Wewe ni mtu wa kulala sana? Saa moja usiku upo kitandani,
unaamka saa nne asubuhi. Inawezekana ukaendelea kulalamika na
kuwanyooshea wengine kidole kwamba ni ‘wachawi’ wanaozuia mafanikio
yako, huku wao wakivuna mafanikio.
Hiyo ni moja ya dhana zinazoaminika kukosesha
wengi mafanikio. Ingawa siyo watu wote wanaolala sana hawafanikiwi,
lakini ukweli unabaki kuwa asilimia kubwa ya watu hao hawafanikiwi, huku
wale wanaotumia muda mfupi kulala na kutumia muda mwingi kufanya kazi
wakivuna kipato kikubwa na mafanikio maishani. Hufanikiwa kwa sababu tu
hutumia muda mwingi kufanya kazi, kuliko kulala. Muda huo hujumuisha
muda wao wa ziada kufanya kazi ili kuongeza kipato.
Tafiti za hivi karibuni zinathibitisha kwamba watu masikini wanaendekeza ‘kuvuta shuka’ zaidi ya matajiri.
Baadhi ya matajiri wapo radhi walale hata kwa saa
nne ili saa zilizobaki wafanye shughuli za maendeleo kwa sababu wanaona
muda walionao hautoshi kufanya shughuli zao za kuwaongezea kipato.
Maisha mazuri na kila kitu kizuri kinakuwa chako
ikiwa utajituma kwa juhudi na maarifa. Watu ambao hata kwenye maeneo yao
ya kazi huwavutia mabosi wao kutokana na uchapa kazi wao, hao pia wamo
katika njia ya mafanikio.
Profesa wa Uchumi wa Chuo cha Texas, Marekani
Daniel Hamermesh anasema kuwa tafiti mbalimbali za hivi karibuni
zinaonyesha kwamba watu wenye kipato kikubwa hulala saa chache kuliko wa
kipato kidogo.
“Dhana hiyo hutokana kujituma na kufanya kwao kazi
kwa bidii kwa hiyo mtu anaona bora ajitolee kufanya kazi saa nyingi
kuliko kulala, ili awaze kupata mshahara mkubwa kutokana na saa ya ziada
anayofanya kazi.”
Hamermesh anasema kuwa kujituma huko pia
kunaambatana na marupurupu ambayo kampuni hutoa kwa wafanyakazi
wanaojituma kwa manufaa ya kampuni husika.
“Mbali na kampuni kuwalipa vizuri wafanyakazi kama
hao kutokana na muda mwingi wanaotumia kuzalisha kwa ajili ya kampuni.
Mabadiliko ya mfumo wa utendaji katika kampuni huwasukuma wafanyakazi
kufanya kazi zaidi,”anasema na kuongeza:
“Tofauti na ilivyokuwa kwa siku za nyuma ambapo
baadhi ya kazi zilikuwa zikifanywa na mtu zaidi ya mmoja, sasa mambo
yamebadilika. Karne hii mtu analazimika kufanya kazi zilizokuwa
zinafanywa na zaidi ya mtu mmoja.”
Hamermesh ambaye pia ni Profesa wa Chuo Kikuu cha
Royal Holloway huko London Uingereza, anasema kutokana na mabadiliko
hayo, mtu hulazimika kutumia muda mwingi kuhakikisha anatimizia wajibu
wake kwa wakati.
Mtaalamu wa uwekezaji katika benki nchini
Marekani, David Solomon anasema: “Hayo yote ni matokeo ya mabadiliko ya
teknolojia, ambayo inatambua kwamba mfanyakazi anatakiwa kuwepo au
kupatikana wakati wowote (saa 24), kwa ajili ya shughuli za kikazi.
Hakuna mipaka wala kupumzika. Ni kukimbizana na matukio, ili kuhakikisha
hatuachwi nyuma katika kila jambo linatokea duniani.” Anatolea mfano wa
miaka 30 iliyopita akisema kuwa, kipindi hicho wajiriwa waliokuwa
wakifanya kazi saa chache ndiyo walikuwa wakilipwa mshahara mnono.
“Lakini sasa wanaofanya kazi saa chache ndiyo wanalipwa kidogo
na wanaofanya kazi saa nyingi wanalipwa mara mbili au zaidi ya wale
wanaofanya kazi saa chache. Kufanya kazi kwako kwa bidii ndiyo kufikia
malengo ya kampuni na ya kwao ambayo ni chachu ya kupata kipato
kizuri,”anasema Solomon.
Kwa nini mishahara mikubwa?
Solomon anabainisha kuwa kampuni zinalazimika kulipa wafanyakazi mishahara mikubwa kwa sababu mfumo wa kufanya kazi umebadilika.
