CHRISTOPHER ALEX MASAWE AFARIKI DUNIA ·

Author
Aliyekuwa kiungo wa timu ya Simba SC Christopher Alex Masawe amefariki dunia leo saa 3 Asubuhi katika hospitali ya Milembe mkoani Dodoma baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Akizungumza na East Africa Radio, Dada wa Marehemu, Wakuru Ndayenda amesema, Christopher alianza kusumbuliwa na TB miezi mitatu iliyopita na kuamua kuanza matibabu ya ugonjwa huo lakini baadaye alipatwa na ugonjwa wa kuchanganyikiwa na alipopimwa tena aligundulika na fangasi ya koo ambayo ilisambaa mpaka kichwani.
Ndayenda amesema, Christopher alizidiwa na magonjwa hayo Februari 11 ambapo alipelekwa hospitali ya Mirembe Februari 12 na ndipo alipokutwa na mauti leo asubuhi.
Christopher Alex Massawe ameacha watoto wawili ambapo anatarajiwa kuzikwa siku ya Jumanne makaburi ya Chinangali West mjini Dodoma.
Christopher Alex atakumbukwa kwa kufunga penati ya mwisho katika mchezo wa Simba dhidi ya Zamalek na kuifanya Simba ifuzu hatua ya Robo Fainali ya michuano ya Klabu Bingwa barani Afrika mwaka 2003 mchezo uliopigwa nchini Misri.
Baadhi ya wachezaji waliounda kikosi hicho kilichoitoa Zamalek ni pamoja na Boniface Pawasa, Juma Kaseja na Suleiman Matola.
Rais wa Simba Evans Aveva ambaye yuko mjini Shinyanga katika pambano la ligi kuu dhidi ya Stand United ametuma salam za rambirambi kwa familia ya marehemu na kumuelezea marehemu kuwa aliitumikia Simba kwa juhudi, mapenzi na uaminifu mkubwa na kusema kwamba Simba itaungana na familia yake katika msiba huo.
Like ·
· ·

0 comments:

Post a Comment