BARCELONA KUJA NCHINI

Author
 Patrick Kluivert
TIMU ya wachezaji nyota wa zamani wa Barcelona FC inatarajiwa kuja nchini kucheza mechi ya kirafiki ya kimataifa na wachezaji wa zamani wa Tanzania, Tanzania All Stars Machi 28 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
Mwakilishi wa wachezaji wa zamani wa Barcelona, Patrick Kluivert ambaye ni mchezaji wa zamani wa timu hiyo alisema jana jijini Dar es Salaam kuwa mechi hiyo itawahusisha wachezaji nyota wa Barcelona wakiwemo Edgar Davids, Gaiza Mandieta, Ludovic Giuly, Francesco Coco na wengine wengi waliopitia klabu hiyo kwa miaka tofauti.
Kluivert alisema kuwa kikosi chao kitakuja na wachezaji nyota ambao ni maarufu duniani na mechi hiyo itakuwa na ushindani mkubwa.
Alisema kuwa yeye ni mwenyeji sana Tanzania kwani huu ni ujio wake wa tatu na anaamini mashabiki wanaopenda soka watatoka uwanjani siku hiyo wakiwa na furaha.
“Ninafurahi kuja Tanzania kwa mara ya tatu, ni faraja kubwa pia kucheza hapa nchini kwa mara ya kwanza, naomba mashabiki wa soka wajae uwanjani siku hiyo kuona mpira wenye ushindani,” alisema Kluivert.
Mwakilishi wa Kampuni ya Prime Time Promotion inayoratibu mechi na ziara ya timu hiyo ya Barcelona, Stuart Kambona alisema kuwa madhumuni ya mchezo huo ni kudumisha uhusiano wa kibiashara ya mpira wa miguu baina ya Tanzania na Hispania, kutangaza utalii na kuendeleza mahusiano mazuri baina ya nchi hizo mbili.
Kambona alisema pamoja na kucheza soka siku hiyo, ujio wao pia utaitangaza nchi nje ya mipaka yake na kuleta fursa nyingi hapa nchini.
“Wachezaji wa Barcelona wanataingia nchini siku mbili kabla ya mechi na watakuwa zaidi ya 20, majina ya wachezaji wengine yatatangazwa baadaye, ila tunaomba wadhamini wajitokeze kufanikisha na kufaidika na mechi hiyo,” alisema Kambona.
Mwenyekiti wa Chama cha Soka cha Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), Almasi Kasongo aliwaomba mashabiki wa soka kujiandaa kuangalia mechi hiyo kwa kufika uwanjani.
Kasongo alisema kuwa DRFA imefarijika kwa ziara hiyo na kuiomba Prime Time Promotion kuhakikisha kuwa inapanua wigo kwa kuandaa mechi nyingi ambazo zitakuwa chachu ya maendeleo ya soka nchini.

0 comments:

Post a Comment