Anasema kuwa wafanyakazi wanafanya kazi kwa saa
nyingi, tofauti na ilivyokuwa siku za nyuma, hivyo ndivyo mfumo huo
unavyondelea kuwa.
Wataalumu hao wanasema, mshahara mkubwa ni hongo
ambayo kampuni hutumia kwa ajili ya kuwashawishi wafanyakazi wajitume na
kuendelea kutumikia kampuni yao.
Mtaalamu wa Utafiti na Uchumi wa Chuo Kikuu cha
Ohio Marekani, Jay Zagorsky anabainisha kwamba, ikiwa kampuni imeingia
gharama nyingi ya kutoa mafunzo wa wajiriwa wake, itajitahidi kwa namna
yoyote kuhakikisha watu hao wanaitumikia kampuni ipasavyo.
“Kampuni haitataka kuwapoteza wafanyakazi wao
wenye kujituma, wanakwenda kufanya kazi sehemu nyingine kwa sababu
wanaamini mafunzo waliyotoa kwao yalilenga kuongeza ufanisi na weledi
katika utendaji kazi,”anasema.
Mtaalamu huyo, anasema kuwa mara nyingi mtu yeyote
anapohitimua cheti, stashahada au shahada na kupata ajira, inakuwa
vigumu kujiendeleza kimasomo.
“Mtu akiwa kazini jukumu hilo linamwangukia
mwajiri tena kama akiona mwajiriwa ana uwezo, anajituma na kuchapakazi,
hapo mwajiri atalazimika kugharamia mafunzo yake kwa sababu anafahamu
akiongeza ujuzi, kampuni pia itanufaika,”anasema Zagorsky na kuongeza:
“Lakini pia waajiri huangalia jinsi ambayo
washindani wao wanawalipa mishahara wafanyakazi wao. Kama wanalipa
mshahara mdogo watahakikisha wanalipa wafanyakazi wao mshahara mkubwa
ili wasishawishike kuhama kampuni.”
Anabainisha kuwa kwa jinsi mambo yalivyo, hasa
kutokana na kukua kwa sayansi na teknolojia, kuna hatihati kwamba
waajiriwa wengi watalazimika kufanya kazi saa nyingi tofauti na ilivyo
sasa.
“Mabadiliko hayo yatakwenda sambamba na ongezeko
la kazi kwa waajiriwa kwani teknolojia imebadili mambo mengi, mfano sasa
kazi,”anasema.
Madhara ya kulala saa chache
Hata hivyo, wataalamu wa masuala ya afya wanabainisha kwamba
kulala saa chache kunaweza kumsababishia mtu madhara ya kiafya .
Dk. Syriacus Buguzi kutoka Hospitali ya
Mwananyamala, wilayani Kinondoni, Mkoa wa Dar es Salaam anasema kuwa
kutolala kwa muda wa kutosha kama inavyopendekezwa kitaalamu kuna
madhara mengi kwa afya ya binadamu.
Anasema kuwa matatizo hayo yanaweza kuwa ya muda
mrefu au mfupi na kushauri kwamba watu, hasa wafanyakazi kuwa makini na
ratiba zao za kila siku, ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza na
kuathiri mipango au shughuli za mhusika.
“Zipo dalili nyingi za mtu ambaye hakupata
usingizi wa kutosha. Kukosa umakini kwa anachokifanya, kutomaliza kazi
aliyonayo na kutokuwa na ufanisi. Hii hutokea kwa watu ambao hawakulala
vya kutosha kwa muda mrefu,” anasema Dk Buguzi na kuongeza: “Kwa watu
wanaokosa usingizi kwa muda mrefu kama mwaka au miaka kadhaa, wapo
katika hatari ya kupata athari kubwa zaidi. Hali hiyo huchangia msongo
wa mawazo, ambao huathiri kinga za mwili.”
“Baada ya muda mtu huyo huugua hovyo. Kinga zake
zinakuwa dhaifu zisizoweza kushambulia vijidudu vyovyote vya magonjwa,”
anaeleza na kufafanua kuwa suala la msingi ni kuchunga majukumu
yasiingilie ratiba nyingine hasa ya kulala.
Profesa Hamermesh anasema tafiti mbalimbali za
hivi karibuni zinaonyesha kwamba mbali na madhara ya kiafya, kutumia
muda mwingi kazini husababisha uhusiano mbaya kwa ndugu, jamaa na
familia kwa jumla.
“Licha ya wajiriwa kama hao kulipwa fedha nyingi
na kuwafanya waingize kipato kikubwa, lakini kutopata muda wa kutosha
kwa ajili ya familia zao ni tatizo pia…fedha hizo zitagharamia mahitaji
yote, lakini haziwezi kukunua upendo kutoka kwa ndugu, jamaa na familia
yake aliyopoteza kwa sababu ya kutumia muda mwingi kazini kuliko
nyumbani,”anasema.
0 comments:
Post a Comment