Katika mkakati huo, chama hicho kimeigawa nchi
katika kanda 10 za utekelezaji huku kikijipanga kuimarisha nguvu zaidi
katika Jiji la Dar es Salaam lenye idadi kubwa ya wapigakura.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema
wakati wa uzinduzi wa mkakati huo kitaifa jijini hapa kuwa watafundisha
viongozi wote wa chama hicho na watangaza nia, mbinu za uongozi bora na
namna ya kushinda.
Mbowe alisema mpango huo wa mafunzo ni sehemu ya
utekelezaji wa maazimio ya chama kwa kuwa hawawezi kushika Serikali Kuu
na Serikali za Mitaa bila kuwa na viongozi bora na weledi.
Alisema Chadema kitakwenda katika kanda zote,
majimbo ya kichama 242, kata 4,852, matawi 22, 749, misingi 64,803 na
kuwafikia viongozi 224,287 na timu zote za mafunzo zimeshatawanyika nchi
nzima.
“Tunawafundisha viongozi wetu walio tayari ndani
ya chama au Serikali za Mitaa namna ya kutekeleza wajibu wao. Lakini
tunawaimarisha wanaokusudia kugombea nafasi mbalimbali kuwa wagombea
wazuri zaidi, kuandaa ajenda za chama na namna ya kukamata madaraka kwa
kuwa safari ya kushika Dola 2015 haina kizuizi,” alisema Mbowe huku
akishangiliwa.
Kuahirisha uchaguzi
Katika mkutano huo uliohudhuriwa na mamia ya
viongozi na watia nia wa Kanda ya Pwani ya chama hicho, Mbowe aliitaka
Serikali kutojaribu kabisa kuahirisha Uchaguzi Mkuu kwa sababu ya
kusuasua kwa uandikishaji wa daftari la kudumu la wapigakura kwa kutumia
teknolojia ya Biometric Voters Registration (BVR) akitishia kuwa ‘moto
utawaka’.
Alisema Ukawa hawakusema chochote wakati wa Tume
ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ilipoahirisha Kura ya Maoni ya Katiba
Inayopendekezwa kwa kuwa ilikuwa batili na ilianzishwa kwa masilahi ya
Serikali na aliahirishwa na wao wenyewe.
Aliitaka Serikali kuharakisha uandikishaji wa
daftari la kudumu la wapigakura kwa kuwa imesalia miezi mitatu na nusu
kabla ya kuanza kwa kampeni za Uchaguzi Mkuu hapo Agosti.
Alisema tarehe ya kupiga kura ambayo ni Jumapili
ya Oktoba ilifahamika tangu awali kwa kuwa ni ya kikatiba lakini mpaka
sasa uandikishaji unasuasua katika Mkoa wa Njombe wenye wapiga kura
340,000 ambao alisema hawafiki hata nusu ya waliopo Jimbo la Ubungo.
“Wanasubiri kama walivyofanya kwenye kuahirisha
Kura ya Maoni na ili waseme ‘ndugu Watanzania kwa kuwa tumechelewa
kuandikisha wapigakura tunaomba Bunge lako tukufu liongezee muda kwa
Serikali ya awamu ya nne’... mtakubali?” aliwahoji wafuasi hao na
kujibiwa “Hapanaaaa”.
“Serikali ikijaribu tu kuahirisha uchaguzi, nchi itawaka moto.
Ikifika tarehe 25 Oktoba, Rais Jakaya Kikwete nenda Msoga (Bagamoyo)
ukapumzike utuachie Ukawa na nchi yetu.”
Kuimarisha ngome Dar
Katika kile ilichoita kuimarisha ngome yenye kura
nyingi, Chadema imetoa maazimio matatu kwa viongozi na wafuasi wake wa
Dar es Salaam kuhakikisha inashika nafasi zote za uongozi hapo Oktoba.
Alisema jiji hili siyo tu makao makuu ya Serikali,
balozi za nchi mbalimbali, au kitovu cha mapato, bali lina majimbo saba
ya kwanza kwa idadi kubwa ya wapigakura kuliko mkoa wowote nchini,
hivyo kusiwe na utani katika kutekeleza mikakati ya ushindi.
Mbowe, aliyesubiriwa kwa hamu tangu saa tatu
asubuhi na kufika saa 6.05, alisema Jimbo la Ubungo ni la kwanza na lina
wapigakura wengi kuliko hata mikoa ya Njombe na Katavi.
Akishirikiana na viongozi hao, Mbowe aliweka
maazimio kuwa, Ukawa wanatakiwa kushinda majimbo yote, nafasi zote za
umeya na madiwani ili kudhibiti mapato na kuleta maendeleo.
“Dhamana kubwa ya Taifa hili inawategemea wana Dar
es Salaam, kazi tutakazozifanya kuanzia leo hadi siku ya uchaguzi
zitasaidia nchi hii kubadilika au kuendelea kuwa na Serikali ya mabavu
ya CCM,” alisema.
Alia kuzuia mpasuko
Kuhusu ugawanaji madaraka ndani ya Ukawa, Mbowe
aliwataka makada hao kuvumiliana na kuzishinda changamoto zinazowakabili
na kuwa Chadema na viongozi wa umoja huo wanaendelea vizuri na mipango
ya ushindi.
Aliwaeleza wafuasi hao kuwa licha ya watu kuwaombea mabaya, wao hawatagombana zaidi ya kuungana kuing’oa CCM.
Alisema wanaotangaza nia wapo wengi kuliko nafasi
zilizopo na atapatikana mmoja katika kila nafasi na watakaozipata,
itakuwa kwa misingi ya haki na siyo dhuluma.
