Jeshi la Polisi mkoani Katavi limewakamata watu wawili kwa
tuhuma za kukutwa na meno ya tembo vipande 22 vyenye uzito wa
kilogramu 46 na thamani ya Sh157 milioni wakati wakiyasafirisha kwa
basi kutoka Mpanda kwenda Mkoa wa Kigoma
Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi wa Mkoa wa
Katavi, Rashid Mohamed aliwataja watuhumiwa hao Justine Baruti
(Zolros) (39) Mkazi wa Kijiji cha Ivungwe makazi ya Wakimbizi ya
Katumba Wilaya ya Mlele Mkoa wa Katavi na Bonifaphace Hoza (40) Mkai
wa Kalele Wilaya ya Kasulu Mkoa wa Kigoma. Alisema watuhumiwa hao
walikamatwa na askari wa doria juzi asubuhi katika eneo la stendi ya
mabasi ya Mpanda.
Mohamed alisema askari hao baada ya kupekua
mizigo ya mtuhumiwa Justine walimkuta akiwa na meno ya tembo vipande
15 vyenye uzito wa kilogramu 33 vyenye thamani ya Sh90 milioni sawa
na tembo wanne waliouawa vikiwa vimehifadhiwa ndani ya mabegi makubwa
mawili.
Alisema baada ya Justine kupekuliwa na kukutwa
na meno hayo ya tembo mtu mwingine ambaye inaonyesha alikuwa na
mtuhumiwa alitupa begi lake la rangi ya ugoro na kisha kutokomea
kusikojulikana.
Mohamed alisema baada ya polisi kufanya ukaguzi
wa kina kwenye basi walilokuwa wakisafiria watuhumiwa, walifanikiwa
kumkamata mtuhumiwa Bonifaphace Hoza akiwa na begi moja alilokuwa
amelihifadhi chini ya siti ndani yake likiwa na vipande saba vya
meno ya tembo vyenye uzito wa kilogramu 13 vyenye thamani ya
Sh67,500,000 ambayo ni sawa na tembo watatu waliouwawa.
Alisema watuhumiwa hao wawili watafikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.
Hata hivyo, baadhi ya wananchi waliozungumza na
mwandishi wa habari hizi wamedai kuwa ipo haja kwa Serikali kupitia
Wizara ya Maliasili na Utalii kuchukua hatua za makusudi ili kudhibiti
biashara hiyo haramu ambayo baadhi ya watumishi wa Serikali ni wazi
watakuwa wakishiriki kwa kuwa vitendo hivyo vimeshamiri na udhibiti wake
kama vile umeshindikana mkoani humo
0 comments:
Post a Comment