NYARI ANGOMEA MATOKEO

Author
MCHUANO wa makada 12 wa CCM katika kuwania Ubunge wa Jimbo la Arusha Mjini, umemalizika kwa kura za maoni kuamua kuwa, mfanyabiashara maarufu wa bidhaa za chakula, Philemon Mollel `Monaban’ ndiye mshindi. Hayo yamethibitishwa na Katibu wa CCM wilaya ya Arusha, Ferouz Banno aliyetangaza matokeo hayo jana.
Alisema Mollel amepata kura 5,320 akifuatiwa na mfanyabiashara mwingine, Justin Nyari (1,894) ambaye hata hivyo amepinga matokeo hayo na kudai amemwandikia barua Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana kuelezea kutoridhishwa na matokeo hayo.
Wengine na kura zao kwenye mabano kwa mujibu wa Banno ni Moses Mwizarubi (1,105), Thomas Munisi (832), Victor Njau (772), Swalehe Kiluvia (446), Mustapher Panju (368), Hamisi Migire (305), Edmund Ngemera (198), Reuben Mwateni (171), Emmanuel Ole Njoro na Mahmoudu Omari, wote kura 90.
Akizungumza jana mara baada ya Katibu wa CCM wilaya ya Arusha, Ferouz Banno kutangaza matokeo hayo nje ya ofisi hiyo, Nyari alisema anapinga matokeo hayo na kudai ni batili.
‘’Nimemwandikia nakala ya barua Katibu Mkuu wa CCM Taifa Abdulrahman Kinana na kumweleza kila kitu kilichokuwa kikiendelea kabla ya kampeni na ndani ya kampeni nasubiri majibu na nina imani na chama kuwa watayafanyia kazi malalamiko hayo,’’ alisema Nyari aliyedokeza kuwa, malalamiko yake yanahusu tuhuma za rushwa, ukabila na pia kuanza mapema kampeni kwa washindani wake.
Kwa upande wake, Mollel aliwashukuru wanaCCM waliompa ushindi na kuahidi kuwatumikia kwa dhati, ambapo pia aliahidi atashirikiana na wagombea wenzake ili kuhakikisha ushindi wa CCM unapatikana na kuijenga Arusha mpya.
Pia, alisema hana wasiwasi na vikao vya juu vya chama kwa kuwa anaamini vitatenda haki na kurejesha jina lake kwa kuwa yeye pia alitenda haki katika kinyang’anyiro chote. Mustafa Panju alisifu mchakato mzima tangu mikutano ya kura za maoni na kwamba bado anaahidi kushirikiana vyema na wagombea wote na yule atakayepitishwa na vikao vya juu.
Monduli Katika Jimbo la Monduli lililoachwa na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, Katibu wa CCM wilaya hiyo, Elisante Kimaro alimtangaza Namelok Sokoine kuwa mshindi kwa kupata kura 29,582, Loota Sanare akipata kura 8860, Lorinyu Nkosi akipata kura 235, Mbayani Tayani akipata kura 226, Amani Torongei akipata kura 107 na Sakaya Kabuti akipata kura 159.
Namelok aliyekuwa mbunge wa Viti Maalumu katika Bunge linalomaliza uhai wake Agosti 20 mwaka huu, ni binti wa Waziri Mkuu wa zamani, hayati Edward Moringe Sokoine. Arumeru Mashariki Katika jimbo la Arumeru Mashariki Katibu wa CCM wilaya Langaeli Akyoo alimtangaza Mjumbe wa Kamati ya Siasa mkoa na Kamanda wa Vijana wilaya hiyo, Danielson Pallangyo, almaarufu Jdee akipata kura 11,342, akifuatiwa na Sioi Sumari (3,491), William Sarakikya (3,159).
Wengine ni Dk Daniel Pallangyo aliyepata kura 1,646 na Elirehema Kaaya aliyepata kura 818.

0 comments:

Post a Comment