soma kisha badili fikra yako haraka

Author
Kama kuna mtu anayesema kuwa hana kitu cha kuandika basi hajafikiri kwa undani au ni mwongo. Kila binadamu ana kitu chema ndani yake. Ukishaandika vitu hivyo, angalia kama vitu vikifanywa na mtu baki, usiyemjua je utasema yeye ni mtu mbaya?
Kama siyo, kwanini unajiona usiyefaa na uliyejaa mabaya tu? Badala ya kutazama yale yaliyo mabaya na yakushindwa katika historia yako, tazama mafanikio.
Kila mmoja ana mafanikio ya aina fulani, hata kama ni madogo. Wengi wetu hatuchukui muda kujiuliza vyanzo vya mitazamo yetu. Ila mara tu utakapogundua kuwa tatizo sio lako wewe bali ni mazingira uliyokuziwa au aina ya wazazi uliokuwa nao, basi utaacha kujidharau.
Wako watoto wanaofurahia kupelekwa shule za bweni mbali na nyumbani, ila wako ambao hawapendi kabisa, lakini wanalazimishwa.
Hali hii hupandikiza ndani ya watoto hawa, upweke, hofu, msongo wa mawazo na kutokutulia (nazungumzia utulivu wa ndani) jambo ambalo huendelea hata katika utu uzima wao.
Wako wengi ambao tabia zao za leo zilianza kuharibikia katika shule za bweni mbali na wazazi kwa mfano tabia za kusagana au kuingiliana kinyume na maumbile.
Sisi tumeumbwa katika mifumo na vipindi mbalimbali, mara nyingine tuko chanya (watu wema, wazuri) na mara nyingine tunakuwa hasi (watu wabaya). Kama mtoto atakuwa akiambiwa kila wakati kuwa ‘kamwe huwezi kuwa na akili kama dada yako’ maneno haya hufanyika halisi kwake.
Je hujawahi kusikia mtu akisema: “Mimi sijui kuogelea”, “Sijui kama nitaolewa”, “Kamwe sitokaa niendeshe gari”, “Mimi sitokaa nijue Kiingereza” na “Mimi na kuimba ni tofauti.”
Haimaanishi kama watu hawa wangeanza kujifunza au kuzaliwa katika mazingira ya vitu hivi, wangevishindwa. Labda kuna sehemu mtu au watu fulani waliwasemea kutoweza au kushindwa na huo ukawa mwanzo wa kuwekewa kizingiti cha ujuzi ndani yao.
Wakati wowote mtu anapojisemea jambo au neno lililo baya, lisilojenga, lakushindwa, kama utalisema kwa sauti au utalifikiria akilini, katika hali yoyote ile jambo hili hulazimisha uhalisi wa maneno yale kuingia katika mfumo wa maisha yako na kutenda kazi kwa hiyo jifunze kukataa, kukanusha na jitahidi kutenda kinyume na zile sentensi mbaya juu yako.
Kama tunaamini utendaji wa kazi wa yale tunayojisemea au kusemewa vibaya basi hata yale tunavyojisemea au kusemewa vema hutenda kazi pia.
Amua kubadilisha yale unayojisema au yale unayosemewa. Badili yale yaliyo hasi (yakufeli) yawe chanya (yakuweza).
Kama hujiamini wewe mwenyewe wala hujithamini, basi utakubali kirahisi kila neno gumu, hutaweza kukabiliana na ushindani wa mtu au watu wenye tabia ngumu.
Kumbuka daima udhaifu huanzia kwako mwenyewe. Ukishajifunza kupunguza kujilaumu na kujipinga mwenyewe na kuboresha jinsi unavyojitazama basi utakuwa salama katika kukabiliana na maneno na matendo magumu toka kwa yeyote mwenye tabia ngumu.
Na kwa kuwa umejifunza vizuri kujielewa basi sasa waweza kuwaelewa vizuri zaidi wale wenye tabia ngumu. Sasa utaweza kuelewa kuwa kuna kitu kimemfanya au kimewafanya wawe vile walivyo.
Mara utakapoweza kumwonea huruma yeyote, haijalishi anatisha kiasi gani basi hawezi tena kukuathiri kwa vyovyote vile.
Kwa jinsi ujasiri wako unavyoongezeka, unaweza pia kuziweka katika matendo mbinu nyingine nyingi za kushughulika na watu wenye tabia ngumu.
Utajikuta unaweza kukabiliana nao na pia kuchukuliana nao katika mazingira tofauti na pia hata katika nyakati ambazo hutakuwa unafanya vizuri katika jambo fulani, hautajilaumu na kujishusha, bali utajisifu kwa kukazana na kujitahidi hata kama haukubahatika.

0 comments:

Post a Comment