Siku moja baada ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana
kuwapokea viongozi wawili akisema wanatoka Chadema na kumtuhumu Mbunge
wa Arusha, Godbless Lema kuwa anatumia madaraka yake kujinufaisha na
mali za umma, mbunge huyo amejibu akisema: “Kinana amepigwa changa la
macho.”
Akiwa Arusha mwishoni mwa wiki Kinana aliwapokea
waliokuwa wenyeviti wa Chadema katika Wilaya ya Monduli, Amani Silanga
na wa Ngorongoro, Revocatus Palapala lakini jana Lema alisema viongozi
hao walikwishatimuliwa Chadema tangu mwaka 2013.
Kinana alisema migogoro ya CCM ndiyo
iliyokinufaisha Chadema na Lema akaingia madarakani, lakini akawataka
wananchi kujutia uamuzi huo na kutorudia kumchagua mbunge huyo.
“Mbunge wenu ameshindwa kutekeleza kile
mlichomtuma bungeni badala yake anatumia madaraka yake kujimilikisha
mali za umma na kutukana hovyo,” alisema na kuongeza:
“Mfano ni lile shamba alilopewa na Mayala ambalo
ameliuza, trekta na vifaa vingine vyote ameviuza lakini migogoro ya
ardhi na maji ameshindwa kuitatua.”
Majibu ya Lema
Akijibu tuhuma hizo, Lema alisema Kinana amepigwa
‘changa la macho’ na amefanyiwa maigizo kama ya futuhi na watu wa
usalama wameshindwa kumwambia ukweli.
Alisema mambo yote aliyoambiwa ni uongo mtupu ambao yeye hawezi kusumbuka nao.
“Kama mimi ni mwizi na tapeli, hivi hata usalama
wanashindwa kuwaeleza ukweli washughulike na mimi? Ndiyo maana watu
tuliowafukuza Chadema wamewapokea eti wamehama chama. Wameingizwa mjini
hao,” alisema.
Alisema: “Silanga na Palapala walifukuzwa tangu
Novemba 30, 2013 baada ya kubainika kuwa kwenye mtandao wa Zitto na wote
walitimkia ACT kama walivyofanya kina Mwigamba (Samson) na Kitila
Mkumbo,” alisema Lema akitoa nakala ya taarifa kwa vyombo vya habari.
Alisema baadaye Silanga na Palapala walijiunga CCM
na Palapala aligombea na kushinda uenyekiti wa Kijiji cha Wasso
wilayani Ngorongoro kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa Desemba 14,
mwaka jana.
“Ni maajabu ya mwaka mwenyekiti wa kijiji kupitia
CCM tangu Desemba 14, mwaja jana, apokewe na Kinana akitangazwa kukihama
Chadema?” alisema Lema.Mbunge huyo alisema taarifa kwa vyombo vya habari ya Novemba 30, mwaka
juzi, iliyosainiwa aliyekuwa Katibu wa Chadema Mkoa wa Arusha, Amani
Golugwa na habari iliyoandikwa kwenye gazeti la Daily News la Desemba 2,
2013, vyote vinaelezea kufukuzwa kwa Silanga.
0 comments:
Post a Comment