
Ilikuwa kama sinema wakati wafuasi 30 wa Chama cha Wananchi (CUF) wanaokabiliwa na kesi ya kufanya maandamano na mikusanyiko isiyo halali, wakitimua mbio mahakamani baada ya kufutiwa mashtaka kwa muda.
Wafuasi hao walifika katika Mahakama ya Hakimu
Mkazi Kisutu jana wakiwa na wadhamini wao wakati kesi hiyo ilipotajwa,
lakini upande wa mashtaka ukaieleza Mahakama kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka
(DPP) hana nia ya kuendelea na mashtaka dhidi yao.
Hata hivyo, Wakili wa Serikali, Joseph Maugo
alisema uamuzi huo wa DPP chini ya kifungu cha 91 (1) cha Sheria ya
Mwenendo wa Makosa ya Jinai haumaanishi kuwa hawezi kuwashtaki tena
wakati wowote atakapoona kuna haja ya kuwafungulia mashtaka.
Kutokana na hatua hiyo, Hakimu Emilius Mchauru anayesikiliza kesi hiyo aliridhia na kuamuru washtakiwa hao waachiwe huru.
Hata hivyo, lengo la upande wa mashtaka la
kuwafutia mashtaka ili kuwaunganisha katika kesi inayomkabili Mwenyekiti
wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba halikutimia, kwa kuwa mara tu
baada ya kuachiwa huru wafuasi hao walitimua mbio.
Dakika chache baadaye, Profesa Lipumba alipanda
kizimbani katika kesi yake na ndipo upande wa mashtaka ukaomba
kubadilisha hati ya mashtaka dhidi yake ili kuwaongeza wafuasi hao ambao
hata hivyo walikuwa wamekwishatoweka.
Baada ya Wakili Mwandamizi wa Serikali, Tumaini
Kweka kutoa ombi hilo, Wakili wa Lipumba, Peter Kibatala aliinuka na
kupinga hatua hiyo.
Alisema katika jalada la kesi hiyo wamewasilisha
hoja nne za kupinga mashtaka hayo na miongoni mwa hoja hizo ni kuhoji
uhalali wa hati ya mashtaka na mamlaka ya Mahakama ya Kisutu kusikiliza
kesi hiyo.
Alidai kuwa kutokana na pingamizi hilo haiwezekani
kubadili, kufuta au kuondoa mashtaka na kwamba ni lazima mahakama hiyo
ijiridhishe kwanza kama ina mamlaka ya kusikiliza mashtaka hayo kabla
haijaendelea.
Wakili Kweka alisisitiza kuwa maombi ya kubadili
hati ya mashtaka yako mahakamani kihalali na kwamba hayaendi katika
mzizi wa kesi ya msingi, kwa kuwa wanachoomba ni kuongeza tu washtakiwa.
Hakimu Mchauru alikubaliana na maombi hayo ya upande wa mashtaka na kuruhusu ubadilishe hati ya mashtaka.
Wakili Kweka wakati akiendelea kuita majina ya
washtakiwa hao, baadhi ya wafusi wa CUF waliofika kusikiliza kesi hiyo
walisikika wakisema kuwa washtakiwa hao hawakupo kwa kuwa waliondoka
baada ya kuachiwa.
Kutokana na hali hiyo, Wakili Kweka aliomba ridhaa ya mahakama aisome hiyo hati ya mashtaka kisha apeleke maombi ya kisheria mahakamani hapo kuwaita washtakiwa hao.
Hakimu Mchauru alikubaliana na maombi hayo na Wakili Kweka akaendelea kuwasomea mashtaka Lipumba na wenzake 30 ambao hawakuwapo.
Mashtaka
Katika mashtaka hayo, Wakili Kweka alidai kuwa
washtakiwa hao wote kwa pamoja walikula njama kwa nia ya kutenda kosa,
kufanya mkusanyiko usio halali, kupinga amri halali ya ofisa wa polisi
iliyowazuia kuandamana.
Alidai kuwa washtakiwa hao walitenda makosa hayo Januari 27, 2015 eneo la Temeke, jijini Dar es Salaam.
Wakili Kweka aliieleza mahakama kuwa upelelezi
bado haujakamilika. Kesi hiyo iliahirishwa hadi Machi 23, mwaka huu kwa
ajili ya kutajwa na mahakama ilitoa hati ya kuwaita washtakiwa hao
kufika mahakamani tarehe hiyo.
Waliotimua mbio
Washtakiwa waliotimua mbio mahakamani ni pamoja na
Shabani Ngurangwa (56), Shabani Tano au Kasakwa (29), Shabani Polomo
(40), Juma Mattar (54), Mohammed Kirungi (40), Athumani Ngumwai (40),
Shaweji Mohamed (39) na Abdul Juma (40).
Wengine ni Hassan Saidi (37), Hemed Joho (46),
Mohamed Mbarucu (31), Issa Hassani (53), Allan Ally (53), Kaisi Kaisi
(51), Abdina Abdina (47), Allawi Msenga (53), Mohamed Mtutuma (33) na
Salehe Ally (43).
Pia wamo Abdi Hatibu (34), Bakari Malija (43),
Abdallah Ally (32), Said Mohamed (40), Salimu Mwafisi, Saleh Rashid
(29), Abdallah Said (45), Rehema Kawambwa (47), Salma Ndewa (42),
Athumani Said (39), Dickson Leason (37) na Nurdin Msati (37).
0 comments:
Post a Comment