
Mapacha hao, Abriana na Adriana, ambao walizaliwa wakiwa wameungana chini ya kifua na tumbo, walitenganishwa Novemba 17, mwaka huu.
Aidha, walikuwa wakitumia mvungu mmoja wa moyo na maini yaliyounganika.
Taarifa ya Hospitali ya Apollo ilisema jana kuwa mmoja wa wataalamu wa upasuaji, Dk. KS Sivakumar, alisema upasuaji huo ulikuwa wa mafanikio licha ya kuwapo kwa changamoto kubwa kwani moyo wa mmoja wa mapacha hao ulitakiwa kurudishiwa mahali pake.
Hii ni mara ya pili kufanyika kwa upasuaji wa aina hii kwa watoto toka hapa nchini katika hospitali hiyo.
Mara ya kwanza ilikuwa mwaka 2013 ambapo watoto Elikana na Eliudi walifanikiwa kutenganishwa.
Upasuaji huo ulifanywa na jopo la wataalam 50 waliobobea katika taaluma mbalimbali za tiba ya afya kabla na baada ya upasuaji ambao uliendeshwa kwa muda wa saa 11.
Wataalam walifanikiwa kutenganisha viungo vilivyokuwa vimeungana na mapacha hao walipona na kupata ahueni kwa haraka na wanatarajia kurejea nchini kesho kutwa wakiwa na wazazi wao, Jimmy na Caroln.
Wazazi wa watoto hao wanawashukuru madaktari wa hospitali hiyo pamoja na serikali kwa misaada mbalimbali waliyoipata katika kipindi chote cha matibabu ya watoto wao, Abriana na Adriana.
0 comments:
Post a Comment