Wabunge wa upinzani wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) jana
walianzisha tafrani bungeni na kusababisha kikao cha Bunge kuvunjika saa
5.18 asubuhi baada ya kusimama na kupaza sauti wakishinikiza Serikali
itoe kauli juu ya hatima ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la
Wapigakura na upigaji wa Kura ya Maoni kupitisha Katiba Inayopendekezwa.
Huku wakiwa wamesimama walikuwa wanapiga kelele wakisema, ‘hatutaki
kuburuzwa’, ‘tumechoka kupelekeshwa’, Watanzania wapo njia panda’ na
‘tunataka majibu,’ ‘Bunge lisitumiwe kuilinda Serikali’, ‘Waziri Mkuu
yupo bungeni kwa nini asitoe kauli’ na maneno mengine mengi bila
mpangilio.
Wabunge hao wa vyama vya NCCR-Mageuzi, Chadema na CUF, kwa umoja wao
walimtaka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kutoa majibu hayo muda huohuo,
kabla ya jioni kutoa hutuba na kuahirisha mkutano huo wa 19 wa Bunge.
Baadaye jana usiku katika hotuba yake ya kuahirisha Bunge hadi Mei 12,
utakapoanza Mkutano wa 20, Waziri Mkuu Pinda alisema Tume ya Taifa ya
Uchaguzi (NEC) itatoa taarifa siku za hivi karibuni kuhusu upigaji wa
kura ya maoni.
“Ni dhahiri muda uliobaki kuanzia sasa ni mfupi lakini Tume ndiyo itakayotujulisha ratiba kamili,” alisema.
Sakata lilivyoanza
Kelele hizo zilitokana na hoja za wabunge wawili, Suleiman Jafo wa
Kisarawe na yule wa Ubungo, John Mnyika waliotaka Bunge lisitishe
shughuli zake zote lijadili suala hilo kwa kuwa ni muhimu na Taifa
halielewi hatima yake, wakati Bunge lilikuwa linaahirishwa jana.
Spika wa Bunge, Anne Makinda alikataa suala hilo kujadiliwa, akisema ni
hoja iliyowasilishwa katika mkutano uliopita, akataka Bunge liendelee na
shughuli zake, lakini wabunge wa upinzani walikataa kukaa na
wakaendelea kupaza sauti.
Hata alipobadili kauli akasema, “nimesema kauli itatolewa, wabunge hao
walisisitiza itolewe papohapo. Hata alipowataka waondoke ndani ya ukumbi
huo, wabunge hao ambao ni wachache ukilinganisha na wale wa CCM,
walikataa, wakisema; “hatutoki hadi kauli itolewe.”
Kelele za wabunge hao zilimfanya Spika Makinda kutoa kauli kali, “Njooni
mwendeshe (kikao) nyinyi basi. Njooni hapa mkae tena wote.”
Baada ya kuona kelele hizo zimedumu kwa dakika tatu, Spika Makinda
alilazimika kusitisha shughuli za Bunge hadi baadaye (jioni), bila
kutaja muda ambao Bunge lingerejea na kuwaacha wabunge wakiwa wamesimama
katika makundi ndani ya ukumbi wakijadili tukio hilo.
Jafo ndiye aliyeanza kuomba mwongozo wa Spika akitaka chombo hicho cha
kutunga sheria kisitishe kujadili jambo lolote lile, badala yake
kijadili mustakabali wa Katiba Mpya, akitaka Serikali iwasilishe muswada
wa sheria kwenye mkutano wa 20 wa Bunge (wa Bajeti) ili Katiba ya Mpito
ipitishwe.
Jafo alitaka Katiba Inayopendekezwa ipitishwe kwa mpito ili kuondoa
sintofahamu ya watu wanaotaka kuwapo mgombea binafsi, kupinga matokeo ya
urais mahakamani, kuweka ukomo wa Bunge na wabunge na kuwapo kwa Tume
huru ya uchaguzi.
Alisema mambo hayo manne ambayo yamekuwa yakipigiwa kelele yamo katika
Katiba Inayopendekezwa, hivyo ni vyema ikapitishwa kwa mpito ili mambo
hayo tu manne yatumike katika Uchaguzi Mkuu.
Alisema wananchi wamejitokeza kwa wingi kujiandikisha kwenye daftari la
kudumu la wapiga kura lakini kuna changamoto za upungufu wa vitendea
kazi, zikiwamo mashine za kielektroniki za Biometric Voters Registration
(BVR).
Alisema kutokana na hali hiyo, ni vigumu upigaji Kura ya Maoni ya Katiba
Inayopendekezwa kufanyika Aprili 30, mwaka huu kama ilivyopangwa.
Alisema upigaji kura ya maoni lazima utanguliwe na utoaji wa elimu kwa
mpigakura, jambo ambalo kwa muda uliobaki ni vigumu kufanyika.
“Tutumie mkutano wa 20 tuhakikishe Serikali inaleta muswada wa hati ya
dharura ili Bunge lipitishe katiba ya mpito, kwa sababu Taifa sasa hivi
lipo katika hali tete kila mtu anasema lake. Endapo tutafanya hivyo
tutakuwa na katiba ya mpito ya kati ya miezi sita hadi 12, itaturuhusu
kufanya uchaguzi na baadaye watu watakwenda kwenye Kura ya Maoni wakiwa
wamepata elimu ya kutosha juu ya Katiba Inayopendekezwa.”
Alisema uamuzi huo utalinusuru Taifa na si busara kuruhusu nchi kuingia katika kura ya maoni huku kukiwa na mvutano.
