Mtibwa Sugar choka mbaya

Author

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Bara Azam jana waliiporomoshea Mtibwa Sugar kipigo cha mbwa mwizi baada ya kuifunga mabao 5-2 katika mechi iliyochezwa kwenye uwanja wa Azam Complex Chamazi.

Kipigo hicho ni cha kushtusha kwa Mtibwa Sugar iliyoanza vizuri ligi ya msimu huu, kwa kukaa kileleni mwa msimamo muda mrefu.

Karamu ya mabao kwa Azam ilianza katika dakika ya 20 ambapo Kipre Tchetche alifunga bao la kuongoza baada ya kuunganisha krosi ya Brian Majegwa na kuujaza mpira wavuni.

Dakika sita baadae, Frank Domayo aliiongezea Azam bao la pili akiunganisha pasi ya Majegwa tena. Bao hilo liliwafanya Azam wazidi kuonana na kufanya mashambulizi ya mara kwa mara langoni mwa Mtibwa Sugar.

Mtibwa Sugar ilijaribu kujibu mapigo katika dakika ya 33 ambapo ilipata bao la kwanza likifungwa na Mussa Nampaka kwa shuti kali baada ya kupokea pasi ya Ally Shomari aliyeingia uwanjani sekunde chache kuchukua nafasi ya Henry Joseph.

Hata hivyo ikijipanga kurudisha bao lingine, Mtibwa ilijikuta ikipachikwa la tatu kupitia kwa Didier Kavumbagu katika dakika ya 40 akiunganisha krosi ya Salum Abubakar, matokeo yaliyodumu mpaka mapumziko.

Timu zote zilikianza kipindi cha pili kwa mabadiliko ambapo Mtibwa Sugar ilimtoa Ally Lundenga na kumuingiza Vincent Barnabas na Azam ilimtoa Kipre Balou na nafasi yake kuchukuliwa na Mudahir Yahya.

Mabadiliko hayo yalijibu haraka kwa Azam ambapo dakika ya 59 Domayo aliifungia Azam bao la nne kwa kazi nzuri ya Kavumbagu. Ame Ally akaifungia Mtibwa bao la pili dakika chache baadae.

Zikiwa zimesalia dakika tatu kabla mchezo kumalizika, Tchetche aliifungia Azam bao la tano akiunganisha pasi ya Hamisi Mcha. Kwa ujumla katika mechi ya jana Mtibwa Sugar walionekana kupoteana karibu muda mwingi wa mchezo huku wakionekana kucheza bila malengo.

Ushindi huo unaifanya Azam irejee kileleni mwa msimamo wa ligi ikiwa na pointi 25 baada ya kucheza mechi 13 sawa na Yanga inayoshika nafasi ya pili sasa baada ya kuzidiwa kwa wastani wa mabao.

Kikosi cha Azam: Aishi Manula, Shomari Kapombe,Erasto Nyoni/ John Bocco, Said Morad, Serge Wawa, Kipre Balou/ Mudahir Yahya, Kipre Tchetche, Frank Domayo, Didier Kavumbagu/ Khamis Mcha, Salum Abubakar, Brian Majwega.

Mtibwa Sugar: Saidi Mohammed, Andrew Vincent, Majaliwa Mbaga, Ally Lundenga, Salim Mbonde, Shaaban Nditi, Ramadhan Kichuya, Mussa Nampaka, Ame Ally, Henry Joseph/ Ally Shomari, Mussa Mgosi/ Abdallah Juma

0 comments:

Post a Comment