EPUKA HAYA KUONGEZA KIPATO KWENYE BIASHARA

Author
Ni siku nyingine mpenzi msomaji wa safu hii ya kona ya wajasiriamali tunapokutana tena. Karibu katika kona ya wajasiriamali yenye maudhui ya kuona namna bora ambazo wajasiriamali wanaweza kuzitumia ili kuendeleza biashara zao na kupata mafanikio. 
 
Sina budi kuwashukuru wasomaji wa kona hii ambao wamekuwa wakiwasiliana nami juu ya kutafuta namna bora ya kuweza  kujenga ustawi katika shughuli zao. Nawashukuru sana kwa kunitia moyo kuwa tuko pamoja na mnafurahi kile mnachokipata.
 
Siku zinayoyoma na sasa ni mwezi wa sita, ambao unatuweka katika nusu ya kwanza ya mwaka huu wa 2015. Leo katika kona hii ya ujasiriamali tutakumbushana juu ya baadhi ya makosa ya kuyaepuka ili biashara yako iweze kupiga hatua. 
 
Mwenye kujua kama unataka mafanikio katika biashara ama la, ni wewe mwenyewe, kaa chini na utafakari baadhi ya mambo ambayo yanaweza kuwa kikwazo cha wewe kupiga hatua. Kumbuka unapaswa kudhibiti mambo yote ambayo yako ndani ya uwezo wako. 
 
Kumbuka ndugu mjasiriamali tunaishi katika ulimwengu wenye mambo yanayobadilika kila siku. Bila kujituma na kufanya kazi kwa bidii na kukabiliana vema na changamoto mbalimbali, huwezi kufikia ndoto zako unazotamani kuzifikia vema, huwezi kupiga hatua.
 
Mjasiriamali ukiwa na kiu ya mafanikio unahitaji kuamka tena bila kukata tamaa kwani bado una nafasi.  Ili kuepuka matatizo ya kushindwa katika biashara, hakikisha baadhi ya makosa kama uliwahi kuyafanya katika kipindi cha mwaka jana huyafanyi tena.
 
Amini unaweza
Kosa la kwanza, epuka kutojiamini. Vipi tangu mwaka huu wa 2015 umeanza mpaka sasa je, umeweza kujiamini wewe mwenyewe ? Kama hukuweza kujiamini unafikiri nani atakuamini ? Hakikisha ndugu mjasiriamali unakuwa mtu wa kujiamini siku zote.
 
Kumbuka ndugu mjasiriamali kwamba kujiamini kwako kutakupa nguvu ya kufikia yale unayotamani, kujiamini kwako kutakuwezesha wewe kuwa na mtazamo chanya (positive attitude) kwa yote unayofanya na kukupeleka kwenye njia ya mafanikio unayotamani.
 
Amini kwamba unaweza kufanya vizuri hicho ambacho umeamua kukifanya na kitakukomboa. Kama mjasiriamali mwenye kiu ya mafanikio, unahitaji kusema unaweza kwa kila unachofanya, kwani kama wengine waliweza kwanini wewe useme huwezi?
 
Jitoe kwa moyo wote
Kosa la pili, kutoweza kujitoa (lack of commitment). Ili kuweza kufikia mafanikio ya kweli huna budi kujitoa kwa moyo wote pamoja na kukaa chini  na kujiwekea mipango yako mbalimbali. Huna budi kujitoa, kama huwezi ni vigumu kufanikiwa. 
 
Mafanikio katika ujasiriamali si suala la kulala na kuamka, unahitaji kujitoa kwa moyo wako wote na akili yako ili mambo yaende. Usione wajasiriamali wakubwa unaowafahamu wamefanikiwa ukafikiri kuna njia ya mkato, unahitaji kubadilika.
 
Kuwa mtu wa vitendo
Kosa la tatu, kutokuwa mtu wa vitendo. Hili ni moja kati ya makosa makubwa yanayofanywa na wajasiriamali wengi. Inawezekana tangu mwaka huu wa 2015 umeanza ulikuwa na mipango mingi lakini mpaka sasa ni michache uliyoweza kuifanya. 
 
Jiulize katika mipango uliyokuwa nayo ni ipi uliitekeleza na ipi uliiacha, ni wakati wa kujiuliza kwanini hukufanya kile ulichopanga? Wapo wajasiriamali ambao wamekuwa wazuri zaidi katika kuongea kuliko kutenda, je, wewe unajiweka katika upande gani?
 
Ni wakati wa kuamka na kubadilisha mwenendo huo, kuwa mtu wa vitendo acha porojo. Kuna wajasiriamali ambao wakikuambia mipango yao unaweza kusema jamaa sasa hivi anakuwa milionea, lakini kuleta mipango katika uhalisia huwa jambo gumu kwao. 
 
Usifuate mkumbo
Kosa la nne, kufuata mkumbo. Watu wengi wameingia kwenye ujasiriamali kwa kufuata mkumbo hasa kwa kuiga kutoka kwa wenzao yale wanayofanya. Wapo ambao kwa mfano wameingia kwenye biashara ya nguo kwa kuona tu wenzao wanafanya hivyo.
 
Unapoamua kuingia kwenye ujasiriamali lazima upate msukumo wa ndani wa wewe kufanya hivyo, hata kama unaiga basi usiige kila kitu kwani kila mjasiriamali anahitaji kutafuta fursa za yeye kuweza kujenga msingi wa mafanikio kwa kusimama mwenyewe.
 