Baada ya kauli ya Jafo, Spika Makinda alisema: “Ulichokizungumza wala
siyo utaratibu. Kwanza suala hilo litatolewa ufafanuzi jioni wakati
Waziri Mkuu akiahirisha Bunge.”
Wakati Jafo akiomba mwongozo huo, Halima Mdee (Kawe - Chadema), John
Mnyika (Ubungo - Chadema), Felix Mkosamali (Muhambwe - NCCR), Moses
Machali (Kasulu Mjini - NCCR), Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini -
Chadema) na Mbatia walisimama bila kufuata utaratibu na kupaza sauti
wakipinga mwongozo huo.
“Hivi huyu katumwa au nini. Anazungumza vitu gani humu ndani,” alisema
Mdee na kuungwa mkono na Machali, huku wakitakiwa kukaa chini na
Makinda.
Baada ya kutulia kwa mvutano huo uliodumu kwa takribani dakika nne,
Mnyika aliomba mwongozo wa Spika kwa kutumia kanuni ya 47 (1) na kusema:
“ Mpaka sasa uandikishaji wa wapigakura nchi nzima haujakamilika hata
katika mkoa mmoja tu wa Njombe. Watanzania wapo katika sintofahamu
kuhusu ni lini wataandikishwa kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura.”
Aliongeza, “Jambo hili ni la dharura kwa sababu limeshatolewa hoja ya
dharura katika mkutano uliopita wa Bunge, ukaagiza (Spika) kamati ya
bunge ilishughulikie, majibu yatolewe kwenye mkutano huu wa Bunge. Leo
hii (jana) mkutano unakwenda kufungwa bila majibu kutolewa.”
Mnyika alitaka shughuli zote za Bunge kwa siku ya jana zisitishwe na majibu juu ya masuala hayo mawili yapatikane.
“Nimeomba miongozo juu ya jambo hili mara mbili na mara zote Serikali
kupitia kwa Waziri Mkuu umeipa maelekezo ya kutoa majibu lakini inakwepa
kutoa majibu,” alisema.
Alisema kwa mazingira hayo, hakuna sababu ya kuendelea na mjadala wowote
katika kikao hicho cha Bunge mpaka majibu yapatikane, akisisitiza kuwa
kwa mujibu wa Ibara ya 63 (2) ya Katiba ya nchi, kazi ya Bunge ni
kuishauri Serikali.
Huku akimnyooshea kidole Pinda Mnyika alisema: “Waziri Mkuu (Pinda) yupo hapa anaweza kutoa majibu na tukajadili jambo hili.”
Baada ya Mnyika kuwasilisha mwongozo wake, Makinda alisema: “Hoja ya
Mnyika inafanana na ile iliyotolewa na Jafo. Tuendelee Katibu
(akielekeza kuendelea na ratiba za Bunge).”
Katibu wa Bunge alianza kusoma miswada minne iliyokuwa ikisomwa kwa mara
ya kwanza, ikiwamo miwili ya habari na hapo ndipo wabunge hao wa
upinzani waliposimama na kuanza kupiga kelele.
Wakiwa wamesimama, wabunge hao walianza kupaza sauti, akianza Machali
ambaye aliwasha kipaza sauti kuwa, “Hoja hii haifanani kabisa na ile ya
(Jafo), ile ya kwanza inataka majibu mkutano wa 20 na hoja hii ya pili
inataka majibu katika kikao hiki cha leo”.
Majibizano
Mnyika: Hoja hii itolewe majibu na Waziri Mkuu yupo hapa. Atoe majibu
Machali: Tunataka majibu, tumechoka kuburuzwa.
Makinda: Anawaburuza nani, nimewaambia kwamba swali lile litajibiwa leo
(jana) na Waziri Mkuu. Waziri kivuli njoo usome hotuba ya kambi ya
upinzani.
Huku wabunge hao wakiwa bado wamesimama, Spika alimwita waziri kivuli wa
Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, ili asome maoni ya kambi
hiyo juu ya Mswada wa Sheria ya Miamala ya Kielektroni ya mwaka 2014 na
ule wa Makosa ya Kimtandao wa mwaka 2015.
Hata hivyo, msemaji huyo hakwenda kusoma maoni yake na badala yake
wabunge hao waliendelea kusimama na kushinikiza kutaka majibu kutoka kwa
waziri mkuu.
Baada ya kuona hali hiyo inaendelea, Makinda aliahirisha kikao hicho na
kiliporejea saa 10 jioni, hoja hizo hazikuendelea, badala yake miswada
iliendelea kujadiliwa. Habari zilizopatikana zilieleza kuwa Kamati ya
Uongozi ilikutana na kukubaliana majibu yatolewe katika hotuba ya
kuahirisha Bunge.
Nje ya ukumbi
Wakiwa nje ya Ukumbi wa Bunge, Mbunge wa kuteuliwa (NCCR-Mageuzi), James
Mbatia na mwenzake wa Bariadi Mashariki (UDP), John Cheyo walisema
wanachokitaka kwa Serikali ni kauli tu juu ya suala hilo na si jambo
jingine.
Tofauti na ilivyozoeleka kwamba wangeitana na kukaa kikao cha Kambi ya
Upinzani, wabunge hao baada ya kutoka bungeni kila mmoja aliondoka zake,
huku wakisikika wakiambiana, “Tukutane baadaye bungeni.”
Baadaye, Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashillilah alisema Bunge
lingeendelea saa 10 jioni, huku akitupa lawama kwa upinzani kwamba
walifanya makosa kugomea kuendelea kwa kikao cha Bunge, badala yake kama
walikuwa na hoja walitakiwa kuiwasilisha kwa Spika.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment