Mtu mmoja mwanaume ambaye jina lake halikufahamika mara moja,
amefariki dunia baada ya kulipukiwa na bomu wakati akijaribu kuwarushia
polisi waliokuwa doria wakati wa Sikukuu ya Krismasi katika Kata ya
Majengo, mjini Songea.
Baada ya bomu hilo kulipuka, lilimpasua tumbo mtu
huyo na kumkata mkono wa kushoto ambao haukuonekana eneo la tukio. Pia
liliwajeruhiwa polisi wawili.
Polisi mkoani Ruvuma ikishirikiana na makachero
kutoka makao makuu ya jeshi hilo, imesema linawasaka watu wengine watatu
ambao wanasadikiwa kujihusisha na ulipuaji mabomu.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye ukumbi
wa mikutano wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Ruvuma, Naibu Kamishna wa Jeshi
la Polisi, Kaimu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jina nchini
(DCP), Diwani Athumani alisema kuwa tukio hilo limetokea jana saa 1.30
usiku katika Mtaa wa Kotazi uliopo kata ya Majengo Manispaa ya Songea.
Alieleza kuwa wakati polisi wakiwa katika doria
kulitokea mlipuko wa kitu kinachodhaniwa kuwa ni bomu, lililotengenezwa
kienyeji na kuwajeruhi askari wa wawili.
DCP Athumani aliwataja polisi waliojeruhiwa PC
Mselem mwenye namba G 7903 ambaye alijeruhiwa mkono wake wa kushoto na
alitibiwa na kuruhusiwa na mwingine PC Mariam mwenye namba WP. 8616
alijeruhiwa kwenye bega la mkono wa kushoto na amelazwa katika Hospitali
ya Rufaa ya Mkoa Ruvuma (HOMSO) akiendelea kupata matibabu.
DCP Athumani alieleza kuwa wahalifu hao
watakamatwa kirahisi kwa kuwa baada ya mwenzao kulipukiwa na bomu hilo
walijaribu kutorosha mwili wake ili kupoteza ushahidi, lakini
walishindwa baada ya polisi wengine kufika eneo la tukio hilo mapema.
“Wahalifu hao waliuvuta mwili wa mwenzao kutoka
katika eneo la tukio kwa umbali wa mita zisizopungua 80 na 90 kwa lengo
la kutaka kupoteza ushahidi, lakini waliwahiwa na polisi wengine wa
doria na kuuacha mwili na kutokomea kusikojulikana,” alisema DCP
Athumani.
Alisema kuwa kikosi chache kimejipanga kukabiliana
na ongezeko la matukio ya mabomu nchini na hususan mkoani humo, ambapo
hilo ni tukio la tatu kwa mwaka huu.
Hata hivyo, amewaomba wadau mbalimbali wakiwamo
viongozi wa dini, wanasiasa, wazee, makundi mbalimbali ya kijamii
pamoja na waandishi wa habari kuwa kitu kimoja katika kuwafichuwa
waharifu hao ili matukio hayo yasiweze kujirudia tena hususan Mkoa wa
Ruvuma.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Said
Mwambungu aliyetembelea eneo la tukio alisema kuwa waharifu hao wanaishi
kwenye jamii hivyo ni vyema kuwafichua ili mkoa uendelee kuwa na amani.
“Nimeumizwa sana na vitendo hivi vya ulipuaji
mabomu, naomba wananchi tuwafichue watu wanaofanya vitendo hivi kwani
tunaishi nao kwenye jamii tuache kuyafumbia macho matendo haya mabaya
ambayo ni hatari kwa jamii,” alisema Mwambungu.
Naye Mganga Mkuu Mfawidhi Hospitali ya Mkoa wa Ruvuma, Dk Benedkto Ngaiza amethibitisha kupokea mwili mmoja wa mtu ambaye amekufa na utumbo ukiwa umetoka nje. Pia majeruhi wawili ambao ni polisi na kwamba mmoja alitibiwa jana na kuruhusiwa huku mmoja akiwa amelazwa wodi ya majeruhi namba mbili akiendelea kupatiwa matibabu na hali yake inaendelea vizuri.
Naye Mganga Mkuu Mfawidhi Hospitali ya Mkoa wa Ruvuma, Dk Benedkto Ngaiza amethibitisha kupokea mwili mmoja wa mtu ambaye amekufa na utumbo ukiwa umetoka nje. Pia majeruhi wawili ambao ni polisi na kwamba mmoja alitibiwa jana na kuruhusiwa huku mmoja akiwa amelazwa wodi ya majeruhi namba mbili akiendelea kupatiwa matibabu na hali yake inaendelea vizuri.
0 comments:
Post a Comment