
Okwi amefunga bao hilo kwa kupiga banana chop akiwa mita 27 baada ya kugundua kipa wa Yanga Ali Mustaph, ametoka langoni mwake na hiyo ilitokana na mpira wa kona iliyokuwa kwenye lango la Simba na kuokolewa na kiungo Abdi Banda aliyempasia Ibrahim Ajibu ambaye naye alipiga mpira mrefu kwa Okwi.
Hilo ni bao la tano kwa Okwi tangu arejee Simba akitokea Yanga mwanzoni mwa msimu huu na kuingarisha timu hiyo aliyoanza kuichezea tangu akiwa na miaka 18 akisajiliwa kutoka klabu ya Soport Club Villa ya Uganda.
Ushindi huo unakuwa wapili mfululizo kwa Simba ambayo wiki iliyopita iliweza kuifunga Tanzania Prisons mabao 5-0 na sasa imefufua matumaini ya kuwania ubingwa baada ya kufikisha pointi 26 katika nafasi ya tatu huku Yanga wakiendelea kubaki kileleni na pointi zao 31.
Katika mchezo huo Simba ilionyesha daliliza ushindi tangu mwanzoni baada ya kutawala mchezo huo hasa eneo la kiungo kwa dakika 20 huku Yanga wakionekana kucheza kwa kujihami na kutumia mashambulizi ya kustukiza ambayo hata hivyo hayakuwa na madhara kwa wapinzani wao.
Mshambuliaji anayechipukia kwa kasi wa Simba alikuwa wa kwanza kulifikia lango la Yanga katika dakika ya pili na kuachia shuti kali ambalo halikuweza kulenga lango na kutoka nje.
Simon Msuva angeweza kuifungia timu yake ya Yanga bao la kuongoza dakika ya saba baada ya kupata nafasi nzuri akiwa ndani ya 18 lakini chakushangazabaada ya kumtengenezea Amissi Tambwe afunge alipiga shuti dhaifu lililodakwa na kipa wa Simba Ivo Mapunda.
Kadri muda ulivyokuwa ikienda Yanga ilionekana kuimarika na kurudi mchezoni na kuanza kuutawala mchezo na kutengeneza nafasi nyingi ikiwemo ile ya dakika 25 aliyoipata Danny Mrwanda lakini alipatwa na kigugumizi cha muguu na kushindwa kufunga.
Dakika tano baadaye kocha wa Yanga Hans van der Pluijm aliamua kumtoa nje Mrwanda na nafasi yake kuchukuliwa na Hussein Javu , hiyo ilitokana na mchezaji huyo kuonyeshwa kadi ya njano baada ya kumuonyesha ubabe beki wa Simba Kessy Ramadhani ambaye awali alimchezea rafu.
Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika timu hizo zilikuwa bado hazija fungana na Yanga ndiyo waliopata nafasi tano za kufunga mabao kupitia kwa washambuliaji wake Mrisho Ngassa, Simon Msuva, Tambwe na Mrwanda.
Kipindi cha pili kilianza kwa Simba kuanza kuliandama lango la Yanga ambapo Ibrahim Ajibu, alipata nafasi nzuri dakika ya 47 akiwa nje ya eneo la hatari na kupiga shuti kali lilitoka nje na kuwa goli kiki.
Yanga ilijibu shambulizi hilo katika dakika ya 49 Javu aliyewapangua mabeki wa Simba na kupiga shuti kali lililopanguliwa na kipa Mapunda na kuwa kona ambayo iliokolewa vyema na mabeki wa Simba .
Baada ya kuingia kwa bao hilo Yanga walionekana kubadilika na kucheza kwa kasi wakitafuta bao la kusawazisha lakini katika dakika ya 74 walijikuta wakicheza pungufu baada ya kiungo Mnyarwanda Haruna Niyonzima kuonyeshwa kadi nyekundu na mwamuzi Martin Saanya kwa kosa la kupiga mpira wakati filimbi imeshapigwa.
Hiyo ilikuwa ni kadi ya pili ya njano awali Niyonzima alionyeshwa kadi ya njano dakika ya 42 kipindi cha kwanza kwa kumchezea rafu Ramadhani Singano .
Simba nayo baada ya kupata bao hilo ilionekana kucheza kwa kupoteza muda huku ikifanya mashambulizi ya kustukiza na dakika ya 80 Okwi tena alipiga shuti kali lilitoka pembeni kidogo ya lango la Yanga.
Kutokana na presha ya mchezo huo kwa nyakati tofauti wachezaji wa timu zote mbili walionekana kuchezeana kibabe ambapo dakika ya 78 beki wa Simba Juuko Murshid na Amissi Tambwe walionyeshwa kadi za njano kwa kuonyeshana undava.
Baada ya kuona mambo magumu kocha wa Yanga aliamua kumtoa Ngassa na kumuingiza Kpah Sherman hwakati kwa uande wa Simba kocha Goran Kopunovic aliwatoa Ibrahim Ajibu ambaye nafasi yake ilichukuliwa na Elias Maguli na dakika ya 87 ilimtua Abdi Banda ambaye nafasi yake ilichukuliwa na Simon Sserunkuma.
0 comments:
Post a Comment