KAMPUNI za simu za mikononi za Tigo na ZANTEL, zimeingia makubaliano ya kibiashara ambapo kwa sasa wateja wake wanaweza kutumiana pesa miongoni mwao kwa gharama za kama kawaida.
Katika makubaliano hayo, mteja wa TigoPesa ataweza kutuma fedha kwa mteja wa EzyPesa, ambapo makato yake yanakuwa ni kama anamtumia mteja mwenzake wa TigoPesa.
Akizungumza kutoka Zanzibar, Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Fedha wa Tigo, Andrew Hodgson alisema hatua hiyo ni muhimu kwa wakazi wa kisiwani humo, ambapo fursa ya kukua kwa huduma za fedha kwa mitandao ya simu bado ni kubwa.
Alisema kampuni hiyo imeona kuwa kuna umuhimu mkubwa wa kufanya kazi kwa kushirikiana badala ya kushindana, ambapo wamekuwa katika huduma hiyo ya kupokea fedha kwa kutumia mitandao Tanzania.
Alifafanua kufanya kazi na wadau wengine, kunawawezesha kupanua wigo wa wateja na hivyo kwa pamoja kutoa huduma ambazo ni bora zaidi, salama na za haraka kwa wateja wa pande zote.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Biashara wa Zantel, Mohamed Mussa, alisema kuwa Zantel inaendelea kutimiza ahadi ya kuwarahisishia huduma za fedha wateja wake kwa kufanya kazi pamoja na Tigopesa.
0 comments:
Post a Comment