
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imefuta ada ya wanafunzi wa shule
za msingi, ikiwa ni utekelezaji wa dhamira ya mapinduzi ya kuwapatia
wanafunzi wote elimu bure, kama ilivyoasisiwa na Rais wa Kwanza wa
Zanzibar, Abeid Amaan Karume. Uamuzi huo ulitangazwa rasmi jana na Rais
Ali Mohamed Shein, wakati akihutubia wananchi katika uwanja wa Amaan
katika kilele cha maadhimisho ya miaka 51 ya Mapinduzi ya Zanzibar ya
mwaka 1964. Rais Shein alisisitiza kwamba, kuanzia sasa Serikali inafuta
ada ya wanafunzi wa shule za msingi walizokuwa wakitoa wazazi, ikiwa ni
malengo ya kutekeleza dhamira ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuwapatia
wanafunzi wote elimu bure, kama ilivyoasisiwa na hayati Karume na
kutangazwa Septemba 23, mwaka 1964. Aidha Dakta Shein amebainisha
kwamba, mafanikio makubwa yaliyopatikana katika sekta za elimu, afya na
usambazaji wa nishati ya umeme, ni mambo ambayo yalikuwa moja ya
vipaumbele, vilivyowekwa katika Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964.
0 comments:
Post a Comment