TANZANIA imeporomoka nafasi tatu kwa ubora wa viwango vya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) vilivyotolewa jana. Kwa mujibu wa tovuti ya Fifa, Tanzania sasa ni ya 107 kutokana na nafasi ya 104 iliyokuwa ikishikilia mwezi uliopita.
Uganda ni ya 76 katika nchi za ukanda wa Afrika Maskariki na Kenya inashika nafasi ya 116. Katika nchi mwanachama wa Baraza la vyama vya soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa), Rwanda ndio inaongoza kwa kushika nafasi ya 72, Ethiopia ya 102, Sudan ya 112, Burundi inashika nafasi ya 124 Sudan Kusini 189, Eritrea ya 202, Somalia 204 na Djibouti 206.
Kwa upande wa mabingwa wapya wa Afrika Ivory Coast wamepanda kileleni mwa orodha hiyo kwa nafasi nane na sasa inashika nafasi ya 20 baada ya kutwaa taji la Kombe la Mataifa Afrika, Afcon mwishoni mwa wiki iliyopita.
Equatorial Guinea ambao walikuwa wenyeji wa michuano ya Afcon mwaka huu, wameingia kwenye 50 bora kwa mara ya kwanza.
Nchi hiyo imevuka kwa nafasi 69 na kukaa kwenye nafasi ya 49 pamoja na Congo baada ya kucheza nusu fainali za michuano hiyo. Algeria imebaki kuwa timu bora Afrika ikishika nafasi ya 18.
Tembo wa Afrika wanashika nafasi ya pili kwa upande wa Afrika nyuma ya vinara Algeria ambao iliwafunga kwenye robo fainali za Afcon. Washindi wa pili wa michuano ya Afcon Ghana wamesogea kwa nafasi 12 na sasa wanashika nafasi ya 25.
Timu iliyoporomoka kwa kiasi kikubwa mwezi huu ni Libya iliyoporomoka kwa nafasi 35 na kuangukia 113. Kinara wa orodha hiyo ni Ujerumani kama kawaida imeendelea kushika nafasi ya kwanza ikifuatiwa na Argentina, Colombia, Ubelgiji na Uholanzi.
Brazil inashika nafasi ya sita na ya saba iko Ureno, Ufaransa ni ya nane, Uruguay ya tisa na Hispania inafunga pazia la timu kumi bora.
0 comments:
Post a Comment