Pluijm anayetarajiwa kuziba nafasi ya kocha Marcio Maximo aliyetimuliwa kazi baada ya kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa wapinzani wao, Simba, Jumamosi iliyopita, anatarajiwa kurudi katika nafasi hiyo akisaidiwa na Boniface Mkwasa.
Kabla ya Maximo, Pluijm na Mkwasa ndio walikuwa makocha wa Yanga lakini waliondoka baada ya kupata kazi katika klabu ya Al Shoula ya Saudi Arabia ambapo hawakukaa muda mrefu wakavunja mkataba na kocha huyo Mholanzi akarudi kwao na Mkwasa akarejea nchini ambapo alipata kazi ya Ofisa Elimu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Mkwasa hakuwa tayari kuweka wazi juu ya kuitosa TFF na kurejea Yanga, lakini habari za uhakika kutoka Yanga na kwa watu wa karibu na Mkwasa zinasema kocha huyo ambaye pia aliwahi kuichezea Yanga, atajiunga na swahiba wake Pluijm kuiongoza Yanga katika mechi zilizosalia za msimu.
Mkwasa aliliambia gazeti hili kwamba yeye bado kocha halali wa Yanga, kwa vile mkataba wake ulibaki mwaka mmoja na nusu na kwamba ataendelea iwapo tu ataitwa tena kuitumikia klabu hiyo kama kocha msaidizi.
“Nilienda likizo miezi mitano sasa nimerudi kama watanihitaji kuendelea kuifundisha timu hiyo, niko tayari,”alisema Mkwasa.
Kuhusu Pluijm habari za uhakika zinasema: “Amepewa mkataba wa mwaka mmoja lakini ndani ya kipindi hicho anatakiwa ahakikishe anavirudisha juu viwango vya wachezaji wa Yanga na timu ioneshe kandanda safi na kupigania ubingwa wa Tanzania bara msimu huu,” alisema mtoa habari huyo.
Mtoa habari huyo alisema Mholanzi huyo pia ametakiwa ahakikishe Yanga inapambana na kushinda pindi inapokutana na timu kubwa kama za Simba, Mtibwa Sugar na Azam FC, ili kuwepo na uhakika wa kunyakua ubingwa msimu huu tofauti na wakati timu hiyo ilipokuwa kwenye mikono ya Maximo.
“Unajua ilikuwa wakati Maximo anafundisha timu idadi kubwa ya mashabiki walikuwa wanakwenda uwanjani bila ya kuwa na matumaini ya ushindi, hasa katika mechi kubwa kama za Simba na Azam ndiyo sababu Pluijm ametakiwa aibadilishe timu ili iweze kuwa na uhakika wa ushindi japo chochote kinaweza kutokea,” kilisema chanzo hicho.
Mtoa habari huyo alisema Pluijm amekubali kutimiza mashrti hayo kwa madai kuwa ana uhakika kazi yake haitakuwa ngumu kutokana ubora wa kikosi cha Yanga na mbinu alizokuwa nazo ambazo anaamini atatumia muda mfupi ili kuibadili timu hiyo icheze soka la kuvutia kama ilivyokuwa nyuma.
“Kwa sasa siwezi kuzungumza chochote kuhusu mambo ya timu kwa sababu sijasaini na jioni hii (jana) natarajia kukutana na viongozi wa Yanga kwa ajili ya kumalizana nao, lakini nitazungumza na nyie kesho (leo) baada ya kusaini mkataba.
Hadi gazeti hili linakwenda mtamboni, Maximo alikuwa hajamalizana na uongozi wa Yanga kuhusu kulipwa stahiki zake ili arudi kwao Brazil na kumuachia kazi Pluijm.
0 comments:
Post a Comment