzi ya
Zanzibar,” alisema Jaji Lubuva.
Kwa nyakati tofauti, vyama vya siasa,
asasi za kiraia, taasisi za kidini na
wananchi wamekuwa wakiishauri Nec
kuahirisha Kura ya Maoni huku
vyama vya siasa vikimtaka Rais
Jakaya Kikwete atii makubaliano
yaliyofikiwa na Kituo cha Demokrasia
(TCD) mwaka jana ya kuahirisha zoezi
hilo hadi baada ya Uchaguzi mkuu.
Jaji Lubuva alisema kuwa tume yake
inaendelea kuboresha daftari la
wapiga kura nchi nzima ambapo
wanatarajia kukamilisha ifikapo Julai
mwaka huu. Nec ilieleza kuwa baada
ya kumaliza uandikishaji mkoani
Njombe watahamia mikoa ya Ruvuma,
Lindi, Mtwara na Iringa.

0 comments:

Post a Comment