Hivyo yafaa kujiuliza, kwanini umeamua kufanya hicho unachofanya? Unaweza ukawa kila wakati unalia kwamba hupati mafanikio katika hicho unachofanya kumbe sababu kubwa ya wewe kutopata mafanikio ni kuingia kwenye uwanja ambao si wako.
 
Una mipango gani?
Kosa la tano, kutokuwa na mipango (no planning). Kuna msemo unaosema "kushindwa kupanga ni kupanga kushindwa". Kama huwezi kujua unaelekea wapi huwezi kufika huko, ni muhimu kuwa na mipango ili kuwa na mwelekeo wenye kueleweka na kufaa. 
 
Tunapozungumzia kuwa na mipango yafaa kukumbuka wakati wote sifa za mipango wajasiriamali wanayopaswa kuwa nayo. Yafaa kuwa na mipango maalum, inayotekelezeka, inayopimika na kufikika katika muda utakaojiwekea.
 
Wajasiriamali wengi huja na mipango ambayo iko juu ya uwezo wao na hata utekelezaji wake huwa mgumu. Yafaa mipango ya wajasiriamali iendane na uhalisia na uwezo walio nao katika kuendesha shughuli zao, vinginevyo watakuwa na mambo yasiyotekelezeka.
 
Nenda na wakati.
Kosa la sita, kutokwenda na wakati. Tunapozungumzia kwenda na wakati maana yake mjasiriamali huna budi kubadilika kutokana na mazingira uliyo nayo. Dunia ya leo si dunia ya jana, dunia imekuwa kijiji mambo yamebadilika huna budi nawe kubadilika.
 
Mjasiriamali lazima ujifunze kubadilika kutokana na mabadiliko mbalimbali katika ulimwengu wa biashara. Ni hatari kufanya mambo kimazoea kwa kuwa tu yale uliyokuwa unayafanya na kufanikiwa yataendelea hivyo hivyo, kila siku sio Ijumaa.
 
Kama unavyoelewa kuna mabadiliko mengi katika dunia ya ujasiriamali kama vile ya ushindani wa kibiashara, teknolojia na mengine mengi. Epuka kufanya mambo kimazoea kwa kuhakikisha unajichanganya na kwenda na wakati. Usijifungie vioo.
 
Jikune mkono unapofika
Kosa la saba, mpangilio usiofaa wa mitaji ( insufficient funding). Kuna msemo wa kiswahili usemao, mgongo hujikuna pale mkono unapofika. Na ndivyo wajasiriamali hufanya kosa hili la kupenda kufanya mambo makubwa bila kuwa na uwezo wa kutosha.
 
Wajasiriamali wengi hulia juu ya ukosefu wa mitaji katika kuendeleza au kukuza biashara zao, lakini pia wapo ambao hupenda kufanya mambo ambayo hayaendani na hali halisi ya mitaji waliyonayo, hupenda kufanya mambo kwa kutafuta mafanikio ya haraka.
 
Inashauriwa ndugu mjasiriamali kujipanga kutokana na uwezo ulio nao na si kuota ndoto za mchana. Wapo ambao wangeweza kufanya vizuri kwenye mambo madogo lakini kwa kutaka mafanikio ya haraka wamejiingiza kwenye biashara zenye mahitaji makubwa.
 
Kubali hali halisi ya uwezo ulionao na amini kuwa unaweza kufanya mambo madogo kulingana na mtaji na kidogo kidogo utasonga mbele na kukua. Kuna baadhi ya biashara unaweza kufanyia nyumbani kwanza bila kuwa na 'fremu', tafakari hilo na chukua hatua sasa.
 
Pokea changamoto
Kosa la nane, kutokuwa tayari kupokea changamoto. Wakati mwingine wajasiriamali wengi hushindwa kudumu katika biashara zao kutokana na kutokuwa tayari kukubali changamoto mbalimbali wanazokutana nazo katika shughuli zao za kila siku.
 
Ikiwa mmoja wa marafiki au ndugu anakwambia juu ya jambo ambalo si zuri katika biashara yako yafaa kutopuuza. Kaa chini na ufanye tathmini ya kile unachoambiwa kwani huenda kikasaidia kuokoa biashara yako juu ya jambo fulani.
 
Kuambiwa jambo fulani juu ya biashara yako hasa usilopenda si kwamba ukae katika nafasi ya kufanya kila wasemalo, bali jambo kubwa la kufanya ni kusikiliza. Huwezi kujua kuna siku watakupa ushauri mzuri zaidi wa kuboresha biashara yako.
 
Kosa kurudia kosa
Kosa la tisa, kosa juu ya makosa yote ni kurudia makosa yale yale kila wakati. Makosa hayakwepeki na ni sehemu ya shughuli za wajasiriamali kila siku. Tatizo linakuja kama utakuwa mtu wa kurudia makosa yale yale kila wakati, utarudi nyuma tu.
 
Wajasiriamali wanapaswa wawe watu wa kujifunza kutokana na makosa si tu wanayoyafanya bali hata yale wanayoyaona kutoka kwa wengine. Kama utakuwa unajifunza kutokana na makosa, basi utakuwa na uhakika wa kuokoa pia fedha zako. 

0 comments:

Post a Comment