Fainali hiyo inatarajiwa kuchezwa kuanzia saa 2:15 usiku na mgeni rasmi atakuwa Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein.
Mchezo huo wa fainali ambao umevuta hisia za mashabiki wa wadau wengi wa soka unatarajiwa na upinzani wa hali ya juu kutokana na timu hizo kutaka kulipizana kisasi hasa kwa upande wa Simba ambao katika mechi yake ya makundi ilifungwa bao 1-0.
Timu hizo zimefika hatua hiyo baada ya Simba kuifunga Polisi Zanzibar bao 1-0 na Mtibwa kuifunga JKU kwa mikwaju ya penalti 7-6 katika mechi za nusu fainali.
Akizungumzia mechi hiyo Kocha Mkuu wa Simba, Goran Kopunovic alisema anachotaka ni kushinda ili atwae ubingwa na kulipa kisasi kwa Mtibwa Sugar ambayo iliifunga bao 1-0 katika mechi ya makundi ya michuano hiyo.
“Mechi itakuwa ngumu lakini nimeitengeneza timu yangu kuibuka na ushindi kesho (leo) nataka kujaribu kukwepa kufungwa mara mbili na Mtibwa,” alisema.
Kwa upande wa kocha wa Mtibwa, Mecky Maxime alisema timu yake iko vizuri na ana imani itaibuka na ushindi, ingawa alikiri kuwa katika wakati mgumu.
“Mechi itakuwa ngumu sana kwetu, kwa sababu tutataka kushinda ili tusitibue rekodi yetu na huku Simba nao wakitaka kushinda kulipa kisasi, lakini wachezaji wangu wanajua cha kufanya, nimeshawaelkeza,” alisema mchezaji huyo wa zamani wa Mtibwa.
Mtibwa ndio timu inayofanya vizuri kwenye msimamo wa Ligi Bara ambapo inaongoza ikiwa na pointi 16, katika mechi ya raundi ya raundi ya kwanza ya ligi timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1 kabla Mtibwa haijashinda mabao 3-0 katika mechi ya kirafiki mwishoni mwa mwaka jana.
Kwa mujibu wa kamati ya maandalizi ya michuano hiyo, bingwa atazawadiwa Sh milioni 10, medali za dhahabu na Kombe na mshindi wa pili atapata Sh milioni tano na medali za fedha.
Mbali na Mtibwa na Simba, timu nyingine zilizoshiriki michuano hiyo ni wenyeji Polisi, JKU, KMKM, Mtende Rangers, Mafunzo na Shaba za Zanzibar na kwa Tanzania Bara ni Yanga, Simba, Mtibwa na Azam na KCCA ya Uganda.
0 comments:
Post a Comment