Usajili ligi kuu Tanzania bara

Author

KLABU 14 zipo katika kupigana vikumbo kwa ajili ya kuviboresha vikosi vyao kabla ya kufungwa kwa pazia la dirisha dogo la usajili Desemba 15 mwaka huu.

Hadi kufikia sasa klabu kongwe na zenye uwezo wa kifedha za Simba, Yanga na Azam ndizo zinazoongoza katika kusajili nyota hasa pengine ni kutokana na kuanza vibaya kwa timu hizo katika mechi saba za awali.
Serge Wawa- Azam FC
Huyu ni mchezaji mpya wa kimataifa kutoka Ivory Coast, hadi sasa usajili wa Wawa umekamilika kwa asilimia zote akijiunga na mabingwa hao watetezi akitokea kwa mabingwa wasoka Afrika Mashariki na Kati El Marreikh ya Jamuhuri ya Sudan.
Wawa ni mmoja wa mabeki mahiri na juhudi zake akiwa na El Marreikh ndizo zilizomvutia kocha wa Azam, Joseph Omog kumsajili kwenye kikosi chake kwa ajili ya kuongeza nguvu za kutetea ubingwa wao na kufanya vizuri kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa ambayo watashiriki Januari mwakani.
Amri Kiemba-Azam
Kiungo wa kimataifa wa timu ya taifa ya Tanzania na klabu ya Simba, Amri Kiemba usajili wake wa kujiunga na Azam FC kwa mkopo umekamilika na tayari mchezaji huyo ameshaanza mazoezi na kikosi hicho cha kocha Omog.
Kiemba amekuwa mchezaji wa pili kujiunga na Azam katika usajili huu wa dirisha dogo baada ya ule wa Wawa kukamilika wiki mbili zilizopita kocha Omog alifanikiwa kukata kiu yake baada ya kunyakua kiungo huyo aliyesimamishwa na Simba ili aweze kusaidiana na kina Kipre Tchetche, Kipre Balou na Didier Kavumbagu.
Masoud Chile- Ndanda FC
Kiungo huyo wa zamani wa Mtibwa Sugar amejiunga na vijana wa Ndanda FC katika dirisha dogo la usajili kama mchezaji huru baada ya kukosa timu kwa miezi sita tangu alipoachwa na Mtibwa mwishoni mwa msimu uliopita. Kutua kwa Chile katika kikosi cha Ndanda FC, kunaweza kubadili mwenendo wa timu hiyo katika ligi na kuifanya iweze kupata matokeo mazuri na kuondoka katika nafasi za mkiani iliyopo kwa sasa.
Charles Mishetto -Stand United
Mapema wiki hii Mkurugenzi wa ufundi wa klabu ya Stand United Muhibu Kanu alifanikisha usajili wa mshambuliaji Charles Mishetto ili kuboresha safu yao ya ushambuliaji ambayo imefunga mabao manne tu katika mechi saba za awali.
Mishetto anakuwa mchezaji wa kwanza kujiunga na Stand United katika dirisha dogo la usajili akitokea Ujerumani alipokuwa akicheza soka katika Ligi daraja la nne na kiwango chake kimemvutia kocha Emmanuel Masewe na kuutaka uongozi wake kukamilisha usajili huo.
Betram Mwombeki- Ruvu Shooting
Huyu ni mshambuliaji mwenye umbo refu aliyewahi kutamba na kikosi cha Simba msimu uliopita kabla ya kutupiwa virago na aliyekuwa kocha wa timu hiyo Mcroatia Zdravko Logarusic na kumfanya awe nje ya uwanja kwa miezi sita bila kupata timu ya kuchezea.
Lakini kiwango alichokionesha mshambuliaji huyo wakati akiwa Simba kilimshawishi kocha wa Maafande wa Ruvu Shooting kumhitaji mchezaji huyo mwenye umbo refu kwa ajili ya kukiongezea nguvu kikosi chake katika usajili huu mdogo. Tayari Mwombeki ameshakubaliana kila kitu na uongozi wa Ruvu Shooting na kilichobaki ni mchezaji huyo kusaini fomu za timu hiyo ili aanze kuitumikia wakati ligi itakapoendelea.
Emerson de Oliveira Neves Roque – Yanga
Huyu ni kiungo mpya Mbrazili aliyeletwa Yanga kwa ajili ya kufanya majaribio ili aweze kusajiliwa na mabingwa hao wa zamani kuziba nafasi ya Geilson Santana Santos ‘Jaja’ aliyekatisha mkataba wa kuendelea kuichezea timu hiyo kwa matatizo ya kifamilia.
Usajili wa Emerson kujiunga na Yanga huenda ukakamilika ndani ya wiki hii kutokana na imani ya kocha Marcio Maximo kwa kiungo huyo kuwa kubwa na inadaiwa huenda akasaini mkataba wa miaka miwili kama ilivyokuwa kwa Mbrazili mwenzake Andrey Coutinho.
Said Morad - Simba
Huyu ni beki wa kati wa Azam FC, ambaye hivi karibuni amekuwa akiitoa udenda klabu ya Simba iliyo na mapungufu katika nafasi hiyo. Uongozi wa Simba umekuwa katika mazungumzo yasiyokuwa na mafanikio na wenzao wa Azam ili kumsajili hata kwa mkopo beki huyo ili akasaidiane na mkongwe Joseph Owino ‘Gera’ kumlinda kipa wao Ivo Mapunda lakini haijajulikana mazungumzo hayo yamefikia wapi.
Huenda Azam wakamruhusu Morad akajiunga na Simba katika usajili huu mdogo ili akapate nafasi ya kucheza kwa sababu mchezaji huyo kwa muda mrefu amekuwa akisugua benchi mbele ya Agrrey Moris na David Mwantika na wiki iliyopita amesajiliwa beki mwingine wa kati Wawa ni wazi beki huyo atapoteza nafasi hata ya kukaa benchi.
Mohamed Traore – Azam FC
Mshambuliaji wa kutumainiwa wa klabu ya El Marreikh ya Sudan huenda akajiunga na mabingwa watetezi Azam FC, katika kipindi hiki cha dirisha dogo la usajili. Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba alisema mazungumzo yao na uongozi wa El Marreikh kwa ajili ya kumchukua mchezaji huyo yamefikia pazuri na kuna uwezekano Traore akaungana na Wawa katika kipindi hiki cha usajili mdogo.
Deusi Kiseke- Simba
Winga wa pembeni wa klabu ya Mbeya City anahusishwa kujiunga na klabu ya Simba katika kipindi hiki cha dirisha dogo la usajili kutokana na vyombo vya habari kumzungumzia mchezaji huyo kuwa hana furaha kwenye timu yake ya sasa. Simba imekuwa na mwanzo mbaya tangu kuanza kwa msimu huu na kocha Patrick Phiri amekuwa na machaguo mengi katika kipindi hiki cha usajili mdogo ili kuimarisha kikosi chake na mara kadhaa amemtaja Kiseke akimuhitaji kufanya naye kazi.
Said Bahanuzi- Stand United
Bahanuzi huenda akajiunga na Stand United katika usajili huu mdogo baada ya klabu ya Stand United kuwasilisha barua kwa uongozi wa mabingwa hao wa zamani wakimhitaji mshambuliaji huyo aliyekosa namba kwenye kikosi cha kocha Maximo.
Mkurugenzi wa Ufundi wa Stand United, Muhib Kanu, amesema ana matumaini makubwa ya Yanga kumruhusu mchezaji huyo akajiunga kwa mkopo na timu yao ili aweze kuimarisha kiwango chake na kuisaidia timu yao.

0 comments:

Post a Comment