“Wale wote watakaokosa nafasi za kugombea ubunge
na udiwani watambue kuwa vita tunavyopigana Chadema na Ukawa siyo ya
kugombea madaraka. Bado wana nafasi kubwa ya kulitumikia Taifa hili
kupitia Serikali yetu ya ushirika,” alisema.
Huku akishangiliwa na kuonyesha kujiamini, Mbowe aliongeza:
“Tunahitaji watendaji wa Serikali, ndiyo nyinyi… msifikiri fursa ni
ubunge pekee, zipo nyingi lakini zipatikane kwenye misingi ya haki,
uwazi na kuheshimiana.”
Mbowe alibainisha kuwa CCM hawatakiwi kugombana
huku wakitegea kusubiri mgombea wa Ukawa atangazwe ili wamtangaze wa
kwao, wakifanya hivyo watasubiri sana na kwamba mgombea wa ushirika wao
atatoka muda ukifika.
Ziara ya Dk Slaa
Akimkaribisha Mbowe, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema,
John Mnyika alisema Tanzania inahitaji viongozi makini watakaoweza
kukiondoa CCM madarakani.
Huku akishangiliwa, Mnyika alisema lengo kuu la
chama hicho ni kushika dola Oktoba mwaka huu, ndiyo maana Katibu Mkuu,
Dk Willibrod Slaa yuko Marekani kwa ajili ya kuzungumza na Watanzania
waishio huko na kuimarisha uhusiano na mataifa rafiki kwa kuwa Chadema
kitashika dola.
Akizungumzia ziara hiyo, Mjumbe wa Kamati Kuu ya
Chadema, Mabere Marando alisema Dk Slaa yuko ughaibuni kuyafuta
yaliyofanywa na Serikali ya Rais Kikwete ili Ukawa iweze kuwa na
uhusiano mzuri na nchi za kigeni.
Ongezeko la madiwani
Mnyika alisema kuongezeka kwa madiwani wa upinzani
katika mabaraza ya madiwani na wabunge Dar es Salaam, kumeonyesha
ufanisi katika kusimamia fedha za umma tofauti na hali iliyokuwa kabla
ya 2010.
“Baada ya kuongezeka kwa wabunge wa upinzani
katika Manispaa ya Kinondoni, mapato ya ndani ya manispaa yaliongezeka
kutoka Sh7 bilioni mwaka 2010 mpaka Sh35 bilioni hivi sasa,” alisema
Mnyika ambaye anakaimu nafasi ya Katibu Mkuu.
Mbunge huyo alisema ufanisi unajitokeza kwa sababu
viongozi wa Chadema wanafanya kazi kubwa ya kusimamia rasilimali za
Taifa na kuhakikisha haziibwi.
Alisema mabadiliko yameanza kuonekana baada ya
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka jana ambao Chadema ilishinda
mitaa 93 iliyopo Dar es Salaam kutoka mitatu kiliyoshinda mwaka 2009.
“Lengo letu si kuongeza idadi ya madiwani kwa
ajili ya kuwa wapinzani, bali kuwa na madiwani wengi katika manispaa ya
Kinondoni ili meya atoke Ukawa kuiongoza halmashauri,” alisema Mnyika
huku wanachama wakimshangilia.
Uimara wa Ukawa
Marando ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Kanda ya
Pwani, alisema Ukawa ni muungano ambao CCM haina ubavu wa kupambana nao
na kwamba umedhamiria kukiondoa madarakani ili kurudisha rasilimali za
nchi kwa wananchi.
Alisema wananchi wamechoshwa na dhuluma za
Serikali ya CCM na kusisitiza kuwa Chadema kina viongozi wengi makini na
wazalendo ambao watarejesha uhuru na haki kama alivyopigania Mwalimu
Julius Nyerere.
“Wananchi wamechoshwa na miaka 50 ya CCM
madarakani na mwisho wao ni Oktoba. Wanachotaka wananchi ni watu wenye
nyota ya uongozi, ndiyo maana tumeanzisha mpango huu wa mafunzo,”
alisema Marando.
Mwalimu na ziara ya ushindi
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema - Zanzibar, Salum
Mwalimu alisema hiyo ni awamu ya pili ya kutoa mafunzo ambayo
yatafanyika katika kanda za Victoria na Nyanda za Juu Kusini na Pwani na
kubadilishana katika kanda zilizosalia.
Alisema wameunda vikosi vitatu vitakavyozunguka
katika maeneo hayo. Kikosi cha kwanza kitakwenda Kanda ya Serengeti
inayojumuisha mikoa ya Mara, Shinyanga na Simiyu. Kikosi hicho
kitakachokuwa chini ya Mnyika kitaendelea na mafunzo katika mikoa ya
Mwanza, Kagera na Geita.
Kikosi cha pili kitakuwa chini Mwalimu mwenyewe na
kitakwenda Kanda ya Nyanda za Juu Kusini inayojumuisha mikoa ya Mbeya,
Rukwa, Njombe, Iringa, Morogoro na kuhitimishwa Dar es Salaam.
Mwalimu alisema kikosi cha tatu kitaongozwa na
Makamu Mwenyekiti wa Chadema – Tanzania Bara, Profesa Abdallah Safari na
kitatoa mafunzo katika mikoa ya Pwani na Tanga.
“Kuanzia Jumamosi itakuwa ni hakuna kulala, hakuna
kula, mpaka kieleweke. Ziara hii ya mafunzo itakuwa ni moto nchi
nzima,” alisema Mwalimu huku wanachama wakipiga makofi.
0 comments:
Post a Comment