Yanga, mabingwa mara 24 wa Tanzania Bara na wawakilishi pekee wa
nchi waliosalia katika michuano ya kimataifa ya klabu mwaka huu, walitoa
kipigo kikubwa cha mabao 8-0 dhidi ya Coastal katika mechi ya Ligi Kuu
ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es
Salaam, ikiwa ni siku ya Jumatano Aprili 8.
Kikosi cha Mdachi Hans van der Pluijm, kitashuka Uwanja wa Taifa
Jumapili Aprili 12, kuikabili timu iliyopunguza makali yake ya msimu
uliopita, Mbeya City katika mwendelezo wa ligi hiyo huku uongozi
ukitamba kuwa City itafuata nyayo za 'Wagosi wa Kaya' kwa kubamizwa
mabao mengi.
Pluijm aliliambia NIPASHE mara tu baada ya mechi ya juzi kuwa mechi
za VPL dhidi ya Coastal na City ni sehemu ya maandalizi yao kabla ya
kuikabili Etoile Sportive du Sahel (ESS) katika michuano ya kimataifa.
Kutokana na kipigo cha mabao 8-0 kuangukia Aprili 8 (juzi), Mkuu wa
Idara ya Habari na Mawasiliano ya Yanga, Jerry Muro, alisema jijini
jana kuwa City inapaswa kuangalia tarehe ya mechi yao inayofuata kisha
ijiandae kupokea idadi ya mabao ambayo alitamba itakuwa sawa na tarehe
husika.
"Coastal tumewafunga mabao 8-0 tarehe nane, Mbeya City kabla ya
kututangazia vita sisi (Yanga), wanapaswa kuangalia tarehe ya mechi yetu
dhidi yao. Tutawapiga mabao 12 Jumapili maana tuna wachezaji wenye
uwezo huo. Yanga hii ni ya kimataifa.
Wazitangazie vita timu za mchangani," alisema Muro.
Baada ya kuishika Azam FC kwa sare ya 1-1 kwenye Uwanja wa Azam
jijini juzi na kuwagombanisha Meneja wa Azam FC, Jemedari Said na Ofisa
Mtendaji Mkuu (CEO), Saad Kawemba, kocha mkuu wa City, Juma Mwambusi,
aliwataka wachezaji wake wajiandae kwa vita dhidi ya Yanga Jumapili.
Mwambusi, kocha bora wa VPL msimu uliopita, alisema: "Nashukuru
wachezaji wangu wamepambana, tumepata pointi moja ni jambo zuri kwetu
kwa sababu tutakuwa tumesogea katika nafasi nyingine, tuna mchezo
Jumapili, hivyo tujiandae na tujue kuwa tunatakiwa kuipigania timu yetu
mpaka dakika ya mwisho."
Yanga iko kileleni mwa msimamo wa VPL ikiwa na pointi 43 baada ya
mechi 20 wakati City iko nafasi ya saba ikiwa na pointi 25 baada nayo
kushuka dimbani mara 21.
City imefungwa mara mbili dhidi ya Yanga katika mechi tatu
walizokutana, na timu hiyo ya Jiji la Mbeya haijawahi kupata ushindi
dhidi ya Wanajangwani hao tangu ipande Ligi Kuu msimu uliopita.






0 comments:
Post a Comment