Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema utitiri wa viongozi wa serikali kujitokeza kuchukua fomu ya kuomba kugombea urais ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu ni sawa na kuidhalilisha taasisi ya urais.
Aidha, kimesema idadi kubwa ya mawaziri kukimbilia kuwania urais
kinaonesha kuwa huenda hawaridhishwi na utendaji kazi wa serikali ya
chama chao, inayoongozwa na Rais Jakaya Kikwete.
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Taifa kutoka Zanzibar, Salum
Mwalimu, alisema hayo juzi wakati akihutubia mamia ya wakazi wa
Manispaa ya Musoma katika mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya
Shule ya Sekondari Mara.
Alisema hatua ya wagombea wa CCM kila mmoja kuonyeshwa kuchukizwa
na vitendo vya rushwa, umasikini unaosababishwa na Serikali iliyopo
madarakani ni sawa na dharau kwa serikali yao.
Mwalimu alisema Watanzania hivi sasa wamechoka na umasikini,
dhuruma na rushwa unaosababishwa na uongozi mbovu wa Serikali ya CCM.
“Kila mmoja anasema atakomesha rushwa, ufisadi na kukuza uchumi,
maana yake ni nini kama siyo kejeli na dharau kwa Serikali yao ya
CCM…sisi tukishinda tutamsaidia Rais Kikwete kupata mapumziko mema kwani
wenzake hasa mawaziri wamemchoka,” alisema.
Kuhusu mgombea urais wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa),
alisema timu ya viongozi wa umoja huo itakayoongoza Serikali ya awamu ya
tano itakuwa kama timu ya soka ya Barcelona na mgombea wake wa urais ni
kama Lionel Messi.
Mwalimu alisema Ukawa wamejipanga vizuri kuhakikisha watakapoingia
madarakani Oktoba mwaka huu wanashughulikia matatizo yanayowakabili
wananchi, ikiwamo kukomesha rushwa, dhuluma, ufisadi, umasikini na
kuboresha huduma zote za jamii.
“Serikali ya Ukawa itaendesha nchi kwa mfumo wa 4, 4, 2 yaani
Morinho staili. Tutakomesha ufisadi, rushwa na kuwapeleka mchakamchaka
Watanzania katika kumiliki uchumi unaostahili kimataifa,” alisema.
Alisema wananchi wamechoka na uongozi mbovu wa Serikali ya CCM na
kwamba serikali itakayoundwa na Ukawa itajenga na kuimarisha viwanda,
reli, kukuza uchumi na ajira, kuboresha huduma za afya, maji, elimu na
kudhibiti rushwa mahakamani, polisi na taasisi zote za umma.
Mwalimu aliwasihi wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha
kwenye daftari la wapiga kura, ili wapate fursa ya kuiangusha CCM na
kuiweka madarakani Serikali ya Ukawa.
0 comments:
Post a Comment